- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
“Simfahamu: ni jamaa tu. Ungependa risasi iingie wapi, Buster? Mimi
ni mtaalamu wa bastola. Risasi ya kichwa ndiyo inayoondoa uhai haraka, lakini
chagua mwenyewe.”
“Huyo jamaa alikuwa anafananaje?” nikamuuliza kwa shauku yenye
hofu.
Akainyoosha bastola kuelekea kichwa changu.
“Huna haja ya kumhofia,” akasema, na kulikuwa na sauti ya kikatili.
“Jihurumie mwenyewe.”
“Dola mia tano hazitoshi. Ninaweza kukuongezea hizo,” nikamwambia.
“Unaonaje ukiiweka bastola hiyo pembeni name nikupatie dola elfu moja?”
Akanibeua.
“Ninapoweka mkataba, lazima niutekeleze,” akasema.
Simu ikaita ghafla.
Kwa sekunde ishirini zilizopita nilikuwa najipongeza mwenyewe. Kengele
ya simu ikamshtua na akageuka kuitazama simu.
Nikamrukia pale pale, kichwa change kikilenga uso wake, mikono
ikiifuata bastola.
Nilimtwanga kama roketi: kichwa change kikampasua mdomo na pua. Mikono
yangu ikaifikia bastola, nikaipiga ikageukia pembeni huku ikifyatuka na kutoa
mlio hafifu. Mikono yake ilikuwa imara mno.
Yeye na mimi na kiti tukaangukia nyuma kwa kishindo kikubwa.
Lakini alikuwa ngangari kweli kweli. Sikuweza kuichukua bastola
mkononi mwake. Kidogo alionekana kushangazwa na kilichotokea, vinginevyo
angenipiga risasi, lakini nilifanya haraka kumlalia na kumtwanga shingoni kwa
karate kali iliyomlegeza. Mkono ukalegea na nikaichukua bastola. Kisha
akanipiga katikati ya macho kwa ngumi nzito ambayo sijapata kukutana nayo
maishani. Ilikuwa nzito kama nyundo.
Nikaiachia bastola. Kwa sekunde chache nilichoweza kukiona ni
nyota zikicheza mbele yangu. Nilikuwa natambaa kwa magoti wakati naye
akihangaika kuinuka kutoka sakafuni, damu ikivuja kutoka puani na mdomoni. Alirusha
teke usoni mwangu, lakini halikuwa na nguvu. Nilikuwa nimemuumiza, na chokoraa
kama huyu akiumizwa, anaumizwa hasa.
Nikalipangua teke hilo kwa mkono wangu, nikabingirika kutoka kwake
na kusimama. Tukatazamana. Bastola ilikuwa sakafuni katikati yetu.
Aliniungurumia, lakini alikuwa mjanja kwa sababu hakuinama
kuchukua bastola. Alijua nitamfinyanga kabla hajaifikia: badala yake akaja kasi
kama nyati aliyejeruhiwa. Nilimtandika ngumi moja nzito usoni wakati akinivamia
na sote tukadondoka chini na kudondosha makopo mawili ya rangi ya Rome ambayo
nilikuwa nimeyaleta nyumbani kama kumbukumbu wakati nikiwa katika kazi moja.
Nilimtwanga kichwa usoni mwake tena na kumtandika ngumi sita za
nguvu tumboni, huku nami nikipigwa ngumi mbili kichwani zilizofanya ubongo
wangu uzubae kidogo. Akarudi nyuma. Ngumi mbili za tumboni zilikuwa
zimemlainisha. Alionekana mnyama sasa. Nikamrukia, nikamtwanga tena. Aliyumba upande
na nikaona amesehika kisu mkononi.
Tukatulia tukitazamana. Alikuwa ametepeta. Kichwa change kilikuwa
kimeuharibu uso wake na damu zilimvuja mno, lakini bado alikuwa na nia ya kuua.
Mtazamo wa macho yake na kisu mkononi vilinitisha.
Nikarudi nyuma.
Aliunguruma na kunijia kwa kasi ya ajabu.
Bega langu likagonga ukuta. Nilifua koti langu haraka na kwa kasi nikajifunga
kwenye mkono wa kushoto. Alinijia kwa kasi kama nyoka anayetaka kugonga. Nilikishika
kisu kwa kutumia mkono wenye koti na kumtandika ngumi shavuni kwa mkono wa
kulia. Ilikuwa ngumi nzuri, yenye nguvu na madhara. Rangi nyeupe kwenye macho
yake ilionekana na akarudi nyuma, akipiga magoti. Kisu kikadondoka mkononi
mwake. Nikakipiga teke kikaenda upande mwingine wa sebule, halafu nilipojiweka
sawa, akaanza kuangukia mbele. Nikamtandika ngumi nyingine shavuni iliyonichubua.
Akadondoka chini kama gunia la pamba, akigonga kidevu chake sakafuni.
Nikaegemea ukuta, nikitweta. Nilikuwa nimechoka balaa. Nilitandikwa
ngumi nzito ambazo sijawahi kupigwa na zilikuwa zimeniachia maumivu makali. Ilikuwa
kana kwamba baadhi ya maisha yangu yalikuwa yameondoka mwilini.
Mlango ukafunguliwa na polisi wawili wakaingia, bunduki mikononi.
Huwezi kuanzisha aina hii ya vita chumbani mwangu bila kuwashtua
wapangaji wote kwenye ghorofa hili.
Wakati wanaingia, Yule chokoraa alitambaa kiubavu. Alikuwa amedondokea
kwenye bastola yake na sasa ilikuwa mkononi. Alikuwa bado anataka apate malipo
yake ya kazi. Alifyatua risasi moja kwangu na nikahisi kitu kimepita usoni
shaaa kabla ya kutoboa ukuta, na kudondosha udongo.
Polisi mmoja alifyatua risasi. Nilipiga kelele, lakini nilikuwa
nimechelewa.
Kijana yule akafa, akiwa anajaribu kufyatua risasi nyingine kwangu.
Alikuwa na ujasiri wa ajabu.
Itaendelea
kesho…
Comments
Post a Comment