Featured Post

WATUMISHI WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO WATAKIWA KUBORESHA ZAIDI MIFUMO YA UKUSANYAJI MAPATO YA SERIKALI


Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), (watatu kushoto) wakiimba wimbo wa kudumisha umoja kabla ya kuanza Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, Jijini Dodoma.

Na Farida Ramadhani & Josephine Majura, WFM, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji , amewataka  Watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato ya ndani na kupanua wigo wa walipakodi pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, wizarani hapo.
Alisema Wizara ya Fedha na Mipango imebeba majukumu ya  kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali na matumizi ya rasilimali fedha yanasimamiwa kikamilifu.
“Watendaji na watumishi wote wa Wizara wanawajibu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na ufuatiliaji wa matumizi ili kuhakikisha rasilimali fedha zilizopo zinatumika kwa ufanisi” ,alisema Dkt. Kijaji.
Alisema ni jukumu la Watumishi wa Wizara kugawa rasilimali fedha kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016-2021)  wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.
Aliwataka Watumishi  kufanyakazi kwa ushirikiano, umoja , mshikamano, ufanisi  na uadilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyopo.
“Ni wajibu wetu pia kutumia busara na hekima, hususan pale tunaposhughulikia maslahi ya watumishi na wananchi kwa ujumla”, alisisitiza Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni  Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Doto James, amemhakikishia Dkt. Kijaji kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kwa haraka na ukamilifu kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa Wizara hiyo ni nguzo ya kusimamia uchumi wa nchi.
Alisema uzoefu unaonesha kwamba vikao vya Baraza la wafanyakazi vimekua na umuhimu mkubwa mahala pa kazi na kwa kuzingatia umuhimu huo Wizara ya Fedha na Mipango imehakikisha kuwa vikao vya Baraza vinafanyika kila mwaka kulingana na Mkataba kati ya Wizara na Chama cha Wafanyakazi cha Serikali na Afya (TUGHE).
Alisema kupitia Baraza la wafanyakazi Wizara imefanikiwa kuongeza mshikamano kati ya Wafanyakazi hivyo kuamsha ari kwa watumishi kufanya kazi kwa kushirikiana na Viongozi wa Serikali.
Aliongeza kuwa hoja mbalimbali zilizowasilishwa kwenye Baraza zimeboresha huduma kwa watumishi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ikiwemo kuwapatia watumishi vitendea kazi pamoja na kuwelimisha watumishi kuhusu magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la damu (BP), Kifua kikuu, HIV na UKIMWI.
Katibu Mkuu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Bw. Doto James akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) kabla ya kuanza Baraza la Wafanyakazi wa Wazara hiyo lililofanyika katika ukumbi wa Kambarage Jijini Dodoma.
Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiimba wimbo wa kudumisha umoja na mshikamano "solidarity forever"  kabla ya kuanza Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kushoto) akimtambulisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kuapishwa hivi karibuni , Bw. Adolf Ndunguru, katika Baraza la Wafanyakazi wa Wazara hiyo , Dodoma.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Katibu Mkuu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Bw.Doto James akitoa salam za utangulizi kwa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani),  wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Jijini Dodoma.
Sehemu ya Wajumbe walioshiriki Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani), katika ukumbi wa Kambarage Dodoma ambapo Watendaji wa Wizara walitakiwa kutekeleza jukumu la kugawa rasilimali fedha kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji  (Mb), akizungumza wakati wa kufungua Baraza la Wafanyakazi, Jijini Dodoma, ambapo aliagiza Watendaji wa Wizara hiyo kuendelea kuboresha mifumo ya kukusanya mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa walipa kodi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji  (Mb), akipongezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.Doto James, baada ya kumaliza hotuba yake alipofungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasilino Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)


Comments