- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
MJUMBE wa
Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, sasa ‘anaweweseka’ kwa kukosa hoja zenye
mashiko za kuikosoa Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika
kipindi ambacho Serikali inafanya kila jitihada za kulifufua na kuliimarisha
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege, yeye anabeza na kuona
kwamba hicho siyo kipaumbele, bali fedha hizo zingetumika kupeleka maji safi na
salama vijijini.
Alitoa
kauli hiyo wakati akizungumza na vijana wa Chadema ambao ni wanafunzi wa vyuo
vikuu (Chadema Students Organisation – Chaso) mjini Tabora na kuhoji kwa nini
serikali imeshindwa kupeleka huduma muhimu vijijini.
"Tumesikia
nia njema yao ya kuagiza ndege nyingine zaidi miaka miwili ijayo, lakini
tunajiuliza, je isingekuwa busara kutumia fedha hizo kupeleka maji safi na
salama mijini na vijijini?" alikaririwa akihoji.
Binafsi
nimeshtushwa na kauli hiyo ya Lowassa
kupinga ununuzi wa ndege katika shirika ambalo kwa miaka mingi limegubikwa na
kashfa mbalimbali za matumizi mabaya ya fedha huku likiwa halina ndege hata
moja.
Mzalendo
yeyote angepaswa kupongeza jitihada hizi za serikali, kwani hivi sasa siyo
kwamba tutaachana na tabia ya kukodi ndege, lakini pia kwa kumiliki ndege zetu
wenyewe tuna uhakika wa kufungua safari za nje kama ilivyokuwa zamani kabla ya
‘wapiga dili’ ndani ya serikali hawajalihujumu shirika na kuingiza ndege zao
wenyewe.
Lakini
nikashangazwa zaidi na kauli kwamba ni vyema serikali ipeleke maji vijijini,
ambayo inatolewa na Lowassa mwenyewe kwa namna ambayo inaonyesha wazi ni
kutafuta ‘kick’ ya kisiasa.
Nimeshangaa,
na ninaamini Watanzania wengine wamemshangaa, kwa sababu jukumu la kupeleka
huduma ya maji vijijini Lowassa mwenyewe alishindwa kulitekeleza kwa miaka
mitano mfululizo, kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, wakati Rais wa Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa, alipompa dhamana ya kuongoza Wizara ya Maji na Maendeleo ya
Mifugo.
Kama
waziri mwenye dhamana ya maji, alipaswa kuhakikisha wananchi, hasa wa vijijini,
wanapata maji safi na salama, lakini hilo halikufanyika na ni wakati yeye akiwa
Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo ndipo tulishuhudia wimbi la wafugaji,
wengi wa jamii wa Wamasai na Wasukuma, wakihama kutoka kwenye makazi yao na
kuvamia maeneo ya Mashariki, Kusini na Kusini-Magharibi mwa Tanzania, hasa
mikoa ya Morogoro, Mbeya, Rukwa, Lindi, Pwani na Mtwara ambako hata ng’ombe
wenyewe walikuwa hawawajui zaidi ya wengi wao kuwaona kwenye picha!
Matokeo ya
kuhama huko kwa wafugaji tangu kipindi hicho ndiyo mapigano ya wakulima na
wafugaji ambayo tunayashuhudia sasa na yamepoteza maisha ya Watanzania wengi
kama kule Kiteto na Kilosa.
Lowassa
anafahamu fika kwamba bajeti zetu ni ndogo, hazitoshi, na hata mradi ambao leo
anaweza kujivunia kuufanikisha wa Maji ya Ziwa Victoria, zilikuwa fedha kutoka
Benki ya Dunia kupitia shirika lake la WaterAid.
Anafahamu
kwamba, mradi ule tusingeweza kuugharamia kwa bajeti yetu, ndiyo maana
ulichelewa kutanuliwa kutoka Shinyanga kwenda mikoa mingine.
Vinginevyo
aseme leo hii ni kwa nini kwa mamlaka yake alishindwa kuyafikisha maji hata
Tabora, ambako siyo mbali na Shinyanga.
Leo hii
serikali inayo mipango mizuri ya kuhakikisha maji hayo yanafika mpaka Singida,
lakini anabeza.
Niliwahi
kusema wakati fulani kwamba, ‘Ukweli wa mwanasiasa ni jina lake tu’, na sasa
wengi wanaamini, kwa sababu mambo mengi wanayoyasema wanasiasa, hasa walio nje
ya madaraka, yanalenga kukosoa serikali iliyoko madarakani na siyo kujenga,
hata kama mambo hayo hayana ukweli wowote.
Ni Lowassa
huyu ambaye aliwahi kusema kwamba ndiye aliyejenga Shule za Kata, lakini
nakumbuka kauli hiyo ilipingwa hadharani na Joseph Mungai,
ambaye alisema: “Lowassa ana mawazo mgando na akili ya kusahau, shule za Kata
zilijengwa na wananchi chini ya Mkapa.”
Pengine
kwa kuwa alisomea sanaa ndiyo maana sasa ameamua kuishambulia serikali kwa
suala la maji, lakini naamini kwa kauli yake hiyo hata wananchi wa Monduli,
wakiwemo wa kijijini Ngarash alikozaliwa siku ile ya Jumatano, Agosti 26, 1953 akiwa
ni mtoto wa 4 kati ya watoto 23 wa mzee Ngoyai Lowassa, wanaweza kumsuta.
Lowassa
amekuwepo Bungeni kwa miaka 30 – kwanza akiwa Mbunge kupitia Jumuiya ya Vijana
kuanzia 1985 – 1990, na kisha Mbunge wa Monduli kwa miaka 25 kuanzia mwaka 1990
– 2015.
Lakini leo
hii, siyo Monduli tu, lakini hata kijijini Ngarash kuna shida kubwa ya maji, na
aeleze leo ni kwa nini kwa miaka yote aliyokaa Bungeni, akishika nyadhifa
mbalimbali za uwaziri, hakuweza kusaidia walau kupatikana maji ya uhakika.
Lowassa
amekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais
(anayeshughulikia Sera, Uratibu wa Bunge na Maafa) kati ya 1990-1993 chini ya
Mzee John Malecela aliyekuwa Waziri Mkuu; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
Mijini kati ya 1993 – 1995; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira
na Muungano) kati ya 1995 – 2000); na Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo
kati ya 2000 – 2005.
Lowassa
amekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka miwili, mwezi
mmoja na siku 17 kati ya Desemba 20, 2005 hadi Februari 8, 2008 alipolazimishwa
kujiuzulu kwa kashfa ya kampuni ya ufuaji umeme wa dharura ya Richmond
Development LLC.
Hivi
katika kipindi chote hicho alishindwa hata kuleta maendeleo ya jamii ikiwemo
huduma ya maji huko Monduli, achilia mbali Tanzania kwa ujumla.
Hizi ni
propaganda za kisiasa ambazo zinapaswa kupuuzwa kwa sababu zinalenga kukwamisha
mipango madhubuti ya maendeleo ya serikali.
Pengine
kwa faida ya walio wengi, tafsiri ya haraka ya neno ‘Propaganda’ ni taarifa, mawazo au uvumi
unaosambazwa kwa makusudi kumsaidia au kumharibia mtu, kundi la watu, harakati,
taasisi, taifa na kadhalika.
Propaganda pia inatafsiriwa kama namna ya mawasiliano yanayolenga
kuwashawishi baadhi ya watu waunge mkono jambo fulani.
Lakini tafsiri nyingine ya Propaganda ni taarifa
ambazo siyo sahihi zinazotumika kwa msingi wa kushawishi hadhira na kuchochea
agenda, mara nyingi kwa kuwasilisha taarifa zilizopangwa ama kutengenezwa
(pengine kudanganya hapa na pale) ili kuhamasisha kundi linalolengwa liamini
kinachoelezwa na liunge mkono.
Neno hili kwa sasa limebebeshwa mtazamo hasi kwa
kulihusisha na harakati za kurubuni kwa maslahi ya kundi linaloendesha harakati
hizo na kwamba wanaofanya propaganda wanaweza kuwaaminisha watu kwamba ile
rangi ‘nyeusi’ ni ‘nyeupe’ na kinyume chake.
Pengine hakuna mtu katika historia aliyetumia nguvu
ya propaganda kwa mafanikio ya kutisha kama alivyofanya Paul Joseph Goebbels,
ambaye alikuwa Waziri wa Propaganda wa chama cha Nazi cha Ujerumani kati ya
mwaka 1933 hadi 1945 wakati wa Hitler.
Wakati wote wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, yeye ndiye
aliyedhibiti mawasiliano yote nchini Ujerumani na kufanikiwa kulibadilisha
taifa lote kuwa kakamavu na la kijeshi.
Inaelezwa kwamba, isingekuwa mbinu za Goebbels,
chama cha Nazi kisingeweza kutawala Ujerumani kwani licha ya kuhamasisha magwaride
ya kijeshi, ndiye aliyewafanya Wajerumani wawe makatili hata wakati wa vita
kiasi cha kufanya mauaji ya kutisha, ikiwa ni pamoja na kuwateketeza Wayahudi.
Goebbels ndiye aliyehamasisha hadi kuanzishwa kwa
somo la propaganda shuleni, ambapo watoto walianza kuaminishwa mambo mbalimbali
tangu wakiwa wadogo, hata kama yalikuwa ya uongo.
Kiongozi wa chama cha National Socialism (au kwa
Kijerumani: Nationalsozialismus), ambacho ni maarufu zaidi kama Nazi, Adolf
Hitler, anasema katika kitabu cha Mein
Kampf Sura ya VI (nanukuu kwa tafsiri ya Kiswahili): "Daima propaganda lazima ijidhihirishe kwa watu wengi. (...)
Propaganda zote lazima ziwasilishwe katika mfumo maalumu na lazima zijikite
kwanza kwa wasomi ili zisiwe juu ya vichwa vya watu wenye uelewa mdogo ambao
ndio walengwa. (...) Sanaa ya propaganda hasa inahusisha uwezo wa kuamsha
matamanio ya watu kwa ushawishi wa kutumia hisia zao, ili kutafuta mfumo mzuri
wa kisaikolojia ambao unaweza kuteka umakini na kuchochea msukumo mioyoni mwa
wananchi wengi. Makundi makubwa ya wananchi hayaundwi na wanadiplomasia au
maprofesa wala hayahusishi watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi baada ya
tafakuri katika kadhia husika, bali ni makundi ya vijana ambao wanayumbishwa na
wazo moja baada ya jingine. (...) Kundi kubwa la wananchi katika taifa lina
tabia za kike na mtazamo ambao mawazo na mwitikio wao unatawaliwa na huruma
badala ya tafakuri makini. Halitofautiani sana, lakini lina mtazamo hasi na
chanya wa kupenda na kuchukia, sahihi na isiyo sahihi, ukweli na uongo.
"Propaganda haihitaji kufanya uchunguzi wa ukweli wa jambo
(objectively) na, kwa namna inavyotamaniwa na upande mwingine, inatakiwa
kuwasilishwa kwa mujibu wa nadharia ya utawala wa haki; lakini lazima
iwasilishwe kwa misingi ya ukweli ambao upande husika unataka. (...) Uwezo wa
wananchi wengi umedumaa, na uelewa wao ni mdogo. Kwa upande mwingine, ni wepesi
sana wa kusahau. Kwa msingi huo, propaganda zote zinatakiwa kujikita katika
mambo machache muhimu na hayo yanapaswa kuhubiriwa katika fomula nyepesi
inayofanana. Kauli mbiu hizo zinatakiwa kurudiwa kila wakati ili kumfanya mpaka
mtu wa mwisho aweze kuelewa na kushawishika na yanayosemwa. (...) Kila badiliko
linalofanywa kuhusu hoja fulani ya propaganda lazima kila wakati iwe na
suluhisho moja. Kauli mbiu kubwa lazima iwekwe katika njia tofauti na kwa namna
mbalimbali, lakini mwisho wa siku lazima kurejea kwenye fomula ile ile."
Mbinu hii
ya propaganda ndiyo iliyotumiwa na Lowassa kwa wanavyuo wale Tabora, ambapo
hakuna aliyekumbuka kwamba kiongozi huyo huyo ndiye aliyekuwa na wajibu wa
kuwaletea maji miaka 15 iliyopita wakati akiwa waziri wa maji lakini
akashindwa.
Watanzania
wanapaswa kuwa makini na propaganda hizi, kwa sababu ndizo kwa miaka mingi
zimekwamisha maendeleo.
Lowassa
ana haki ya kujinadi na kugombea kwa sababu ni haki yake ya Kikatiba, lakini
hana budi kuunga mkono juhudi njema za serikali zenye kuleta maendeleo.
+255 656
331974
Comments
Post a Comment