- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Baadhi
ya bidhaa zinazozalishwa kutokana na unga wa muhogo. Hii ni kazi nzuri ya
kikundi cha akinamama wa Kitanga Green Voices katika Kijiji cha Kitanga
wilayani Kisarawe.
Mchanganyiko
wa mihogo, maharagwe, mboga za majani na nyama. Ni chakula kizuri sana hiki
chenye aina nyingi za vitamin, wanga na protini.
PENGINE unafahamu faida tatu au nne tu za muhogo ambazo ni
kuutafuna mbichi, kuuchemsha au kuuchoma; unga wake kwa ajili ya lishe, majani
yake kama mboga ya kisamvu na dawa pamoja na miti yake inapokauka kutumika kama
kuni.
Inawezekana
hujui kama maganda ya mihogo baada ya kumenywa ni chakula bora cha mifugo
yakikaushwa au mabichi.
Siyo ajabu pia
hufahamu kwamba muhogo ukitwangwa mbichi na kuchujwa, maji yake yake yanatoa
wanga (starch) ambao hutumika
kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari
(sugar syrup) na pia ni lishe nzuri.
Lakini zao la
muhogo ni zaidi ya linavyofikiriwa kwa sababu licha ya faida hizo chache,
lakini pia linazalisha bidhaa zaidi ya 300 kama ambavyo akinamama wa Kijiji cha
Kitanga, Kata ya Msimbu wilayani Kisarawe wameamua kufanya.
Akinamama hao
kupitia kikundi chao cha Kisanga Green Voices mbali ya kuzalisha unga pamoja na
chips, sasa wanatengeneza bidhaa lukuki zenye ubora kama chapati, maandazi,
skonzi, biskuti, tambi, cassava chop, na nyinginezo nyingi.
Hatua hiyo
imekuja baada ya kupatiwa mafunzo kupitia mradi wa Green Voices unaofadhiliwa
na taasisi ya maendeleo ya wanawake wa Afrika inayojulikana kama Women for
Africa Foundation, ambayo iko chini ya Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, MarÃa Teresa Fernández de la Vega.
Baadhi
ya akinamama wa Kitanga Green Voices wakiwa wameushikilia muhogo pamoja na
viongozi wa kijiji na Kata ya Msimbu wilayani Kisarawe.
Kijana
akiwa amebeba muhogo baada ya kuchimba shambani.
Kuanzishwa kwa mradi huo wa
kusindika muhogo pamoja na bidhaa zake kumeliokoa zao hilo ambalo licha ya kuwa
na manufaa makubwa kwa jamii, lakini limekuwa likidorora hata katika soko la
vyakula.
“Tangu tumeanzisha
kikundi hiki miezi mitatu iliyopita hivi sasa muhogo hauwezi kuozea shambani na
wananchi wanaona umuhimu wa zao hilo,” anasema Mama Abia Magembe, ambaye ni
mratibu wa mradi huo.
Mama Magembe, ambaye yeyé pamoja na akinamama wengine
tisa walipatiwa mafunzo nchini Hispania kwa nia ya kuanzisha shughuli za
ujasiriamali unaoendana na utunzaji wa mazingira pamoja na kupambana na
mabadiliko ya tabianchi, anasema kwamba zao la muhogo sasa limepata thamani
kubwa kijijini hapo na wana uhakika wakulima wa wilaya ya Kisarawe wanaweza
kugeukia miradi kama hiyo ili kuongeza mnyororo wa thamani.
Akinamama 10 wanaofanya miradi mbalimbali ya ujasirimali
kupitia mradi wa Green Voices wanatoka mikoa
ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.
Silvera Mujuni,
Ofisa Chakula na Lishe wa Wilaya ya Kisarawe, anasema kwamba wilaya hiyo ina
fursa kubwa ya kusindika na kuchakata mazao mengi yatokanayo na muhogo kwa kuwa
zao hilo ndilo kuu kwa chakula na biashara.
Anasema kwamba,
ardhi katika vijijini vingi vya wilaya hiyo inastawisha muhogo kwa wingi, hivyo
ikiwa wananchi watajizatiti na kujifunza namna ya kuchakata bidhaa za muhogo
wanaweza kupata faida kubwa kiuchumi.
“Muhogo ndilo
zao kuu katika maeneo mengi ya wilaya hii ambayo haiwezi kustawisha mazao
mengine kama mahindi, hivyo ni vyema wananchi wakajifunza utengenezaji wa
bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo,” anasema Bi. Silvera
aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Wilaya hiyo na ambaye ndiye alikuwa akiwafundisha
akinamama hao namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Diwani
wa Kata ya Msimbu, Amina Lilomo, akizungumza na akinamama wa kikundi cha
Kitanga Green Voices wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Kijiji cha Kitanga
hivi karibuni.
Mshiriki
kiongozi wa Kitanga Green Voices Women Group, Mama Abia Magembe, akiwahamasisha
wanawake wenzake katika uzinduzi huo.
Awali Ofisa
Mtendaji wa Kijiji hicho, Wazir Yakoub Wazir, aliwataka akinamama hao wajipange
wasajiliwe rasmi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali na
taasisi nyingine za binafsi.
“Ofisi yangu
iko wazi wakati wote, mkitaka kwenda kusajiliwa wilayani hata leo niko tayari
kuwasaidia, nawaombeni mje niwasaidie hata namna ya kuandaa katiba ya kikundi
pamoja na taratibu nyingine,” alisema.
Naye Diwani wa
Kata ya Msimbu, Anna Lilomo, amesema atajitahidi – kwa kushirikiana na diwani
mwenzake wa viti maalum Mossy Sultan Kufurumbaya – kuwapigania akinamama hao
kwenye vikao vya Baraza la Madiwani ili waweze kupatiwa misaada na mikopo hata
kupitia katika asilimia 10 ya bajeti ya halmashauri ambayo hulenga kuwasaidia
wanawake na vijana.
“Bahati nzuri
sisi hapa ni madiwani wanawake, kwa hiyo tutalipeleka suala la akinamama hawa
kwenye Baraza la Madiwani na kuelezea umuhimu wa kuongeza thamani kwenye zao
letu la muhogo ili limkomboe mkulima,” alisema Diwani Lilomo.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi.
Secelela Balisidya, anasema kwamba anafarijika anapoona wanawake wakihamasika
kushiriki shughuli za maendeleo, hasa ujasiriamali unaolenga kupambana na
mabadiliko ya tabianchi.
“Suala la kuhakikisha uhakika wa chakula, kutokomeza
umaskini, kuwawezesha wanawake kiuchumi na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
ni mambo yaliyopewa kipaumbele katika Malengo Endelevu ya Dunia, hivyo wanawake
wanaotekeleza miradi ya Green Voices wanayatekeleza malengo hayo kwa wakati
mmoja,” anasema Secelela.
Diwani
wa Kata ya Msimbu wilayani Kisarawe, Amina Lilomo (kushoto) na Diwani wa Viti
Maalum, Mossy Sultan Kufurumbaya, wakiwa makini kusikiliza maelezo
kuhusu namna ya kusindika bidhaa mbalimbali kutokana na zao la muhogo.
Akinamama
wa Kitanga Green Voices wakiwa katika picha ya pamoja na mwandishi Tukuswiga
Mwaisumbe (kilemba cha njano).
Muhogo ni zao linalochukuliwa na wengi kama la ziada hasa
kwenye ukame, lakini wengi hulifanya kama mlo wa hamu bila kutambua kwamba zao
hilo lina manufaa makubwa kwa lishe na kibiashara.
Wengi wanauchukulia muhogo kama chakula cha maskini, hawa
wale wanaojitiahidi kulima zao hilo, huyapa kipaumbele mazao mengine kuliko
muhogo.
Lakini muhogo ni zao mojawapo ambalo linaweza kuiepusha
jamii na baa la njaa huku katika baadhi ya mataifa likitumika kama chanzo cha
nishati ili kukabiliana na bei ya mafuta na nishati nyinginezo.
Baa la njaa ni tatizo kubwa linalozikumba nchi nyingi barani
Afrika, Tanzania ikiwa miongoni mwazo, lakini licha ya watu kuhimizwa kulima
muhogo, bado wanalipuuza zao hilo na kuliona kama zao fulani la mizizi tu.
Katika mikoa kama Lindi na Mtwara ambayo kwa miaka mingi
inalima kwa wingi muhogo, chakula chao kikuu kilikuwa ugali wa muhogo.
Licha ya kudharauliwa kwa zao hilo, lakini siyo ajabu ukakuta
mlo wa siku hiyo umetokana na muhogo kasoro chumvi na nazi, kwani inawezekana
kuni zilizopikia ni matawi ya muhogo, ugali wa muhogo na kisamvu cha muhogo!
Na wakulima wengi katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara
wanakula ugali wa muhogo pale wanapokosa unga wa mahindi, ambapo wanaokula
ugali huo wa muhogo (Wazaramo wanasema ‘bada’ na Wamakua wanauita ‘matamba’)
huonekana maskini wa kutupa.
Leo hii wanapohamasishwa kulima muhogo kwa sababu ya
kustahimili ukame, bado wengi wanasuasua, lakini watakapoambiwa kwamba unga wa
muhogo unatoa bidhaa nyingi zenye faida kubwa, huenda wengi wakaligeukia zao
hilo na kulima kibiashara.
Inafurahisha sana siku hizi kuona watu wengi wakikimbilia
ugali wa muhogo hata hotelini, lakini hiyo bado haijatosha kulirasimisha zao hilo
ili liwe na tija kubwa.
Akinamama wa Kijiji cha Kitanga wanaweza kuwa mabalozi
wazuri wa zao hilo, kwa sababu tayari wameanza kutengeneza bidhaa mbalimbali
ambazo hata wananchi wa kijiji hicho wameshangazwa nazo baada ya kuzionja na
kuona ubora wake.
Kilimo cha muhogo siyo tu kitasaidia kukuza pato la mkulima,
lakini kinaweza pia kuokoa mazingira pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu
Dola za Marekani 20 milioni sawa na Shs. 42 bilioni zinazotumika kuagiza
chakula nje, jukumu ambalo kikundi cha Kitanga Green Voices kimeamua kulibeba.
Mashine
hizi ndizo zinazotumika kuuponda muhogo na kuucharanga kama chips. Kila kijiji
kikiwa nazo kinaweza kutengeneza unga bora wa muhogo ambao utazalisha bidhaa
mbalimbali.
Mihogo
ikiwa imeandaliwa tayari kwa kuchakatwa kwenye mashine.
Faida za muhogo ni nyingi kama zilivyoelezwa hapo juu,
lakini kwa msisitizo ni kwamba, unga wake hutumika kutengeneza vyakula
mbalimbali, baadhi ni uji na ugali, vitafunwa kama keki, mikate, skonzi,
biskuiti, mandazi, mafuta ya lishe, sabuni ya unga, kuni, mboga, huksi pamoja
na bidhaa nyingine nyingi
Mazao yanayopatikana katika mzizi wenyewe, miti na majani
huweza kuzalisha bidhaa anuwai za viwandani kama vifaa vya nguo, karatasi,
mafuta, kilevi, dawa za binadamu na plastiki wakati ambapo wanga hutumika
kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari
(sugar syrup).
Takwimu za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa,
Afrika ni bara la tatu duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalishaji
takriban tani milioni 102.6 kila mwaka.
Tanzania ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa
muhogo barani Afrika baada ya Nigeria, Ghana na Kongo DRC ambapo
inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha
muhogo, zao linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima ambapo
karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Mikoa inayozalisha muhogo kwa wingi
ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na
maeneo yote ya Zanzibar. Ukanda wa Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa
na ukanda wa kusini. Mkoa wa Ruvuma huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote Tanzania.
Muhogo ndilo zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada
ya mahindi.
Taarifa ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya
Mazao ya Chakula Tanzania (TIRDO) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi
kirahisi.
Hii ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi na
magonjwa au wadudu wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao
mengi katika ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.
Kwa mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga
mwingi baada ya viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na
kwamba asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.
Comments
Post a Comment