- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Said Ameir –
MAELEZO
Agosti 15, 2017 -
Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri amesifu
ushirikiano kati ya taasisi za Tanzania na Misri zinazoshughulikia mapambano dhidi
ya rushwa na kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuonesha mfano wa uongozi
bora unaopambana na maovu katika nchi yake.
“Nampongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za
kupambana na rushwa na ufisadi na huo ni mfano wa sifa za uongozi bora”
alieleza Rais Al Sisi wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar
es salaam.
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania
(TAKUKURU) na Taasisi ya Udhibiti wa Utawala ya Misri (Administration Control
Authority of Egypt) zimekuwa na ushirikiano wa karibu kwa kubalidilishana
utaalamu, uzoefu na mbinu katika kutekeleza majukumu yao.
Katika mkutano, huo ambao uliofanyika mara baada
ya kumalizika mazungumzo rasmi kati ya nchi hizo, Rais Al Sisi alieleza dhamira
ya nchi yake ni kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuunga mkono jitihada
za kuleta amani barani Afrika na kuendelea kuwa na msimamo mmoja katika masuala
ya kimataifa.
“Tunampongeza Rais Magufuli na Tanzania kwa
mchango wake mkubwa katika kutafuta amani barani Afrika hasa katika eneo la Maziwa
Makuu” Rais Al Sisi alisema na kumpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu
Benjamin Mkapa kwa jitihada zake za usuluhishi katika mgogoro wa Burundi.
Rais huyo ambaye alikuwa nchini kwa ziara rasmi
ya siku mbili, ameeleza kutambua mzigo mkubwa inaoubeba Tanzania katika
kushughulikia migogoro ikiwa ni pamoja na kuhudumia maelfu ya wakimbizi kutoka
katika nchi mbalimbali.
Katika mkutano ambao ulihutubiwa pia na mwenyeji
wake Rais Magufuli, Rais huyo wa Misri alieleza utayari wa nchi yake kuendeleza
na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania kwa kuhimiza kubuni na kutekeleza
miradi ya pamoja, kuongeza biashara na uwekezaji pamoja na kubadilishana
wataalamu.
”Misri na Tanzania hatma yao ni moja,
tutaendelea kushirikiana kwa hali na mali na kwa kuwa tuna dhamira,
matumaini yetu makubwa ni kufanikiwa” Rais Sisi alisisitiza.
Kabla ya mkutano huo na wanahabari, Rais wa
Misri alikuwa na mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Rais Magufuli na baadae
kuhudhuria mazungumzo rasmi ya mashauriano kati ya Tanzania na Misri.
Comments
Post a Comment