- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Judith
Mhina-MAELEZO
Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere ulikuja hapa
duniani Aprili 13, 1922 kupitia kwa Mpendwa
Marehemu Bibi Mgaya wa Buritho kama
zawadi kwa nchi ya Tanzania.
Mwalimu
tunamshukuru Mungu kwa kutupa wewe ambaye umeitendea mambo makubwa Tanzania,
Afrika na Dunia kwa ujumla.
Mwalimu
wakati nakumbuka kuzaliwa kwako nimepata fursa ya kuangalia kazi ulizozifanya
mara baada ya kuacha madaraka ya Urais na kujikita katika kazi kuu tano; Mosi pamoja
na kubaki na kofia moja ya Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya kuimarisha
Chama na alianza maandalizi ya kukabidhi Uenyekiti huo kwa Rais aliyepokea
madaraka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa Rais Mstaafu wa
Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Pili, mwaka
1986 baadhi ya Viongozi wa nchi za Kusini mwa Dunia, walikuomba kuanzisha Tume
ya Uchambuzi wa maendeleo ya nchi za
Kusini tangu miaka 30 iliyopita na kuweza kuona hatua za maendeleo na
changamoto zilizopo katika mataifa hayo na mapendekezo ya nini kifanyike ili
kuboresha ustawi wa wananchi.
Mwalimu Nyerere
alikubali jukumu hilo, ndipo alianza kutembelea nchi 19 katika Bara la Asia na Marekani
ya Kusini kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa majukumu hayo mapya. Safari ya
kutafuta maoni hayo ilikuwa ni pamoja na kupata uthibitisho wa kuwaelewesha wananchi
na nchi hizo kuhusu majukumu ya Tume na aina ya maoni yanayokusanywa.
Kazi hiyo aliifanya
kwa miaka mitatu na kutoa ripoti kuwa nchi za Kusini zifanye maendeleo yao yenyewe
yalenge maslahi ya wananchi walio wengi kwa kielelezo kuwa ili nchi za Afrika
ziweze kupiga hatua za maendeleo ni vyema ziwe na mshikamano kama zinahitaji
kushindana na nchi za Kaskazini.
“Nchi za
Kusini zishirikiane kibiashara, kwa kuwa nchi za Kusini zina mazoea ya kufanya
biashara na nchi za Kaskazini lakini hakuna utaratibu mzuri wa nchi za Kusini
kufanya biashara wenyewe kwa wenyewe, au hata katika uwekezaji rasilimali”
alisema Mwalimu Nyerere.
Aidha,
Mwalimu Nyerere alisema Wataalam wengi wako Kusini lakini nchi za Kusini
zinatafuta wataalam kutoka Kaskazini, hivyo ni wajibu wa nchi za Kusini kujenga
na kuimarisha ushirikiano wa pamoja baina yao.
Tatu,
Mwalimu alianzisha kituo cha muda cha Nchi za Kusini pale Geneva ambapo Mwalimu
na Viongozi wengine walifanya kazi kwa muda wa miaka miwili, jukumu lao likawa kuelezea shughuli za maamuzi na mapendekezo ya
Tume.
Nne,
kuanzisha Ofisi ya kudumu ya Nchi za Kusini pale Geneva kwa ajili ya Mataifa
hayo kutoa hoja kupitia vuguvugu la nchi za kundi la 77 ambazo hazikuwa na
chombo cha kuwasaidia kupaza sauti zao.
Mwalimu
akapokea jukumu hilo na kuanzisha Ofisi ya kudumu ambayo ilikuwa chombo cha Serikali
badala ya chombo cha kiraia na kuhusisha nchi 49 ambazo ziliweka sahihi, pamoja
na nchi kubwa ulimwenguni ikiwemo India, Brazil na Afrika ya kusini.
Tano,
alikuja na wazo la kuanzisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere, hatua iliyotokana na
harakati za kazi yake ya kuunganisha nchi za kusini, ambapo alitaka taasisi
hiyo kufanya kazi zake katika ukanda wote wa nchi za Bara la Afrika.
Miongoni mwa
kazi hizo ni pamoja na kuangalia maendeleo ya watu, kupitia dhana ya umoja
na ushirikiano miongoni mwao.
Nakumbuka
hotuba ya Mwalimu Nyerere aliitoa mwezi Februari
mwaka 1960, akiwa Rais wa chama cha Tanganyika
African National Union (TANU) , alikaribishwa nchini Marekani katika
Kongamano la Afrika katika Chuo cha Wellesley Massachusetts kuongelea kuhusu
“Nafasi ya Afrika Duniani” .
Katika
hotuba hiyo, Mwalimu alizungumzia hatua mbalimbali za ukombozi wa Bara la
Afrika, mchango wa Waafrika katika Mataifa ya Ulaya na Marekani. Mwalimu
alilisemea Bara la Afrika Kama Bara la matumaini kwa ubaguzi wa rangi.
Mwalimu
alisisistiza kwa kusema “Muda utafika ambapo Marekani na Ulaya Magharibi
watajisikia vibaya jinsi walivyoitumia Afrika” huku akitolea mifano ya mateso
na manyanyaso waliyoyapata Waafrika ikiwemo vita vya Mau Mau nchini Kenya, vifo
vya watu wa kabila la Waherero nchini Namibia, vita vya Majimaji nchini
Tanzania.
Hotuba hiyo
ilikuwa ya kwanza kwa Mwalimu Nyerere kuchapishwa kimataifa, hakika imeonyesha kwa
dhati, Mwalimu hata kabla ya Uhuru alitambua nafasi ya umoja katika kupigania
uhuru wa Bara la Afrika.
Aidha, ndoto
hii ya umoja alisafiri nayo katika kujenga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nafasi
ya Uenyekiti Jumuiya wa Nchi zilizo mstari wa mbele katika Ukombozi Kusini mwa
Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) na nyingine nyingi.
Taasisi ya
Mwalimu Nyerere dhumuni lake kuu ni kuendeleza Amani, Umoja na Utulivu wa
Maendeleo ya pamoja Barani Afrika. Mwalimu alikuwa muanzilishi na Mweneyekiti
wa kwanza wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Septemba 14,
1996 alikaribishwa Kilimanjaro hoteli kuhutubia na kuzindua Taasisi ya Mwalimu Nyerere. Umuhimu wa Umoja,
umuhimu wa ukubwa wa soko, Amani baina ya nchi ndani na nje ya nchi na Maendeleo katika Afrika.
Alipata
fursa ya kukutana na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwaeleza
juu ya Taasisi hiyo na madhumuni yake. Katika kipindi hiki Mwalimu alikuwa msuluhishi
wa mgogora wa Burundi.
Mwalimu leo
ungetimiza miaka 95 tangu kuzaliwa,
kimwili hatupo pamoja nawe, lakini fikra zako, mitazamo yako, utendaji wako
bado ni dira na muelekeo wa Taifa letu Daima tutazifuata. Hakika siku ya leo ni
siku muhimu sana kwa nchi yetu. Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika.
MWISHO
Comments
Post a Comment