Featured Post

HAYA NDIYO MABADILIKO YA KWELI, CCM SASA ITAKUWA IMARA ZAIDI




Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
JUHUDI za ndani kwa ndani za kuzamisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimegonga mwamba. Lakini zinaendelea.
Mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kulikuwa na tetesi nyingi kwamba mradi mkubwa wa wanachama na viongozi kuhama chama hicho ulikuwa umeiva. Mradi huo uliwahusisha wanachama wote waliokuwa kwenye kambi za vigogo wa chama hicho waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi.
Jitihada za ‘kuwashinikiza waasi’ hao waondoke haraka ndani ya chama hata kupitia uamuzi wa ‘Kujivua Gamba’ hazikuweza kusaidia, ingawa tetesi ziliendelea kuwataja baadhi ya vigogo hao ‘wakifunga mikataba’ na baadhi ya vyama ama viongozi wa vyama vya upinzani na kwamba tayari walikuwa wamewatanguliza ‘watu wao’ kwenye vyama hivyo.

Zoezi la kujivua gamba liliposhindika, ikabidi baadhi ya vigogo ndani ya chama, wale ‘watuhumiwa’ waliotajwa ndani ya chama na hata nje, waamua kujizatiti kwamba hawataondoka kamwe.
Mkakati wao mkubwa ulikuwa wa mwaka 2012 wakati wa Uchaguzi wa Chama ambapo vigogo hao walihakikisha wanaimarisha mtandao wao kwa kusimika watu wao kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi taifa.
Rushwa ya mabilioni ya fedha ilitumika na ilikuwa nje nje kiasi kwamba Dodoma ilibadilika ghafla hata wakati wa uchaguzi wa ngazi ya taifa, ambapo watu walikuwa wakiwatumia mafundi viatu, wauza magenge na mama lishe kupitisha rushwa hiyo kwa watu wao kuhakikisha mkakati wao unafanikiwa.
Mbinu hiyo ilifanikiwa, lakini ilionekana kama Chama hakikuwa na uthubutu wa kuwaadhibu wahusika, hali ambayo iliendelea kukidhoofisha kwa kuwa rushwa na ufisadi ni kinyume na misingi ya CCM na ilishangaza ni kwa vipi viongozi walishindwa kuwawajibisha.
Yalisemwa mengi ndani na nje ya CCM, baadhi wakayabeza na kuyadharau, lakini yalidhihirika mwaka 2015 wakati kundi kubwa la wanaCCM, wakiwemo viongozi wa Chama wa Mikoa, walipoamua kumfuata Edward Lowassa kujiunga na upinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ndilo kundi hilo hilo ambalo lilitaka kuleta fujo wakati wa uteuzi wa mgombe urais kupitia CCM Julai 11, 2015 pale Dodoma kiasi cha kuanzisha mapambio ndani ya ukumbi huku uongozi wa juu ukiwaangalia tu.
Tena ni kundi hilo hilo ambalo ilielezwa lilikuwa limewakusanya vijana takriban 400, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, kwenda Dodoma ili kuanzisha maandamano endapo Lowassa angeshindwa kupitishwa kuwa mgombea urais.
Baada ya vyombo vya ulinzi na usalama kuwadhibiti vijana hao, bado hawakuacha kuwashawishi wanafunzi kadhaa wa vyuo vya mjini Dodoma kutaka kuanzisha fujo nje ya ukumbi, jambo ambalo pia lilidhibitiwa ipasavyo.
Lakini makandokando yale yaliendelea kubakia ndani ya CCM licha ya kundi kubwa kuondoka, ambapo waasi hao ndio waliokuwa wakivujisha siri za chama na mikakati yote ya kampeni kupeleka upinzani.
Leo hiiCCM imewafagia. Wameondoka. Ingawa uchunguzi unaonyesha kwamba, bado tu wapo baadhi yao ambao wamesalia.
Hata hivyo, imebainika kuwa juhudi za kudoofisha CCM zimekuwa hafifu kwa maana kwamba hoja hazijawa thabiti na wengi wanaotumika na, au kutumiwa wana sifa za uanasiasa wa magazetini, redioni na kwenye televisheni tu; siyo wana-mikakati.
Chuki,fitina na visasi pamoja na ubabe ndiyo mabango makuu ya wanaliotimuliwa CCM ambao tayari baadhi yao wamekwishapatiwa hifadhi katika vyama vya upinzani.
Kila wakati Chadema inapoopoa mwanachama wa CCM, viongozi wake wanataka “anyee kambi” hadharani; atoe lawama, shutuma na tuhuma kwa viongozi na chama chake cha zamani huku akiwa amevalishwa magwanda na kuonyesha ishara ya VEMA!

Misingi iliyobomoka
KilichofanyikaDodoma katika kusafisha Chama ndicho hasa kinachotakiwa, kwa maana CCM ilikwishapotezza sifa kitambo na ilihitaji kujitafakari.
Kauli ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli, kwamba hivi sasa ni mwisho kuomba omba misaada kwa wafanyabiashara – ambao wengi wao ndia yao si njema bali kuficha madudu yao – ni ya msingi kabisa katika kurejesha misingi iliyopotea.
CCM ilikuwa ‘pango la wafanyabiashara, wapiga dili na mafisadi’. Tena tunaambiwa hata wafanyabiashara haramu na wahalifu wengine walijiingiza huko kwa kutumia fedha walizozichuma kiharamu ‘kununulia’ uongozi.
Ahadi zake zote alizozitoa wakati wa kampeni ndizo anazoendelea kuzitekeleza kwa sasa ndani ya serikali, lakini atafanikiwa kuchimbua mzizi ambao umekifanya chama hicho kikongwe kabisa barani Afrika na kinachoheshimika kutokana na kusaidia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, kionekane kimeyumba kwa kiasi kikubwa kwa kusimamia misingi imara huku akiwawajibisha wasaliti na waasi.
Watanzania wanaopenda haki na demokrasia wameshuhudia jinsi alivyotumia staili yake ya kutumbua majipu ndani ya chama hicho na kukisafisha na ombwe la uongozi ambao uligeuzwa kama ‘zabuni’, mwenye fedha nyingi ndiye anayechaguliwa.
Kila mmoja anaamini kwamba Magufuli anaweza kurejesha misingi imara ya TANU na baadaye CCM, ambayo imeachwa kwenye makaratasi.
“Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa!” Hii ni mojawapo ya Ahadi 10 za Mwana-TANU ambazo zilirithiwa na CCM inayosisitiza kwamba mtu yeyote anayepewa uongozi hapaswi kuutumia kwa maslahi yake binafsi bali kwa maslahi ya wote.
Ahadi hii na nyinginezo zilikuwa zikiimbwa kila mahali kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu ambako somo la Siasa lilianzishwa na serikali ya TANU na kuendelezwa na CCM kabla ya kufutwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
TANU (na baadaye CCM) kupitia Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliamini binadamu wote ni sawa na kusisitiza raia wote kwa pamoja wamiliki utajiri wa asili wa nchi hii ukiwa kama dhamana kwa vizazi vyao; na Kwamba ni wajibu wa Serikali, ambayo ni watu wenyewe, kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi ya Taifa ili kuhakikisha usitawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na siasa ya watu wote kuwa sawa.
Katiba ya chama hicho inaeleza bayana kwamba, Serikali lazima itumie mali yote ya nchi kwa kuondoshea umaskini; ujinga na maradhi; Kuona kwamba Serikali inaondoa kila namna ya dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa na upotofu; na Kuona kwamba Serikali ya nchi inasimamia barabara njia kuu za kuzalisha mali na inafuata siasa ambayo itarahisisha njia ya kumiliki kwa jumla mali za nchi.
Njia kuu za uchumi ambazo zinapaswa kuwa chini ya wakulima na wafanyakazi ni pamoja na ardhi, misitu, madini, maji, mafuta na nguvu za umeme; njia za habari, njia za usafirishaji; benki, na bima; biashara na nchi za kigeni na biashara za jumla; viwanda vya chuma, mashine, silaha, magari, saruji, mbolea; nguo, na kiwanda chochote kikubwa ambacho kinategemewa na sehemu kubwa ya watu katika kupata riziki zao au kinachotegemewa na viwanda vingine; mashamba makubwa na hasa yale yanayotoa mazao ya lazima katika viwanda vikubwa.
Suala la mgawanyo wa mali za umma limekuwa kitendawili kigumu kuteguliwa hasa baada ya kushuhudia namna viongozi wa chama na serikali wanavyozitafuna mali za umma, wakijali zaidi matumbo yao kuliko ya Watanzania licha ya kuwepo kwa maadili ya uongozi ambayo nayo yameendelea kubaki kwenye makaratasi na kufungiwa kabatini huku agizo la kutenganisha biashara na siasa likiwa ni shairi lisilo na vina!
Viongozi hawa ambao wanaagizwa na chama kwamba ‘Cheo ni dhamana’, pamoja na kubadili mfumo wa siasa kutoka Ujamaa kuja kwenye Ubepari Mamboleo, bado wanashindwa kufuata maadili sahihi ya uongozi, yakiwemo kutojilimbikizia mali kwa kutumia vyeo vyao, kutaja mali zao kabla ya kuingia madarakani na baada ya kutoka, badala yake wanaendelea kuchota mali za umma kadiri wapendavyo huku wananchi wakiendelea kuogelea kwenye umaskini.
Kila kiongozi anayeingia madarakani huangalia kwanza tumbo lake, na kadiri siku zinavyosonga hupata tamaa ya kuchota zaidi na zaidi na mwishowe huona kwamba ni haki yake kuwa tajiri huku wengine wakiendelea kupiga miayo bila kuwa na uhakika hata wa kipande cha muhogo kushibisha tumbo kwa mlo mmoja.
Tunashukuru kuona kwamba Rais Magufuli ameliona hilo na ameanza kuwashughulikia kwa kasi. CCM sasa itakuwa imara zaidi, ni ‘Nginja nginja hadi 2020!’.
Wenyewe ‘wanaisoma namba’!

Comments