Featured Post

CHATO WAITAMANI DHAHABU YA KIJANI ILIYOPO WILAYA YA MUFINDI


Mkuu wa msafara huo Mkuu wa Wilaya ya Chato Eng. Mtemi Msafiri akipata maelezo kutoka kwa mkurugenzi wa Rasilimali Misitu na Nyuki TFS, Zawadi Mbwambo jinsi gani wanavyoweza kuzalisha miche ya miti ambayo inakuwa kwa muda mfupi sana.
Mkuu wa msafara huo Mkuu wa Wilaya ya Chato Eng. Mtemi Msafiri akiwa na baadhi ya viongozi wa kutoka mkoa wa Geita walipokuwa kwenye ziara ya kutembelea shamba la miti ya kupandwa la Sao Hill lililopo mkoani Iringa
Moja kati ya maeneo ambayo yanatumika kuzaliSHa miche ya miti.

NA FREDY MGUNDA, IRINGA
Uchumi wa wilaya ya Mufindi mkoani Iringa umetajwa kutegemea zao la miti katika kukuza uchumi na kuongeza pato la taifa tofauti ya wilaya nyingine kama Chato ambao wamekuwa wakitegemea ufugaji,uchimbaji wa dhahabu,uvuvi na kilimo.
Hiyo imebainika wakati wa ziara ya baadhi ya viongozi wa wilaya ya Chato,Mkoa wa Geita na viongozi wa vijiji vinavyolizunguka Shamba la Miti la Biharamulo lililopo mkoani Geita baada ya kutembelea Shamba la Miti Sao Hill linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za uendeshaji katika shamba hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa msafara huo Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Eng. Mtemi Msafiri alisema kuwa kwa mara ya kwanza amejifunza faida kubwa inayotokana na zao la miti katika kukuza uchumi wa nchi na kujionea jinsi gani wananchi wa wilaya ya Mufindi wanavyonufaika na dhahabu ya kijani
“Leo ndio nimegundua kuwa zao la miti ni dhahabu ya kijani kwa namna inavyosaidia kukuza uchumi tofauti na walivyodhani hapo awali kwa namna ambavyo wao wamekuwa wakitegemea kuchimba dhahabu ambazo hazionekani tofauti na zao la miti ambavyo limekuwa linaonekana,” alisema Eng Msafiri.
Eng Msafiri alisema kuwa shamba la Miti Sao Hill ndilo shamba kubwa zaidi kati ya mashamba yote ya Serikali na ni nguzo ya maendeleo, na mkombozi wa mazingira wa Wilaya ya Mufindi na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nasi tumeona ni vema tujifunze kutoka kwa wenzetu.
“Tumejionea jinsi shamba hili lilivyo kuwa dhahabu ya ukuaji wa sekta ya viwanda vidogo na vikubwa vya uchakataji wa mbao,  linavyosaidia kuongezeka kwa ari ya upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa wananchi wanaozunguka shamba na wananchi wa Wilaya za Mufindi, Kilombero na jamii jirani wamekuwa wakipatiwa gawio la asilimia 5 ya mrahaba kila mwaka”alisema Eng. Msafiri.
Eng. Msafiri anasema ziara hiyo imeweza kuwafumbua macho na kuona jinsi gani shamba hilo lilivyo toa  fursa ya ajira zinazotokana na kazi za msimu za mashambani na viwanda tegemezi vya mazao ya misitu, fursa za uwekezaji,  na ufugaji wa nyuki unaotokana na na uwepo wa misitu ya asili na ile  ya kupandwa pamoja na vyanzo mbalimbali vya maji.
Awali akitoa ufafanuzi wa shamba la Sao Hill mkurugenzi wa Rasilimali Misitu na Nyuki TFS, Zawadi Mbwambo alisema shamba hilo ni miongoni mwa mashamba 23 ya miti ya kupandwa ya serikali ambayo yanasimamiwa na wizara ya maliasili na utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
“Shamba la Sao Hill lililopo hapa Mufindi lilianzishwa kwa majaribio mnamo mwaka 1939 hadi mwaka 1951 na upandaji kwa kiasi kikubwa ulianza rasmi mwaka 1960  hadi 1980 na shamba hilo linaukubwa wa hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwa ajili ya upandaji wa miti  na uhifadhi wa mazingira,” alisema Mbwambo.
Mbwambo alisema shamba hilo limehamasisha kwa kiwango kikubwa upandaji wa miti kwa jamii inayolizunguka ambapo pia hutoa msaada wa mafunzo na miche ya miti kwa ajili ya kupandwa ili kupambana na uharibifu mkubwa wa misitu unaoendelea nchini.
 “Takribani hekta 372,000 ya misitu inapotea kila mwaka na ili misitu hii isiweze kupotea tunatakiwa tuendelee kupanda angalau hekta 185,000 kwa mwaka kwa hapa Mufundi na Ukanda wote wa Nyanda za Juuu Kusini hamasa ya kupanda miti imekuwa kubwa kutokana na thamani inayoonekana Sao Hill kiasi kwamba imefikia hatua sasa Serikali inawaelimisha watu waache baadhi ya maeneo kwa ajili ya kilimo cha mazao mengine ya chakula na biashara” Alisema Mbwambo.
Kwa upande wake meneja wa Shamba la Miti la Biharamulo Thadeus Shirima alisema kupitia ziara hiyo ya siku mbili anaamini sasa kutakuwa na uelewa wa pamoja wa umuhimu wa shamba hilo katika kuleta maendeleo katika Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla.
Thadeus alitoa shukurani kwa Mkuu wa Wilaya ya Chato, kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Chato na Mkoa wa Geita, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Bukombe kwa msaada na maelekezo yao muhimu yaliyosaidia kuhakikisha uanzishwaji wa Shamba la Miti la Biharamulo unafanikiwa kwa kufanikisha kuwaondoa wananchi waliovamia msitu wa hifadhi Biharamulo ili kuanzishwa shamba hilo la miti.
Ziara hiyo ina wajumbe 45 ambao vingozi wa Wilaya na Mkoa wa Geita, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mkurugenzi wa halmashauri,Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani, Maafisa tarafa, Jeshi la Zima moto na uokoaji, Mwenyekiti na katibu wa Chama cha Mapinduzi, baadhi ya Wakuu wa Vitengo na Idara za Halmashauri ya Wilaya, baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ,  Katibu Tawala wa Wilaya na Wataalamu kutoka Shamba la miti Biharamulo.

Comments