- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Majike ya Alpine yenye pembe
Dume la Alpine
Jike la Alpine lisilo na pembe.
Na Daniel Mbega
Mbuzi jamii ya Alpine, mara nyingi wakifahamika kama
French Alpine, wana shingo ndefu na ngozi nzito ambayo huwa na rangi
mbalimbali, na kila moja ina jina lake. Kwa kawaida, rangi ya mbele ni tofauti na rangi ya nyuma japokuwa baadhi wana rangi ya aina moja.
Mbuzi jike mkubwa huwa na uzito wa
kilogramu 61.2 na beberu huwa na uzito wa kilogramu 77. Mbuzi jamii ya Alpine ndio
hutoa maziwa mengi zaidi kuliko jamii nyingine za mbuzi wa maziwa, ambapo mbuzi
moja hutoa takriban lita 907.18 za maziwa kwa mwaka yenye kiwango cha siagi cha
asilimia 3.5.
Mbuzi hawa wa Alpine wana maumbile
yenye ukubwa wa kati na makubwa zaidi, ni warefu wa kimo, na ndiyo jamii pekee
ya mbuzi wenye masikio yaliyoinuka ambayo huwa na rangi tofauti na
kuwatofautisha na wengine.
Mbuzi jamii ya Alpine ni
wastahimilivu, wanaoweza kuishi katika mazingira yoyote na kuwa katika afya
bora pamoja na kutoa maziwa ya kutosha. Manyoya yao ni mafupi. Nyuso zao ndefu,
rangi kama za jamii ya Toggenburg inapatikana pia.
Walikotokea mbuzi wa Alpine
Inaaminika kwamba, mbuzi ndio wanyama
wa kwanza kufugwa na binadamu. Mifupa ya mbuzi iliwahi kupatikana kwenye
mapango pamoja na dalili za uwepo wa binadamu kuishi kwenye mapango hayo.
Mojawapo kati ya mifupa ya mbuzi ilikuwa na uthibitisho kwamba mguu mmoja
ulikuwa umepona baada ya kuvunjika na kupona kwake kunaweza kuwa ni kwa msaada
wa binadamu. Wanasayansi wanasema mbuzi huyo angeweza kufa porini bila msaada
wa binadamu. Mabaki hayo ya mbuzi yamechunguzwa kwa kutumia carbon na
inaonekana mbuzi huyo aliishi kati ya miaka 12,000 – 15,000 iliyopita. Mbuzi
hao walikuwa wa Kiajemi (Mashariki ya Kati) maarufu kama “Pashang.” Baadhi ya
mbuzi wa Pashang walihamia kwenye Milima ya Alps. Inawezekana kabisa baadhi ya
mbuzi hao walihamia Milima ya Alps wakiwa na binadamu waliokuwa wakiwafuga na
wanyama wengine wa mwitu wakawepo pia milimani.
Mbuzi wa Alpine wa sasa asili yao ni
mbuzi wa Pashang, pia wanajulikana kama Bezoar. Kwa hiyo mbuzi hawa wa Alpine
wanapatikana kwa wingi katika maeneo ya Milima ya Alps barani Ulaya.
Kwa maelfu ya miaka, jamii ya mbuzi
wa Alpine imeendelezwa katika hali ya ustahimilivu kwenye miteremko mikali ya
milima ambako wamekuwa wastahimilivu na wanaweza pia kuishi hata kwenye jangwa
bila shida. Ni katika kipindi hicho ambapo wafugaji barani Ulaya walianza
kuwafuga kwa ajili ya maziwa.
Uwezo wa mbuzi hao wa Alpine kuzowea
mazingira haraka, ustahimilivu, na rangi zao murua ambazo zinavutia umewafanya
waenee sehemu nyingi duniani ambako walisambazwa katika safari za awali za
mahajazi na meli. Safari za awali za majahazi na meli zilikuwa zinaonekana
nzuri zaidi kama watu walichukua pia na mbuzi kwa ajili ya maziwa na nyama. Manahodha
wa zamani waliacha jozi moja ya mbuzi katika visiwa ambako safari zao zilipitia
na waliporejea walikuta mbuzi hao wamezaliana hivyo waliweza kuwakamua maziwa
ama kuwachinja kwa kitoweo. Hivi leo mbuzi wa jamii ya Alpine wanapatikana
katika mazingira yote duniani.
Usishangae leo ukisikia kuna aina nne
au tano za Alpine: French Alpine, Rock Alpine, Swiss Alpine (ambao sasa
wanaitwa Oberhasli), German Alpine na hata American Alpine.
Mbuzi hawa wanapatikana hata katika Afrika Mashariki, hivyo
unaweza kumuuliza ofisa mifugo akakuelekeza namna ya kuwapata. Ni wazuri kama
umeamua kufanya ufugaji wa kibiashara wa mbuzi wa maziwa kwa sababu wanatoa
maziwa mengi kuliko jamii nyingine za mbuzi.
Ikiwa una maoni au ushauri, usisite
kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au
nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.
Comments
Post a Comment