Featured Post

NAIBU WAZIRI WA MAJI AWESO AMPA KONGOLE DK ANGELINE MABULA


 NAIBU WAZIRI WA MAJI AWESO AMPA KONGOLE DK ANGELINE MABULA

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akipanda katika Tanki la maji kujionea ujenzi wa tanko hilo wakati Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso alipokagua  miradi ya maji katika Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza.


Na Munir Shemweta, ILEMELA
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametembelea miradi ya Maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa jitihada za kuwapatia wananchi wa jimbo hilo huduma ya maji safi na salama.

Katika ziara hiyo Aweso alijionea changamoto mbalimbali zinazoikabili miradi ya maji katika manispaa hiyo pamoja na kero ya maji wanayoipata wananchi wa Kata ya Bugogwa yenye mitaa kumi na tano na wakazi wapatao 32,000 ambao kwa muda mrefu hawana huduma ya maji licha ya juhudi za mbunge wa jimbo la Ilemela Dk Mabula kuwachimbia visima.
Mbunge wa Jimbo hilo Dk Mabula ameiomba Wizara ya Maji kuwapatia wananchi wa kata ya Bugogwa huduma ya maji katika mradi wa maji vijijini kutokana na chanzo cha maji cha mradi huo kupitia eneo lao.
Kwa Mujibu wa Dk Mabula, pamoja na chanzo cha mradi wa maji vijijini kuwa katika kata ya Bugogwa jimboni humo lakini wananchi wake hawajajumuishwa kwenye mradi jambo linaloleta sintofahamu kwa wakazi hao ambao sasa wanaona kutengwa na serikali  jambo alilolieleza kuwa linaweza hata kutishia usalama wa mradi.
Alisema, njia pekee ya kuwafanya wananchi wa kata ya Bugogwa kufurahia matunda ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ni kuwapatia huduma ya maji safi na salama kitendo kinachotafsiriwa kama kumtua ndoo mama kichwani.
Kufuatia ombi hilo, Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso alimuagiza Mhandisi wa Maji katika Manispaa ya Ilemela Anna Mawala pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Mwanza (MWAUWASA) Injinia Anthony Sanga  kushirikiana kuandaa mpango mdogo utakaowezesha wakazi wa kata nao kufaidika na mradi na mapendekezo hayo yawasilishwe wizarani mapema ili kufanyiwa kazi.
Aweso alisema kuwa, Wizara ya Maji haiwezi kuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma ya maji kwa kuwa huduma hiyo haina mbadala hivyo Serikali itafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi hao wanapata huduma ya maji safi na salama ili kuondokana na kero ya muda mrefu.
Mtendaji wa Kata ya Bugogwa Manispaa ya Ilemelea mkoa wa Mwanza Rashid Sukwa alisema kata yake imekuwa na tatizo la maji kwa muda mrefu pamoja na juhudi za mbunge wa jimbo hilo Dk Mabula kusaidia kuchimba visima lakini baadhi ya wananchi wanatumia visima vya asili.
Ameitaja baadhi ya mitaa yenye changamoto kubwa ya maji katika kata hiyo kuwa ni pamoja na Lugezi, Igombe A na B, Bugogwa, Kigote, Bugigwa, Kabaganja, Kasamwa, Kayenza Ndogo, Kisonde, Kilabela, Isanzo, Igogwe pamoja na Nkoronto.
Mmoja wa wakazi wa Bugogwa Janet Lusia alimshukuru Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa kuona umuhimu wa wananchi wa kata hiyo nao kufikiriwa kupata maji katika mradi huo kwa kuwa wametaabika kwa muda mrefu pamoja na jitihada za mbunge wao kuwachimbia visima.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso Akielekea kukagua tanki la Maji katika mradi wa Igogwe katika Manispaa ya Ilemela wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua miradi ya maji mkoani Mwanza. Wa pili kulia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Wazari wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula.
 Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso (wa tatu kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mijini mkoani Mwanza Injinia Anthony Sanga wakati wa wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua miradi ya maji mkoani Mwanza. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso (wa pili kulia ) akimsikiliza Mhandisi wa Maji katika Manispaa ya Ilemela Anna Mawala wa wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua miradi ya maji mkoani Mwanza. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso (wa pili kushoto) akiangalia ujenzi wa mradi wa maji katika kata ya Bugogwa Manispaa ya Ilemela wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua miradi ya maji mkoani Mwanza. Wa tatu kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza baada ya Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso kukagua miradi ya maji katika jimbo la Ilemela mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wanaojenga tanki la maji katika mradi wa maji vijijini eneo la Igogwe Manispaa ya Ilemela Mwanza wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua miradi ya maji mkoani Mwanza. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA)


Comments