Featured Post

UIMARISHAJI MPAKA WA TANZANIA NA KENYA WAENDELEA KWA KASI

Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi akitoa maelekezo kwa timu ya ukaguzi wa Tanzania na Kenya katika eneo la Namanga mkoani Arusha kuhusiana na kigingi cha mpaka kilichoanguka eneo la Namanga baada ya kutembelea kuona ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya kuimarisha mpaka wa nchi hizo kutoka eneo la Ziwa na Natron hadi Namanga. Kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Ukaguzi kwa upande wa Tanzania kutoka Wizara ya Ardhi Joseph Ikorongo.

Mkuu wa Kikosi cha Ukaguzi wa mpaka wa Tanzania na Kenya kwa upande wa Tanzania kutoka Wizara ya Ardhi Joseph Ikorongo akimuonesha Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi (Wa pili Kulia) muelekeo wa alama ya mpaka kati ya nchi hizo eneo la Namanga mkoani Arusha wakati alipotembelea kuona ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya uimarishaji mpaka wa nchi hizo kutoka eneo la Ziwa na Natron hadi Namanga.


Na Munir Shemweta, NGORONGORO
Kazi ya uimarishaji mpaka wa Tanzania na Kenya kuanzia eneo la Ziwa Natroni katika wilaya ya Ngorongoro hadi Namanga wilaya ya Longido mkoani Arusha inaendelea kwa kasi kubwa na sasa ukaguzi kwa ajili ya kuimarisha mpaka huo umekamilika.
Ukaguzi wa mpaka katika eneo hilo unafuatia kukamilika zoezi la uimarishaji mpaka kwa kuweka alama za mipaka ya nchi hizo mbili kuanzia Ziwa Victoria mkoani Mara hadi Natron wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa umbali wa kilomita 238.
Tayari timu za wataalamu kutoka nchi za Tanzania na Kenya zimefanya ukaguzi eneo la mpaka kuanzia eneo la Natroni wilaya ya Ngorongoro hadi Namanga wilaya ya Longido ambapo timu hizo zimeainisha mahitaji ya uimarishaji mpaka huo na kilichobaki ni uwasilishaji ripoti.
Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi mwishoni mwa wiki alitembelea mpaka wa nchi za Tanzania na Kenya kijiji cha Engoserosambu, eneo karibu na Ziwa Natron la cha Nani katika wilaya ya Ngorongoro pamoja na Namanga wilaya ya Longido mkoani Arusha kwa ajili ya kujionea kazi ya ukaguzi iliyofanyika ikiwa ni maandalizi ya uimarishaji mpaka.
Katika ziara hiyo Katambi alijionea jinsi wataalamu wa nchi mbili za Tanzania na Kenya walivyoshiriki katika kazi ya ukaguzi kwa nia ya kuanisha mahitaji ya uimarishaji mpaka kwa kuwekaji alama kwenye maeneo ambayo vigingi vya mipaka vimeharibika ili kupata picha halisi kwa ajili ya kuhuisha mpaka huo.
Kwa mujibu wa Katambi, ukaguzi wa mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la kuanzia  Natroni hadi Namanga ni matokeo ya mkutano wa Narok uliofanyika nchini Kenya ambapo nchi husika zilikubalina kabla ya kuanza kazi ya kuimarisha mpaka zifanye ukaguzi ili kujua mahitaji halisi wakati wa kuimarisha mpaka.
‘’Ukaguzi ni muhimu sana ili kuwa na bajeti halisi ya kazi, kufahamu ni vigingi vingapi vinahitajika kuongezwa na umbali wa kuweka vigingi hivyo sambamba na njia za kupitisha vifaa wakati wa ujenzi wake’’ alisema Katambi
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi alisema, zoezi hilo la uimarishaji mpaka wa Tanzania na Kenya litakapokamilika litaendelea maeneo mengine kutoka Namanga kuelekea mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Tarakea mkoani Kilimanjaro, Hororo hadi kijiji cha Jasini kilichopo wilaya ya Mkinga mkoa wa Tanga na hivyo kukamilisha uimarishaji  mpaka huo wenye urefu wa kilomita 760 kutoka Ziwa Victoria hadi Jasini.
Mkuu wa Kikosi Kazi cha Ukaguzi Uimarishaji Mpaka wa Tanzania na Kenya kwa upande wa Tanzania Joseph Ikorongo kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, zoezi la ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya uimarishaji mpaka wa nchi hizo mbili eneo la Ziwa Natron hadi Namanga limeenda vizuri na jumla ya kilomita 128 zimeshakaguliwa na lengo la ukaguzi huo ni kuandaa taarifa ya kina itakayowezesha kuwa na mpango kazi halisi.
Kwa mujibu wa Ikorongo, ukaguzi huo umehusisha kipande cha eneo ambalo halijawahi kuwekewa alama tangu enzi za ukoloni la Ziwa Natroni kati ya kijiji cha Nani na Jema lenye urefu wa kilomita 20 na eneo la kilomita 110 lilokuwa na alama kati ya kilomita moja hadi mbili.
Mkuu huyo wa Kikosi kazi cha Ukaguzi wa mpaka kwa upande wa Tanzania alibainisha kuwa, katika ukaguzi huo, kikosi kazi kimebaini jumla ya alama 47 zikiwa imara huku alama 11 zikihitaji kujengwa upya na alama 3 zikihitaji marekebisho.
Ikorongo alisema, eneo la mpaka kuanzia Ziwa Victoria mkoani Mara hadi Jasini mkoa wa Tanga lenye urefu wa kilomita 760 ndiyo eneo refu la mpaka ukilinganisha maeneo mengine ya mipaka ya Tanzania na   nchi jirani.

Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi akiangalia moja ya kigingi cha mpaka kilichowekwa katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la kijiji cha Engoserosambu wilaya ya Ngorongoro wakati alipotembelea kuona ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya kuimarisha mpaka wa nchi hizo kutoka eneo la Natron hadi Namanga. Kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Ukaguzi upande wa Tanzania kutoka Wizara ya Ardhi Joseph Ikorongo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi (Kulia) akielekea kuangalia moja ya alama za mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la kijiji cha Engoserosambu wilayani Ngorongoro wakati alipotembelea kuona ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya uimarishaji mpaka wa nchi hizo kutoka eneo la Ziwa Natron hadi Namanga. Kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Ukaguzi kwa upande wa Tanzania kutoka Wizara ya Ardhi Joseph Ikorongo.
Mkuu wa Kikosi cha Ukaguzi kwa upande wa Tanzania kutoka Wizara ya Ardhi Joseph Ikorongo (Wa pili Kulia) akimuonesha Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi (Wa pili Kushoto) muelekeo wa alama ya mpaka kati ya Tanzania na Kenya katika kijiji cha Engoserosambu Loliondo wilaya ya Ngorongoro mkoa wa Arusha wakati alipotembelea kuona ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya uimarishaji mpaka wa nchi hizo kutoka eneo la Ziwa na Natron hadi Namanga.

Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi akioneshwa eneo unapopita mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Namanga mkoani Arusha na Afisa aliyeshiriki ukaguzi wa mpaka huo kutoka Wizara ya Ardhi John Solwa wakati alipotembelea kuona ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya uimarishaji mpaka wa nchi hizo kutoka eneo la Ziwa na Natron hadi Namanga. Kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Ukaguzi kwa upande wa Tanzania kutoka Wizara ya Ardhi Joseph Ikorongo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi akiangalia kigingi cha mpaka kati ya Tanzania na Kenya kilichoanguka katika eneo la Namanga mkoani Arusha baada ya kutembelea kuona ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya uimarishaji mpaka wa nchi hizo kutoka eneo la Ziwa na Natron hadi Namanga. Kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Ukaguzi kwa upande wa Tanzania kutoka Wizara ya Ardhi Joseph Ikorongo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Samuel Katambi (wa sita waliosimama) akiwa katika picha ya pamoja na kikosi kazi kilichoshiriki kazi ya ukaguzi mpaka wa Tanzania na Kenya baada ya kutembelea kuona ukaguzi kwa ajili ya maandalizi ya uimarishaji  mpaka wa nchi hizo kutoka eneo la Ziwa na Natron hadi Namanga. Kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Ukaguzi kwa upande wa Tanzania kutoka Wizara ya Ardhi Joseph Ikorongo. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA-WIZARA YA ARDHI)


Comments