Featured Post

WALIOMALIZA CHUO KIKUU CHA USHIRIKA MOSHI WAHAMASISHWA KUCHANGIA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA CHUO HICHO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt Anna Mghwira akizungumza wakati wa uzinduzi wa Harambee  ya kuchangia ujenzi wa miundombinu katika Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi (MoCU).

Baadhi ya Watumishi wa Chuo Kikuu cha Ushirika ,Moshi (MoCU) wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ,Dkt Anna Mghwira wakati wa uzinduzi ya kuchanga ujenzi wa Miundombinu ikiwemo Hosteli katika chuo hicho. 
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi (MoCU) Prof. Faustine Bee akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katik aukumbi wa mikutano wa Ushirika.
Baadhi ya Viongozi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) wakiwa katika mkutano huo wa uzinduzi . 
Mwenyekiti wa Kamati ya Harambee ya kuchangia ujenzi wa Miundombinu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Noel Nko ambaye pia ni mhitimu wa chuo hicho akizungumza juu ya wazo la kuwashirikisha Wahitimu wote wa Chuo hicho tangu mwaka 1963 katika kuchangia ujenzi wa miundombinu Chuoni hapo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof ,Faustine Bee akimueleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Dkt Anna Mghwira alipotembelea baadhi ya maeneo katika Chuo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Dkt Anna Mghwira akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Ushirika ,Moshi (MoCU) mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi wa Harambee ya kuchangia ujenzi wa miundombinu katika chuo hicho.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii, Kanda ya Kaskazini 

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) wanaoishi katika hosteli za nje ya chuo hicho wako kwenye mazingira hatarishi kutokana na baadhi yao kufanyiwa vitendo vya kinyama huku ikidaiwa wengine tayari wamepoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

Matukio mengine yanayotajwa kuwafika Wanafunzi hao ni pamoja na kuvamiwa na kuporwa mali ,kujeruhiwa kwa kuchomwa visu na kupigwa hasa kwa wanafunzi wa jinsia ya Kike jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limechangia baadhi yao kuathirika kimasomo na hata kupunguza hali ya kuendelea na masomo.

Kutokana na hali hiyo, Wahitimu wa Chuo hicho kuanzia mwaka 1963 wameanza kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa hosteli yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 ili kupunguza changamoto zilizopo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Harambee hiyo Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Dkt Anna Mghwira amesema miundombinu ya Chuo kikuu cha Ushirika Moshi haikidhi mahitaji ya sasa na ya baadae kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kwamba kwa kiasi kikubwa inahitaji kuboreshwa.

Dkt Mghwira amesema hosteli zilizopo sasa zilizojengwa miaka ya 60 na 70 , pamoja na kuwa katika hali ya uchakavu zinauwezo wa kuchukua wanafunzi 766 tu ikiwa ni sawa na asilimia 20 ya idadi ya wanafunzi waliopo na ambayo inaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka .

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika ,Moshi (MoCU) Prof ,Faustine Bee alisema jambo ambalo limeibuliwa na wahitimu wa chuo hicho ni jema na kwamba Uongozi wa chuo utaendelea kuwaonga mkono katika jitihada hizo.

“Niwashukuru kwa kuja na wazo hili ,nimpongeze Noel Nko ambaye amejitolea kuwaongoza wenzake katika jambo hili,sisi kama viongozi na wadau tunawashukuru na tunawaunga mkono kaitka jitihada hizi,mchango wao ni mkubwa na unachangia katika kuunga mkono juhudi za rais Magufuli ya kuona  taasisi za elimu zinakuwa na mundombinu iliyobora”alisema Prof Bee .

Alisema uwepo wa  miundombinu bora kutatoa nafasi kwa wanafunzi kujifunza  kwa bidii huku akiishukuru Serikali kwa kutoa kiasi cha Sh Bil 1.3 ambazo tayari zimesaidia katika kuboresha baadhi ya miundombinu ya chuo hicho.

“Hata hivyo bado hatujakamilisha ,tunamahitaji mengine makubwa kama barabara za ndani hazijakamilika,tumefanya tu sehemu ,lakini pia upande wa malazi kwa wanafunzi ni changamoto ,wanafunzi wetu kiasi cha silimia 70 wanakaa nje ya chuo na kati ya hao kuna vijana wa kike ambao wanahitaji uangalizi mkubwa”alisema Prof Bee.

Naye Mwenyekiti wa Harambee hiyo,Noel Nko alisema wakati huu chuo kikiendelea kukua tuliona ni vyema wanafunzi wote waliohitimu chuoni hapa tangu mwaka 1963 tuone ni kitu gani tunaweza tukafanya kwa chuo zikiwa ni moja wapo ya kuunga mkono serikali.

“Niombe kutoa hamasa kwa wahitimu wote wa Chuo Kikuu cha Ushirika zoezi hili tulifanye kwa moyo ,hamasa itakuwa kwa mwenye kiasi chochote cha fedha atachangia na harambee hii itakuwa endelevu ,tutaifanya wanaushirika nchi nzima na niwaombe wanaushirika kote nchini ,wakiwa ni warajisi wa mikoa,maafisa ushirika wa halmashauri,popote pale walipo wahamasihe zoezi hili kwa nguvu zote”alisema Nko. 

Kukamalika kwa harambee hii kwa kiasi kikubwa litasaidia kuboresha ulinzi na usalama kwa wanafunzi pamoja na mali zao sambamba na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujisomea kwa wanafunzi na pia itasaidia wanafunzi wengi wa kike kupata elimu bora .
Mwisho
 

Comments