- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Akafungua mlango wa gari na kuingia. Akaingia haraka na kwa nguo
alizovaa, hata magoti hayakuonekana. Aliufunga mlango haraka kabla hata
sijaugusa.
“Usiku mwema, Bwana Ryan,” alisema, na akawasha gari, akaendesha
na kuondoka eneo hilo.
Niliitazama gari hadi ilipotokomea, halafu nikatazama saa yangu. Ilikuwa
saa mbili na dakika thelathini na tano. Ningependa anipe kampani kwa chakula
cha usiku. Usiku huo ukawa mrefu kwangu: mtupu na uliodumaa. Nilisimama kwenye
maegesho na kuanza kuwafikiria kati ya wasichana wanne au watano niliowafahamu
ambaye angeweza kuja kupata chakula cha usiku na mimi, lakini hakuna hata mmoja
aliyemfikia Bi. West: hakuna hata mmoja ambaye angenipa wakati mzuri usiku huu
kwahiyo nikaamua kwenda kununua sandwich nyingine na kurudi nyumbani kuangalia
televisheni.
Nilifikiria Jay Wayde angesemaje kama angejua nilikuwa na mpango
wa kuwa na Bi. West jioni ya leo. Kwa vyovyote vile angeshtuka na kutahayari. Angetegemea
nitakuwa mahali nikizungumza kwa ukali na mrembo huyu au tukivutana na mrembo
mwingine.
Nikaingia kwenye mgahawa. Muziki kutoka kwenye juke-box ulikuwa
ukipigwa. Wasichana wawili waliovalia jeans na visweta vya kubana waliketi
kwenye stuli katika baa, makalio yao yalionekana na mvuto, nywele zao zilisukwa
katika staili ya Bardot, vidole vyao vikiwa na kucha ndefu.
Wakanitazama wakati ninaingia, macho yao makavu ya ujana yakaanza
kunisawiri, halafu wakatazama pembeni. Waliona kama mzee, sina swagger wala
mvuto.
Nilikula nyama na sandwich, nikionekana mwenye mawazo. Hata
kwenda Hong Kong asubuhi hakukuonyesha
furaha yoyote. Nikachukua picha za Herman na Jo-An na kuziangalia kwa makini. Walinekana
wako tofauti mno. Mwanamume ndiye aliyenitisha. Sikuweza kuelewa ni kwa nini
msichana kama Jane West siyo tu kwamba alizama kwenye penzi bali alimzalia na
mtoto.
Nikaachana nao na kuziweka picha mfukoni. Baada ya kulipia sandwich,
nikaingia mitaani, nikitambua kwamba wasichana wale wawili walikuwa wanaendelea
kunitazama. Mmoja wao akacheka kimbeya. Pengine aliona ninachekesha. Kuna
nyakati ninaponyoa ndevu huwa najifikiria hivyo pia.
Nikaendesha hadi nyumbani kwangu, kwenye vyumba vya ghorofani,
ambapo kulikuwa na sebule kubwa, chumba kidogo cha kulala na jiko dogo tu. Nimeishi
hapo tangu nilipoingia jijini Pasadena. Ilikuwa ni katikati, gharama nafuu na
mahali tulivu. Hakukuwa na lifti, lakini sikujali kabisa. Kupandisha ngazi za
ghorofa tano kuliufanya mwili wangu uwe mkakamavu na ulimfanya adui yeyote akae
mbali pindi tunapokabiliana kwa sababu ya wepesi wangu na mapigo matakatifu.
Nilikuwa ninahema kidogo wakati nilipoufikia mlango wangu. Wakati
nikihangaika na ufunguo, nikajiambia kwamba inabidi nipunguze sigara, lakini
nilikuwa najidanganya.
Niliufungua mlango na kuingia sebuleni. Sikumuona mpaka nilipokuwa
nimeufunga mlango. Mwanga ulikuwa mdogo: kulikuwa na kiza kidogo na yeye alikuwa
amevaa nguo nyeusi.
Kulikuwa na bango la tangazo mtaani ambalo mwanga wake wa buluu,
kijani na mwekundu ulimulika dari yangu. Kama isingekuwa kwa bango hilo, wala
nisingemuona kabisa.
Alikuwa ameketi kwenye kiti changu nilichokipendelea ambacho alikisogeza
karibu na dirisha. Aliketi akiwa amekunja miguu yake, mikono yake ikiwa kwenye
gazeti lililokunjwa mapajani na alitulia kabisa.
Kwa hakika alinipa mshtuko ambao ulifanya moyo wangu upoteze
mapigo.
Swichi ya kuwashia taa ilikuwa jirani yangu. Nikaiwasha.
Alikuwa ni kijana mdogo tu: kama umri wa miaka kumi na nane au
kumi ta tisa hivi, lakini mwenye umbile lenye nguvu na kifua kipana. Alivalia
jaketi jeusi, kofia nyeusi na skafu chafu nyekundu, suruali aina ya corduroy nyeusi
na kitambaa cheusi alichojifunga shingoni mwake.
Ni aina ya vijana ambao utawaona wakati wowote usiku wakiwa nje ya
baa: uzao wa watoto wa mitaani: katili kama panya buku.
Ngozi yake ilikuwa chafu. Macho yake yalikuwa ya kikatili kama ya
mvuta bangi na muuaji. Sikio lake la kulia lilikuwa limekatika na alikuwa na
alama ya jeraha kubwa iliyotokana na kisu kwenye taya lake. Alikuwa ni miongoni
mwa viumbe hatari ambao nimewahi kukutana nao.
Kwa kweli alinitisha mno.
Akanitazama kwa dharau na tabasamu la kejeli.
“Hallo, Buster, nilidhani huwezi kurudi kabisa,” alisema katika
sauti ya jeuri inayokwaruza.
Itaendelea
kesho…
Comments
Post a Comment