- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA HAMZA TEMBA - WMU
...................................................................
Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu leo imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela Peter Kabi na Leonida
Loi Kabi ambao ni wanandoa baada ya kukutwa na meno ya tembo 210 yenye uzito wa
kilo 450.6 pamoja na mifupa mitano ya tembo.
Meno hayo yanayodaiwa
kuwa ni sawa na idadi ya tembo 93 waliouwawa yalikutwa nyumbani kwa washtakiwa
hao tarehe 27 Oktoba, 2012 eneo la Kimara Stop Over Jijini Dar es Salaam.
Hakimu Mkazi Mkuu wa
Mahakama hiyo, Huruma Shahidi amesema ametoa hukumu hiyo leo baada ya mahakama
kujiridhisha na ushahidi wa upande wa Jamhuri ukiongozwa na mawakili Paul
Kadushi na Elia Athanas ambao kwa pamoja umewatia hatiani washtakiwa hao.
Amesema katika kosa
la kwanza kila mtuhumiwa atatumikia kifungo cha miaka 15 jela, kosa la pili na
la tatu miaka 20 kila moja na kwamba hukumu hizo zitaenda kwa pamoja.
Akitoa ushahidi wa upande
wa Jamhuri juu ya athari za ujangili nchini, Mtaalamu kutoka Taasisi ya Utafiti
wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), aliyefahamika kwa jina moja la Lymo amesema
idadi ya tembo hapa nchini imepungua kwa kiasi kikubwa kwani sensa ya mwaka 2006
inaonyesha tembo walikuwa 1,034,000 tofauti na sesa ya mwaka 2012 ambayo
ilionesha idadi hiyo kupungua na kufikia 43,000.
Alisema sensa ya
mwaka 2013 ilionesha idadi ya tembo kuongezeka na kufikia 50,000 ambayo ni
matunda ya jitihada za Serikali katika kukabiliana na ujangili kwa kuongeza nguvu
katika doria na mikakati mbalimbali ya kudhibiti ujangili.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof.
Alexandre Songorwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya
hukumu hiyo amesema, kila mtanzania anapaswa kujifunza kupitia hukumu hiyo kwa
kuwa binadamu wote hujifunza kutokana na makosa na kwamba ni jukumu la kila mtanzania
kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa.
“Rasilimali hizi ni
zetu sote watanzania, sio za Serikali, sio za Wizara ya Maliasili na Utalii,
sisi ni vibarua wenu, tuwalindie watoto wetu na wajukuu zetu hizi rasilimali, wasijekututukana
huko mwishoni kama hawatakuta chochote wakalazimika kupanda ndege kwenda
kuangalia vitu vilivyokuwa hapa hapa, watatutukana hatuna sababu ya kusubiri
matusi” alisema Songorwa.
Watuhumiwa wa Ujangili, Peter Kabi (wa pili kulia) na mke wake Leonida Loi Kabi (wa tatu kulia) wakielekea kusomewa mashtaka ya kukutwa na meno 210 na mifupa mitano ya tembo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam leo, wote wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Mtuhumiwa wa Ujangili, Peter Kabi (wa pili kulia) akielekea kusomewa mashtaka ya kukutwa na meno 210 na mifupa mitano ya tembo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam leo, mtuhumiwa huyo na mke wake Leonida Loi Kabi (hayuko pichani) wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexandre Songorwa (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya hukumu hiyo leo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara hiyo anaeshuulikia Maendeleo ya Wanyamapori, Kanisius Karamaga.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexandre Songorwa akizungumza na wanahabari katika moja ya ukumbi mahakamani hapo.
Comments
Post a Comment