Featured Post

MAWAZIRI WATANO WAKAGUA MSITU WA MAKERE KIGOMA Inbox x


 MAWAZIRI WATANO WAKAGUA MSITU WA MAKERE KIGOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akikatiza katika moja ya vichaka vilivyopo kwenye hifadhi ya Msitu wa Makere Kasulu Kigoma wakazi wa ziara ya Mawaziri watano kukagua msitu.

Na Munir Shemweta, WANMM Kasulu
Mawaziri watano wakioongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jafo wamekagua hifadhi ya  Msitu  wa Makere Kusini  uliopo wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma kwa takriban saa tano ili kubaini changamoto mbalimbali za msitu huo na kuzipatia ufumbuzi.
Mawaziri hao ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangala, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Musa Sima.
Ziara ya mawaziri hao katika hifadhi ya msitu huo ambao pia unatambulika kama Kagera Nkanda ambayo ni ya kihistoria kutokea hapa nchini ilianza majira ya saa saba mchana jana Mawaziri hao wakitokea wilayani Kigoma ambako walikuwa na kikao cha utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi katika hifadhi ya Msitu na Pori la Akiba Moyowosi mkoani Kigoma na kumaliza ukaguzi majira ya saa kumi na mbili jioni.
Baada ya kumaliza ukaguzi katika Msitu wa Makere Kusini, Mawaziri hao watano walielekea kijiji cha Kabulanzwili na kukagua mpaka baina ya kijiji hicho na hifadhi ya msitu huo kwenye mto Migezibiri na baadaye kukutana na wananchi wa kijiji hicho kwa lengo la kuwaeleza nia ya serikali kunuru hifadhi ya msitu ambapo walizungumza nao hadi saa moja na nusu usiku.
Wakazi wa kijiji cha Kabulanzwili waliwapokea mawaziri hao kwa mabango wakionesha kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa na askari wa wanyama pori kuwaondoa kwa nguvu wananchi  wanaoendesha shughuli za kilimo na ufugaji kwenye hifadhi hiyo huku baadhi yao wakidai kutofahamu mipaka halisi baina ya kijiji na hifadhi.
Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Magharibi Valentine Msusa alisema eneo lote la hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini linalopakana na Halmashauri za wilaya za Kasulu na Uvinza lina ukubwa wa hekta 72,000 lakini baada ya hekta 10,000 kutolewa kwa wananchi sasa imebakia na hekta 62,000.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kabulanzwili Nolvet Mtana alieleza kuwa awali waliambiwa waendelee na shughuli za kilimo katika maeneo waliyoanza kufanya shughuli hiyo bila kuanzisha maeneo mapaya lakini wameshangazwa na uamuzi wa kuwaondoa katika maeneo hayo kinyume na kauli ya awali jambo walilolieleza linawafanya waishi maisha ya wasiwasi.
Mkazi mwingine Kidaga Tito alisema hata kama wao walivamia eneo la hifadhi basi  ni vyema wakapewa muda kuvuna mazao yaliyopo shambani ili kuepuka hasara na kutaka mipaka kati ya hifadhi na kijiji iwekwe wazi ili ifahamike kuepuka wananchi kuingia ndani ya hifadhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula aliwaeleza wananchi wa kijiji cha Kabulanzwili kuwa, tatizo lilipo katika kijiji hicho ni kukosekana mpango wa matumizi bora ya ardhi na kubainisha kuwa suala hilo halihitaji wizara bali kijiji chenyewe kupitia watendaji wake kuanza mchakato wa kupanga maeneo kama vile kilimo, ufugaji, makazi na maeneo ya huduma za jamii.
Aliwataka wananchi wa kijiji hicho kukaa pamoja na kupanga maeneo kulingana na mahitaji na kuacha ile dhana ya kutaka baadhi ya wananchi waliohamia kuondoka na kubainisha kuwa cha msingi ni kujua idadi na mahitaji ya wakulima na wafugaji pamoja na maeneo ya huduma za jamii na halmashauri ya wilaya ya Kasulu na serikali ya kijiji zinapaswa kupanga maeneo na kazi ya wizara yake itakuja kuanisha mipaka na hapo hakutakuwa na migogoro tena.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jafo alieleza kuwa ujio wa mawaziri hao watano ni wa kihistoria na unaangalia changamoto zinazokabili hifadhi ya msitu wa Makere sambamba na kuona namna bora ya kutatua tatizo linalowakabili wananchi wa eneo linalozunguka hifadhi ya Msitu huo ambapo aliwataka kukubaliana na maamuzi yoyote ya serikali yatakayofikiwa kwa kuwa maamuzi hayo yatakuwa kwa maslahi ya taifa.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Luteni Simon Anange aliwaeleza wananchi wa Kabulanzwili kuwa ujio wa mawaziri watano katika eneo la hifadhi ni kuangalia namna bora ya kuitunza misitu ya Makere na Mvuti iliyopo Kasulu Kigoma ambayo imeanza kuharibika kutokana na uwepo wa shughuli za kilimo na ufugaji na kueleza kuwa kazi ya kushughulikia suala hilo bado haijafika mwisho na kinachofanyika sasa ni kuangalia namna bora ya kunusuru msitu huo.
Hifadhi za Misitu na Mapori ya Akiba ya Moyowosi yamekuwa na mgogoro kwa muda mrefu kutokana na wananchi kuendesha shughuli za ufugaji katika hifadhi za misitu na mapori ya akiba, uchomaji mkaa, uchimbaji haramu wa madini ya chokaa, uwepo silaha za kijeshi, uvunaji haramu mazao ya misitu na uendeshaji kilimo cha mazao ya chakula jambo lililopelekea Katibu Mkuu kiongozi kuandika barua kwa Makatibu Wakuu wa Wizara husika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo Novemba 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Luteni Simon Anange akiwaonesha Mawaziri Dk Hamis Kigwangala Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Angeline Mabula Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Suleiman Jafo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Musa Sima pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina eneo la hifadhi la Msitu wa Makere lililopo Kasulu Kigoma walipofanya ziara katika hifadhi hiyo kujionea changamoto mbalimbali ndani ya Msitu huo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jafo akiwaongoza Mawaziri wenzake kukagua maeneo mbalimbali katika hifadhi ya Msitu wa Makere Kasulu Kigoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jafo (wa pili kushoto) , Dk Hamis Kigwangala Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Angeline Mabula Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Musa Sima wakiangalia ndege inayochukua picha angani (Drones) wakati wakikagua hifadhi ya Msitu wa Makere uliopo Kasulu Kigoma.
Mawaziri Dk Hamis Kigwangala Waziri wa Maliasili na Utalii, Suleiman Jafo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Musa Sima, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina na Dk Angeline Mabula Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakiwasikiliza wananchi wa kijiji cha Kabulanzwili alipofanya ziara katika eneo la hifadhi la Msitu wa Makere Kasulu Kigoma.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kabulanzwili kilichopo Kasulu Kigoma wakati wa ziara ya Mawaziri watano kukagua eneo la hifadhi la Msitu wa Makere.

Comments