- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
TUMEONA
katika makala iliyotangulia kwamba,
mbuzi kama mnyama mwingine wa kufugwa, ana faida mbalimbali. Kwa wachache ambao
wanaofuga wanaweza kukwambia kwamba siyo kazi rahisi na huwezi kuwa tajiri!
Hilo siyo
kweli ikiwa kama utazingatia mbinu bora za utunzaji wa mifugo yako na kama
utaelewa faida zitokanazo za ufugaji huo, ambazo ndizo kichocheo kikubwa kwako
kuanzisha ujasiriamali huo.
Mbuzi
wanatoa samadi na ikiwa unalima pia, hasa kilimo hifadhi na kinachozingatia
uhifadhi wa mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali pamoja na kisichotumia
kemikali (organic farming), unaweza kuitumia samadi hiyo shambani na ukatoa
mazao bora ambayo kwa sasa yana soko kubwa kulinganisha na yale yanayotumia
kemikali.
Bustani za
mboga mboga, matunda, maua na mazao ya nafaka yanayotumia mbolea asilia ni
mazuri kwa afya ya binadamu na mifugo pia.
Lakini bado
kuna faida nyingine kwa samadi, ambayo mbali ya kuongeza rutuba kwenye ardhi ya
kupanda mimea pia inaweza kutoa kawi ya biogas, nishati ambayo utaitumia hata
kijijini kwa ajili ya kupikia na hivyo kuokoa matumizi ya mkaa yanayoendana na
ukataji ovyo wa miti.
Bidhaa
zingine za wanyama zinazoweza kuuzwa ili kupata pesa zinajumulisha ngozi, pembe
na kwato ambavyo hutumika katika viwanda kuzalisha bidhaa zingine.
Nimezungumza
katika makala ya Ufugaji Bora Wa Mbuzi Wa Maziwa, kwamba maziwa ya mbuzi ni mazuri kwa afya na yana ladha nzuri
kuliko ya ng’ombe, yakiwa na protini nyingi.
Ni mazurikwa lishe, rahisi kunywewa na yana viinilishe vingi kwa sababu yana madini
mengi ya kalsiumu, fosforasi na klorine kuliko maziwa ya ng’ombe.
Maziwa ya
mbuzi yana uwezo mkubwa wa kuongeza kinga katika mwili (immune) kwa watoto na
hata watu wazima. Kuna watu ambao hawawezi kunywa maziwa ya ng’ombe kwa sababu
wana mzio (allergy), lakini hakuna anayeweza kushindwa kunywa maziwa ya mbuzi.
Nasisitiza,
kwamba, ikiwa unafuga ng’ombe wa maziwa na mbuzi wa maziwa, nakushauri maziwa
ya mbuzi uyatumie nyumbani halafu ya ng’ombe ndiyo uyauze.
Nyama ya
mbuzi ni tamu sana na inaliwa na watu wengi.
Lakini mbali
ya maziwa na nyama, wafugaji wengi wa mbuzi wa maziwa wana faida kubwa ya
kutengeneza mtindi, siagi, samli na jibini, mazao ambayo yana soko kubwa.
Kimsingi, maziwa ya mbuzi yana mafuta mengi hivyo ni rahisi kupata siagi nyingi
zaidi.
Kwa upande
mwingine, mbuzi wanahitaji usimamizi mdogo kuliko ng’ombe. Mbuzi wana gharama
ndogo sana ya chakula kulinganisha na ng’ombe. Ng’ombe mmoja anaweza kula
chakula kinachowatosha mbuzi watatu mpaka sita kwa siku, kutegemeana na aina (breed)na mahitaji ya mbuzi husika. Mbuzi wanaweza kula nyasi, majani na magamba
ya miti na kadhalika, vyakula vingine ambavyo ng’ombe hawezi kula.
Faida
nyingine kwamba, mbuzi wanazaa mara mbili kwa mwaka wakati ng’ombe anazaa mara
moja. Ukipata bahati ya mbuzi wanaozaa mapacha, unaweza kuongeza mifugo ndani
ya muda mfupi. Kwa kawaida, mbuzi hubeba mimba kwa muda wa wiki 20 au miezi
mitano (siku 150) na hunyonyesha kwa miezi miwili. Kumbuka pia mbuzi pia ni
wastaarabu kuliko ng’ombe.
Kuhusu kiasi
cha maziwa unayopata kila siku, mbuzi hawako nyuma sana ya ng’ombe. Wakati
ambapo ng’ombe aliyetunzwa vizuri anaweza kutoa mpaka lita 15 au 20 kwa siku, mbuzi wa maziwa wa uzao bora na aliyetunzwavizuri anaweza kutoa mpaka lita 7 kwa siku na katika nchi ambayo mbuzi wa
kienyeji wanaweza kutoa lita 2 kwa siku, hii ni faida kubwa kuwa na mbuzi wa
maziwa.
Kwa maana
nyingine, kuwa na mbuzi watatu ni sawa na kuwa na ng’ombe mmoja, jambo ambalo
ni la faida pia, kwa sababu ikitokea ugonjwa ng’ombe huyo mmoja anaweza kufa,
lakini mbuzi watatu hawawezi kufa wote, unaweza kuwaokoa wengine, hivyo
kuendelea kuwa na maziwa.
Masoko
Kuuza maziwa ni suala la msingi. Kama unao mbuzi wengi ama wanazalisha maziwa
ya ziada, unaweza kuyauza ambapo bei yake ni zaidi ya mara mbili kwa ile ya
maziwa ya ng’ombe.
Tatizo wengi wanalalamika kwamba
watapata wapi soko la maziwa ya mbuzi. Ukiwa
mfugaji wa mbuzi wa maziwa huna haja ya kuhofia kuhusu uchakataji wa maziwa
yako ili utoe siagi, jibini na samli, kwa sababu soko la uhakika la maziwa
lipo, tena kubwa hata hapa Tanzania.
Nchini
Kenya, kwa mfano, wakati lita moja ya maziwa ya ng’ombe inauzwa kwa KShs. 40
(takriban Shs. 800 ya Tanzania), maziwa ya mbuzi yanauzwa kati ya KShs. 80 na
100 (TShs. 1,600 na 2,000) kwa lita.
Inawezekana hujalisikia soko la
maziwa kwa sababu wewe siyo mfugaji wa mbuzi wa maziwa, ama huyahitaji maziwa
hayo.
Lakini ukweli ni kwamba, kama ilivyo
kwa biashara nyingine, unapokuwa mfugaji wa mbuzi wa maziwa lazima utaanza
kutafuta soko na hapa nikwambie, kabla hujaanza kwenda kuuliza kwenye hoteli na
migahawa, wateja wako wa kwanza wanaweza kuwa jirani zako.
Hawa, mbali ya kuwa wateja, lakini
pia wanaweza kutumika kama ndio ‘maofisa masoko’ wako kwa sababu watakwenda
kueneza taarifa kwamba kwa Mbega kuna maziwa ya mbuzi. Wateja wengine ni
watengenezaji wa jibini na siagi.
Hata hivyo, kwa kuwa ufugaji huu wa
mbuzi wa maziwa unahamasishwa pia na serikali ili kumuondolea mwananchi
umaskini katika kutekeleza Mpango wa Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi
Tanzania (Mkukuta II) na Mpango wa Maendeleo Endelevu ya Dunia, ni wazi kwamba
unapokuwa mfugaji kuna mahali ambako utapata soko.
Katika kipindi hiki cha Awamu ya
Tano, hata Rais John Magufuli amekwishasisitiza kwamba anataka kuona ‘Tanzania
ya viwanda’ kwa kuhimiza viwanda vidogo vidogo vya kusindika bidhaa zitokanazo
na mazao ya kilimo na mifugo. Kwa hiyo, umoja wa wafugaji ukijizatiti unaweza
ama wenyewe kukusanya fedha kwa ajili ya kuanzisha kiwanda kidogo cha kusindika
maziwa ya mbuzi au kuwawezesha wakulima elimu ya namna ya kutengeneza wenyewe
samli, siagi na jibini.
Uwekezaji wa viwanda vikubwa mara
nyingi hutegemea na upatikanaji wa malighafi, lakini kama Watanzania wengi
watahamasishwa kufuga mbuzi wa maziwa na maziwa yakapatikana kwa wingi, haihitaji
kupiga baragumu kuwahimiza wawekezaji wajenge viwanda, bali wenyewe tu
watajenga kwa sababu malighafi zipo za kutosha.
Katika baadhi ya mataifa, wafugaji wa
mbuzi wa maziwa hugandisha maziwa yao na kuuza kama mtindi, lakini wengine
wamepatiwa utaalam na wanatengeneza wenyewe samli, siagi na jibini katika
kuongeza ubora na mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo.
Kutengeneza
jibini ya maziwa ya mbuzi ni rahisi. Inahitaji vifaa vichache au viungo ambavyo
havipo nyumbani. Utahitaji birika kubwa, vijiko, kisu kikubwa, nguo maalum ya
kuchujia jibini, kipimajoto maalum kwa ajili ya jibini (au chochote ambacho
kitakuonyesha kwamba maziwa yana joto kati ya nyuzi 86º na 100ºF) na viungo
vingine hasa rennet. Rennet, ambayo inapatikana katika vidonge au majimaji, inasaidia
kuigandisha na huwa ina maelekezo ya namna ya kutengeneza jibini.
Maziwa ya
mbuzi yanaweza kugandishwa na kuwa mtindi, tena mtamu sana.
Ngozi za
mbuzi zinaweza kutengenezwa bidhaa za ngozi kama mikoba na kadhalika. Manyoya
ya mbuzi ni mazuri kwa kazi mbalimbali zikiwemo nyuzi na weaving. Kwa ujumla,
kuanzia mwanzo hadi mwisho, mbuzi ndiye mnyama mwenye faida kubwa ambaye
anafugwa. Haishangazi kuona hivi sasa watu wengi wametambua umuhimu wake na
wameanza kuwafuga.
Soko ni muhimu, lakini wakati mwingine
lisiwe kikwazo kwako kwa kubuni mradi ambao unadhani kwamba unaweza kuleta
manufaa.
Vinginevyo tusingeweza leo hii kuwa
na simu, magari, ndege na mitambo kwa sababu hata wabunifu wa mambo hayo wakati
wanaanza utafiti wao hawakujiuliza kama kulikuwa na soko bali walitengeneza na
baadaye masoko yakapatikana, tena kwa wingi.
Jambo la msingi zaidi ili upate faida
katika mradi wako wa mbuzi wa maziwa ni kuhakikisha unakuwa na mpango wa mradi
(project plan) hata kama ni mdogo, halafu baadaye uwe na mpango wa biashara
(business plan) pamoja na mpango wa masoko (market plan). Hii itakusaidia sana
kuona unawekeza namna gani na utapata faida kiasi gani, baada ya muda gani na
wapi utauza bidhaa zako.
Muhimu tu ni kuweka rekodi zako
vizuri kuanzia unapoandaa banda la mifugo, kununua mbuzi, chakula, tiba na
mambo yote ikiwa ni pamoja na gharama nyingine za wahudumiaji (labour force).
Niwaambie tu ndugu zangu, hakuna kazi
rahisi duniani na wala hakuna kazi ngumu. Urahisi wa kazi unakuja kutokana na
kujitoa kwako na kuzingatia maadili ya kazi hiyo, vivyo hivyo, ugumu wa kazi
unakuja ikiwa hujazingatia misingi ya kazi husika.
Ukulima na ufugaji ni kazi rahisi
ukiwa na nia ya dhati, mpango na malengo. Kwa sasa inaonekana kuwa ngumu kwa
sababu siku zote tumekuwa tukilima ama kufuga kwa mazowea tu, hatuzingatii
misingi ya kilimo bora ama ufugaji wa kisasa ndiyo maana wengi wetu tunaendelea
kuogelea katika umaskini.
Ukikutana na mkulima ama mfugaji wa
miaka yote ambaye hajaona faida ya kile anachokifanya ukampa wazo hilo kwamba
na wewe unataka kuingia kwenye kilimo na ufugaji, anaweza kukukatisha tamaa
pengine hata kwa kumtazama tu. Lakini nakuhakikishia ndugu yangu, leo hii
unaweza kujiingiza kwenye ufugaji au kilimo na ukawa mfano wa kuigwa kutokana
na matunda utakayoyapata. Hata wale wazoefu wanaweza kuja kwako kujifunza.
Usikate tamaa.
Wakati mwingine ukipata nafasi nenda
kawatembelee wafugaji amba wakulima waliofanikiwa uone wametumia njia ama
teknolojia gani. Hiyo itakusaidia sana.
Zaidi jenga tabia ya kujisomea mambo
mbalimbali, tembelea hapa MaendeleoVijijini kila mara ili ujifunze mambo mbalimbali pamoja na kusoma ama kusikiliza shuhuda
za watu waliofanikiwa katika miradi mbalimbali.
Usijiulize mara mbili wala usianze
kuwaza mambo ambayo yatakuwa vikwazo kwako kabla hujaanza. Anza kufuga mbuzi wa
maziwa, halafu faida yake utaiona.
Comments
Post a Comment