- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Makamu
wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa
kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert Bwele huku akicheza ngoma ya Ndolela
ya kundi la Utandawazi Theatre la mjini Nansio, Ukerewe. Mama Maria Teresa
alikuwa ziarani kisiwani humo kuangalia kilimo cha viazi lishe pamoja na
usindikaji wa bidhaa mbalimbali za zao hilo kilachotekelezwa kupitia mradi wa
Green Voices unaofadhiliwa na taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika, ambao yeye
ndiye rais wake.
WAKATI wasanii wa
kundi la ngoma za utamaduni la Utandawazi wanajipanga kutumbuiza, watu wengi
waliokusanyika kwenye viwanja wa shule ya msingi Bukongo mjini Nansio walikuwa
wanajiuliza mtoto Gozbert Bwele (8) aliyekuwa amekumbatia ngoma alikwenda
kufanya nini pale.
Lakini mara tu ngoma
zilipoanza kupigwa, uwanja mzima ukalipuka kwa furaha na haikushangaza wakati
makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega,
aliposhindwa kuvumilia na kutoka kwenda kucheza na mtoto huyo aliyeonyesha
ufundi mkubwa katika upigaji wa ngoma.
Mama Maria Teresa,
ambaye ni rais wa taasisi ya Mfuko wa kusaidia Wanawake Afrika, alijitoma
uwanjani kucheza na kumtunza mtoto huyo anayesoma darasa la kwanza kwenye shule
ya msingi Nansole katika halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.
Makamu huyo wa rais
mstaafu wa Hispania alizuru kisiwani Ukerewe akiwa ameongozana na ujumbe wake
kwa lengo la kujionea kilimo cha viazi lishe na usindikaji wa mazao mbalimbali
yatokanayo na viazi hivyo.
Kilimo hicho
kinafanywa na akinamama 25 chini ya Mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na
taasisi ya Mfuko wa kusaidia Wanawake Afrika, ambao kwa hapa nchini umewawezesha wanawake wa Tanzania kubuni
miradi endelevu inayoendana na utunzaji wa mazingira pamoja na kupambana na
mabadiliko ya tabianchi.
Mtoto Gozbert
Bwele akiwajibika na ngoma yake.
Gozbert Bwele siyo tu
alionekana kukibeba kikundi hicho na kuwafanya wananchi waliokusanyika kumtupia
macho yeye na kusahau kama kulikuwa na wasanii wengine, bali alionyesha uhodari
mkubwa wa kupiga ngoma kwa mbwembwe nyingi huku akitumia kichwa, miguu na
makalio, akilala na ngoma bila kupoteza midundo ya ngoma na wimbo.
Noti nyekundu zilikuwa
zikipepea usoni kama maua, lakini hakujisumbua kupokea wala kuokota hata moja,
bali ndiyo kwanza akaongeza ufundi katika kukung’uta ngoma huku akiimba.
“Ninapenda sana kupiga
ngoma,” ndivyo anavyosema Gozbert ambaye anabainisha kwamba katika familia yake
hakuna msanii isipokuwa yeye pekee.
Anaongeza: “Tangu
utotoni nilipenda kupiga ngoma, nilikuwa natumia vikopo, lakini nikaona
havinitoshi.”
Kebela Mganga ni
kiongozi wa kikundi cha Utandawazi Theatre Matwi ga charo (Masikio ya Dunia),
ambaye anaeleza historia ya mtoto Gozbert, ambapo anasema mtoto huyo aliibuka
tu kwenye mazoezi ya kikundi chao.
“Miaka sita iliyopita,
yaani mwaka 2010, tulishangaa kuona mtoto mwenye miaka kama miwili hivi akiingia
kwenye mazoezi yetu na kusema anataka kujifunza kupiga ngoma, yeye alitaka
ngoma tu,” anasema Kebela.
Anaongeza: “Wakati huo
tulikuwa tunajiandaa kwenda Bagamoyo, hivyo tukamwambia kwamba asubiri kwanza
turudi. Kwa hiyo mwaka uliofuata akiwa na miaka mitatu tu
akajiunga nasi na tukaenda naye Bagamoyo pale Chuo cha Sanaa.”
Mpaka sasa ameshashiriki matamasha mbalimbali ndani
na nje ya nchi ambapo Desemba 9, 2012 alishiriki sherehe za uhuru jijini Dar es
Salaam.
Wasanii
wa kundi la Utandawazi Theatre ‘Matwi ga charo’ la Nansio, Ukerewe,
wakitumbuiza wakati wa ziara ya makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Maria
Teresa Fernandez de la Vega (hayupo pichani) katika viwanja vya shule ya msingi
Bukongo mjini Nansio.
“Mwaka 2013 tulikwenda naye kwenye sherehe za uhuru
wa Rwanda na kule aliacha gumzo kubwa, mwaka 2014 tulikwenda naye kwenye
Sherehe za Mapinduzi Zanzibar na mwaka 2015 tulikwenda naye kwenye Maonyesho ya
Kilimo Zambia, ni msanii mahiri sana na tegemeo kwetu,” anasema Kebela.
Kebela anasema kwamba, katika kundi lao yupo pia
binti wa miaka 8 pia ambaye ni mahiri katika uchezaji wa ngoma.
Anaeleza kwamba, wanawalea watoto hao kama wa kwao,
lakini shule ndiyo kitu cha kwanza kuwahimiza ili waweze kuwa na msingi mzuri.
“Wote wanajitahidi sana shule, na tunawahimiza
wazingatie masomo,” anasema na kuongeza kwamba wanapata ushirikiano mkubwa
kutoka kwa wazazi wa watoto hao.
Mama Maria Teresa anapenda sana watoto. Hapa aliamua
kusitisha ziara kwa muda baada ya kumkuta mtoto huyu akiwa na mama yake (majina
yao hayakupatikana mara moja) wakiwa nje ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe.
Comments
Post a Comment