Featured Post

UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI: MRADI WENYE FURSA KEDEKEDE WATANZANIA WANAPASWA KUZICHANGAMKIA

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli (kushoto) na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga Tanzania.

Hivi Karibuni, Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda kwa pamoja waliweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga Tanzania. Katika Makala hii pamoja na mambo mengine Mwandishi Said Ameir wa Idara ya Habari- MAELEZO anaeleza kwani nini mradi huu ni kipimo cha utayari na ujasiri wa watanzania katika kuchangamkia fursa.

Mradi huu unaojulikana kama Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unatekelezwa kwa ubia kati ya washirika wa sekta binafsi na sekta za umma za nchi za Tanzania na Uganda.

Washirika hao ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Petroli ya Uganda (UNOC), Kampuni ya Mafuta ya Total ya Ufaransa, Kampuni ya TULLOW yenye makao makuu yake London nchini Uingereza na Kampuni ya China National Offshore Oil Company (CNOOC).

Bomba ambalo litagharimu dola za kimarekani 3.5 bilioni, sehemu yake kubwa yaani kilomita 1,115 kati ya kilomita 1,445 litajengwa katika ardhi ya Tanzania na kupita mikoa 8, wilaya 24 na vijiji 184.

Kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa, mradi huu wakati wa ujenzi na utakapokamilika, utatoa na fursa nyingi za kiuchumi ambazo zitasaidia sana kuchangamsha shughuli za kiuchumi hivyo kuchangia ukuaji uchumi na kuinua kiwango cha maisha ya watanzania kwa namna mbalimbali.

Mradi huu ni mfano wa ushirikiano kati ya nchi za Tanzania na Uganda na kwa upande mwingine ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta za umma katika nchi hizi. 
Katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake, mradi huu utahitaji ushiriki wa sekta binafsi katika nchi zote mbili na wakati mwingine hata taasisi nyingine za umma ambazo zinatoa huduma zitakazohitajika na mradi.

Kwa hiyo, wakati tukisifia kuwa ni mfano wa mradi wa ubia wa sekta ya umma na sekta binafsi katika nchi zetu, watanzania hawana budi kuelewa kuwa wana wajibu mkubwa wa kuzitumia vyema fursa za mradi huu.

Kwa Tanzania, mradi huu unaweza kuonesha picha halisi ya ushirikiano wa sekta hizo kwa kuzingatia namna makampuni na taasisi za humu nchini zitakavyoweza kushiriki na kufanikisha mradi huu.

Kwa maana nyingie ni mradi ambao unaweza kutumika kupima utayari, umakini, uwezo na ujasiri wa watanzania katika kuchangamkia fursa za kiuchumi.

Kama alivyoeleza Rais Magufuli wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi kuwa katika mradi huu, Serikali imesamehe mambo mengi ili uweze kutekelezwa kwa kuishirikisha Tanzania. Wataalamu wa nchi walichambua na kupembua hadi kubaini kuwa kusamehe huko kutafidiwa na fursa nyingi zitakazoletwa na mradi huu.

Kwa maana hiyo bila ya watanzania kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha wanazitumia kadri itakavyowezekana fursa hizo uamuzi huo wa Serikali kusamehe hivyo ilivyovisamehe hautakuwa na maana yeyote.

Kuja kwa mradi huu Tanzania, watanzania hawana budi kuipongeza Serikali chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa kwa kutumia ushawishi wa kisiasa, kidiplomasia, uchumi na ukaribu wa viongozi wa nchi hizo mbili pamoja na hoja nyingine hadi kufanikisha mradi huu kuja Tanzania.

Jitihada hizi ni kielelezo cha dhamira ya kweli iliyonayo Serikali ya Awamu ya Tano ya kutafuta kila aina ya fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kutimiza ahadi zake kwa watanzania ya kujenga Tanzania yenye uchumi imara.

Serikali imejitwika mzigo mkubwa wa kushiriki katika kutekeleza mradi huu mkubwa wa aina yake lakini imefanya hivyo kwa kuamini kuwa watanzania wako tayari na wako imara kuupokea kwa hali na mali.

Imeelezwa mara kwa mara kuwa mradi huu utaliingizia taifa mapato makubwa, utaleta tekinolojia na utalaamu na fursa za kiuchumi ambazo watekelezaji wake kwa kiwango kikubwa ni kutoka sekta binafsi. Kwa mnasaba huo, Serikali hapa imefanya zaidi ya wajibu wake ambao ni wa kujenga mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji.

Wale wahenga wa Cambrigde walisema“give us the tools and lets finish the job” na hivi ndivyo ilivyofanya Serikali kwa mradi huu. Imeleta mradi na kufungua fursa tele ambazo watanzania wanapaswa kuzitumia kujenga kiuchumi wao binafsi na uchumi wa taifa.

Haitakuwa na maana hata kidogo katika ngazi ya serikali na katika ngazi ya Mtanzania mmoja mmoja kufika wakati fursa za mradi huu kuchukuliwa na wageni kwa sababu zozote na katika mazingira yeyote yale. Ikifikia hatua hiyo watanzania watakuwa wamewaangusha viongozi wao.

Hii kutokana na mazingira ambayo Serikali imeyaweka kuwawezesha watanzania kushiriki katika sekta ya mafuta na gesi asilia. Mbali ya kupitisha Sheria ya Local Content Act ya 2015 ambayo inasisitiza ushiriki wa watanzania lakini zaidi dhamira ya kweli ya kisiasa iliyonayo uongozi wa Serikali ya kuhakikisha kuwa watanzania wanafaidika ipasavyo na mradi huu.

Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa baadhi ya Taasisi za Serikali na za sekta binafsi zimeshaanza maandalizi au zimejitokeza kuwaandaa watanzania kuchangamkia fursa hizo na kuhakikisha wanazitumia vyema.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS) ambayo inawakusanya pamoja watoa huduma katika sekta hiyo ambapo lengo lake kubwa ni kuhakikisha kuwa fursa za mradi huo zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya muda mfupo na mrefu ya watanzania.

ATOGS, kama taasisi nyingine zitakazoelezwa baadae, imeonesha mfano wa utayari kwa kuwa na mpango mkakati wake ambao unalenga kuwawezesha watoa huduma wa humu nchini wanapata fursa hizo kwa kuwasaidia kwa namna mbali mbali tangu hatua za awali za kuwania fursa hizo hadi utekelezaji wake.

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Abdulsamad Abdulrahim katika moja ya mikutano na waandishi wa habari alisema taasisi yake imejipanga kuwajengea uwezo watoa huduma na kutoa wito watoa huduma hao kwa waliokuwa bado hawajajiunga wajiunge na taasisi hii kwa minajili ya kufaidika na uwezeshaji wao.

Halikadhalika, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) nalo linaeleza kuwa limejidhatiti kuhakikisha kuwa watanzania watakaobahatika kupata fursa za kutoa huduma katika mradi huo hawashindwi kwa kukosa fedha za kutekeleza kandarasi zao.

“Hatutaki kusikia mtanzania amekosa fursa hii kwa sababu ya kukosa fedha …ukibahatika njoo kwenye Baraza tutakushauri… Serikali ina mifuko 17 yenye fedha za kutosha kukuwezesha” anaeleza Mkurugnezi wa uwezeshaji wa NEEC Bwana Edwin Chrisant.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Bwana Godfrey Simbeye aliwaambia waandishi wa habari kuwa taasisi yake imejipanga kuhakikisha kuwa mikataba ya kandarasi itakayofikiwa inazingatia maslahi ya pande zote na utekelezaji wake unafanyika kulingana na vipengele vya mikataba.

Dhamira hizi zilizoelezwa na taasisi hizi muhimu nchini, hapana shaka yoyote kuwa ni habari njema inayoashiria matumaini makubwa na kuonesha sasa watanzania wameamka na wamedhamiria kujenga Tanzania mpya kwa kila mmoja kwa nafasi yake kuyatumia mazingira yaliyopo kujenga uchumi wa taifa.

Kama kweli taasisi hizi zitatekeleza yale ziliyojipangia ikiwemo kuwapatia watoa huduma msaada wa kitaalamu, huduma za kisheria, kifedha, viwango na vigezo katika manunuzi, utaalamu, kuwaunganisha na wabia, kuwajengea uwezo vijana wasomi ili waweze kushika nafasi zitakuwa zimetoa msaada mkubwa kwa nchi.

Kwa hakika mradi huu kama ilivyoelezwa awali utakuwa kigezo muhimu kupima utayari, umakini na uwezo wa sekta binafsi kuchangamkia fursa zinapotokea na mafanikio ya ushiriki wa sekta hiyo huenda ukawa mwanzo mzuri wa kuupa mgongo utamaduni ulizoeleka wa watanzania kulalamika hususan kuilalamikia Serikali kuwa haiwapi fursa kama hizi.

Wahenga walisema “shike shike na mwenyewe nyuma” kwa hili Serikali zimefanya wajibu wake sasa mpira uko kwa wadau katika sekta binafsi kuucheza kwa zitumia fursa na ni vyema kukumbuka kuwa “mso matendo hula uvundo” hivyo watanzania wachangamkie fursa wasije wakajikuta karamu imekwisha ‘wakaramba vyungu.

 Ni vyema pia kutanabahisha kuwa fursa za mradi huu haziko kwa watoa huduma kama hao pekee ambao wao ni wafanyabiashara na wataalamu ambao tayari wanajielewa, wana uwezo na wako katika sekta hiyo hivyo tunaweza kusema wana angalau uzoefu.

Lakini ukweli hi kuwa fursa za mradi huu zimetapakaa kila mahala katika ngazi mbali mbali kuanzia wakulima wa jembe la mkono, wafugaji wadogo wadogo, mafundi mchundo, hadi vibarua wa ujenzi. Hivyo taasisi zinazohusika zinapaswa pia kuliangalia kundi hili kubwa na kuhakikisha linashiriki vyema.

Hii ni kwa sababu, inapozungumziwa ajira elfu kumi na ajira nyingine zaidi ya elfu thelathini nyingi zinawagusa watanzania wa kundi hili. Ikumbukwe kuwa kundi hili ambalo ndilo litakalokuwa karibu na mradi ndilo litakalokuwa la kwanza kulalamika pindi litakapokosa fursa na kujikuta halina namna ya kushiriki na kufaidika.

Utekelezaji mzuri na wenye ufanisi wa mradi huu kwa kushirikisha sekta binafsi nchini utakuwa kigezo cha kufungua milango kwa miradi mingine mikubwa ya aina hii humu nchini.

Watanzania hawana budi kumpongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kujenga Tanzania Mpya yenye matumaini mapya. Hakika Tanzania yenye uchumi wa kati na ya viwanda inawezekana, kama kila mmoja atatimiza wajibu wake.

Comments