- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Nikaelekea chumbani kwangu. Niliona chumba cha Leila kikiwa
kimefungwa na nikasimama kugonga. Hakukuwa na jibu. Nikajaribu kufungua mlango,
lakini ulikuwa umefungwa. Nikagonga tena, likasikiliza, baada ya kutosikia
chochote, nikaamua kwenda chumbani kwangu.
Ilikuwa ni mapema mno kufanya chochote hivyo nikavua jaketi langu,
tai na viatu na kujilaza kitandani. Nikajaribu kuwaza kidogo lakini sikufika
popote, halafu likapitiwa na usingizi.
Ilikuwa ni saa nne wakati niliposhtuka kutokana na mtu aliyekuwa
akigonga mlangoni kwangu. Nikainuka haraka na kufungua mlango.
Kijana wa Kichina akainama, akiwa anatabasamu, na kuelekeza niende
ukumbini. Nilivaa viatu vyangu na kumfuata hadi mapokezi. Mhudumu mzee akanipa
mkonga wa simu.
Alikuwa Inspekta Mkuu MacCarthy.
“msichana huyu uliyeniambia,” akasema, “Ulisema umemnunulia pete
ya jade jana usiku?”
Nikaganda kwa muda.
“Ndiyo . . . ilikuwa ni ya kulingana na jade.”
“Unaweza kuchukua teksi hadi kituo cha polisi cha Chatham Road?
Kiko upande wa Kowloon. Wana msichana pale – anaweza kuwa huyo unayemzungumzia.
Amevaa pete ya jade.”
“Amekufa?” nikauliza, nikijua mishipa yangu ya tumbo ilikuwa
imebana.
“Oh, kitambo.” Niliweza kuhisi harufu ya moshi wa tumbaku lake
kupitia kwenye simu. “Itasaidia kama utakwenda kumtambua. Muulizie Sajini
Hamish.”
“Mskochi mwingine?”
“Ni sahihi kabisa. Waskochi wengi wako kwenye jeshi la polisi.”
“Pengine ni jambo jema kwa Scotland,” nikakata simu.
Dakika arobaini baadaye, nikapandisha ngazi za kituo cha polisi
cha Chatham Road. Ndani ya ukumbi tu kulikuwa na ubao mkubwa ukutani wenye
picha za kutisha hamsini za maiti za wanaume na wanawake wa Kichina waliokutwa
mto Straits au mitaani huku kukiwa na maelezo ya Kiingereza na Kichina ya
kuomba watambuliwe.
Sajini wa mapokezi akanielekeza kwenye ofisi ndogo ambako kijana
mdogo mwenye uso mng’avu na mtazamo wa kipolisi alikuwa akikagua faili.
Aliitikia wakati nilipoingia na kujitambulisha. Alisema jina lake alikuwa
Sajini Hamish.
“Kuna maiti ambayo ninapaswa kuitambua,” nikamweleza.
Akachukua mfukoni mwake mtemba. Polisi wa Hong Kong walionekana ni
wavuta mitemba. Nikamtazama akiujaza tumbaku, huku macho yake ya kijani
yakiniangalia bila hamu yoyote.
“Ni sahihi. Inspekta Mkuu anadhani unaweza kumtambua. Aliopolewa
kwenye Mto Straits jana usiku majira ya saa nane. Hakuna chochote kilichosalia.
Inawezekana aliingia kwenye mojawapo ya injini za boti kwa namna alivyo.”
Nilihisi jasho jembamba likivuja mgongoni kwangu.
Akainuka.
“Hawa wanaharamu kila siku wanauana,” alisema kimazungumzo. “Kila
siku tunaokota maiti si chini ya sita. Wachina wanaonekana hawayathamini maisha
yao.”
Tulipita kwenye uchochoro, katika eneo la wazi hadi tukafika
mochwari. Kulingana na rundo la karatasi na fomu zilizojazwa, inaonekana
biashara ya kupokea maiti ilikuwa imepamba moto asubuhi hii.
Aliniongoza hadi kwenye meza, ambayo ilifunikwa na shuka zito la
plastiki. Akainua upande mmoja wa shuka, akachungulia na kutoa kono mdogo ulio
na pete ya jade.
“Nimekula mayai na nyama wakati wa kifungua kinywa,” alisema. “Kama
utamtambua kwa pete, inaniokoa nisitapike.”
Niliitazama pete na vidole vidogo vyembamba. Ilikuwa ni pete
niliyomnunulia Leila.
“Hiyo ndiyo pete haswa,” nilisema, na nilijihisi vibaya mno.
Akaurudisha mkono ndani ya shuka.
“Sawa, nitamwambia Inspekta Mkuu.”
Nikasogea mbele na kulifunua shuka la plastiki. Nikatazama kwa
muda mrefu kuhusu mabaki ya aliyekuwa Leila. Bora hata nisingetazama, lakini
nilipaswa kumuaga. Nikalirudisha shuka mahali pake.
Nikakumbuka jinsi alivyopumua kwa furaha baada ya kula kile
chakula cha kumbukumbu. Nikakumbuka umbile lake kwa nyuma wakati alipokuwa
amenitangulia. Sikuwa nimemfahamu kitambo, lakini tabia zake zilikuwa
zimenifurahisha. Nikahisi nimempoteza mtu muhimu sana kwangu.
Kulikuwa na kachero aliyekuwa akinisubiri upande wa pili wa Feri.
Alikuwa bonge la mtu mwenye uso mpana ambaye aliitwa MacPherson: ilionyesha
hakuna mwisho wa hawa Waskochi. Akanirejesha hotelini kwenye gari ya polisi.
Itaendelea
kesho…
Comments
Post a Comment