- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA ALOYCE NDELEIO
Dunia hivi sasa inatawaliwa na mageuzi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na hata hivyo moja ya njia inayoonekana
kuwa inatawala katika kuhabarisha katika
maeneo ya vijijini ni redio hali
inayoonyesha kuwa mageuzi yake
hayajazifikia jamii nyingi na hususani maskini.
Jenga taswira tu kuwa umepata safari (kwa wale wanaoishi
mijini) kwenda vijijini lakini katika mazingira ya kawaida imekuwa ni utaratibu
wa kawaida kupata habari au taarifa
mbalimbali za matukio kila siku kupitia
vyombo vya habari.
Aidha yapo matukio nyeti ambayo ukiwa mjini ni rahisi kuyapata lakini unapowasili kwenye makazi mapya vijijini
unakwama kuyapata matukio hayo pamoja na
mengine kwa njia rahisi kama ilivyozoeleka mjini.
Kadhalika unabaini ni vigumu kuyapata magazeti kwa kuwa
hayafiki maeneo hayo kwa wakati mwafaka na mara nyingine hufika kwa kuchelewa
na hivyo kuifanya habari kuwa imeshapitwa na wakati.
Pia unabaini kuwa kutokana na kipato duni cha jamii ya eneo
husika asilimia kubwa ya watu wa eneo hilo hawamudu kununua magazeti, na wenye
magazeti hawaoni haja ya kuyapeleka
huko, likionekana jua siku hiyo kuna mtu
ametoka mjini.
Hali hiyo inakufanya ufikie hitimisho kuwa njia mbadala na muafaka ya kupata habari ni redio peke yake, inahabarisha juu
ya matukio mbalimbali yanayoendelea
ndani ya nchi na duniani kwa
ujumla na hata kutoa burudani.
Njia hiyo ya redio unaiona inasadifu kiuchumi kwa kuwa
asilimia kubwa ya wanajamii wa vijijini wanamudu kununua betri na wanaweza
kuzitumia kwa muda mrefu.
Hapa ndipo linapojitokeza jambo moja muhimu kuwa
linapozungumzwa suala la Tehama miongoni mwa jamii nyingi za nchi maskini kwa asilimia kubwa kinachoweza kuzungumzwa ni
redio.
Kigezo muhimu kinachofanya hali hiyo kuwa hivyo ni kutokana
na sababu kuwa hata kama redio hiyo
haimilikiwi na familia ni dhahiri matangazo yake yanafika au kusikilizwa na jirani zaidi ya mmoja. Hivyo upashanaji wa
habari husambaa kwa njia ya kupeana
taarifa au kusimuliana.
Hali ya aina hii hubainisha
kuwa seti za televisheni na
magazeti kwa baadhi ya jamii hizo huonekana kwa nadra pamoja na dhana kuwa
teknolojia kwa walio na hali ya uchumi nafuu na kipato chao kinaruhusu na ambao
ni wachache.
Hali kadhalika utabaini kuwa katika maeneo mengi ya vijijini
hakuna umeme kwa hiyo nishati mbadala inayoweza kutumika ni betri ambazo pia
hupatikana kwa urahisi kwenye maduka
yaliyo vijijini.
Asilimia 80 ya jamii inaishi maeneo ya vijijini kupata seti
za televisheni ni vigumu lakini redio ni jambo la kawaida kama zilivyo
baiskeli ambazo pia ni moja ya njia
muhimu za usafiri, uchukuzi na mawasiliano.
Hapa ndipo unapotokeza msamiati ‘nakalando’ miongoni mwa
jamii za mashariki mwa Uganda ambalo
linamaanisha mtu kuzungumza bila kuonekana
hali ambayo jamii hiyo inafananisha na kuzungumza na mizimu.
Hali hiyo ni kwa kuwa njia hiyo ilijulikana kwa wale
waliokuwa na imani zinazohusiana na mizimu kuwa kusikiliza redio ni kusikiliza
mizimu kwa kuwa anayezungumza haonekani machoni mwa wasikilizaji, hivi sasa ni
jina la utani kwa redio.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ni
kwamba watu milioni 65 walikuwa wanapata
matangazo ya redio mwaka 1996 idadi ambayo ni sawa na wastani wa redio moja kwa
watu kumi.
Hali kadhalika kwa mujibu wa mtafiti binafsi Helen Hambly,
wa mradi wa utafiti wa kuunganisha kilimo na redio vijijini idadi hiyo ya redio
itaongezeka kutokana na kuwepo aina nyingi za redio tena za uhakika kutoka
China na India ambazo zinafurika katika masoko ya Afrika, na hususan katika
kipindi hiki cha biashara ya soko huria.
Matangazo ya redio,
mazingira
Haiyumkiniki kuwa pamoja na kuhabarishwa mambo mbalimbali
jamii za vijijini zingepiga hatua zaidi iwapo matangazo na habari zinazorushwa
zingehusiana na jitihada za kujikomboa kutoka kwenye lindi la umaskini
unaozikabili sehemu hizo.
Mtafiti Hambly anafahamisha kuwa hali hiyo inawezekana kwa
kutumia teknolojia ya kuanzisha vituo vya redio vijijini ambavyo vinajulikana
kama vituo vya redio vya ndani ya
‘mkoba’ kwa gharama ya dola za Marekani 3,000 sawa na takribani milioni 6.0/-.
Anadokeza kuwa vifaa vya redio ya aina hiyo vimefungwa hivyo
kwamba vinaweza kurusha matangazo yake
hadi masafa ya kilometa 50 kwa kutumia jenereta ambayo inatumia nishati ya jua.
Hambly ambaye ni mwanasosholojia wa mazingira na mwandishi
wa vipindi vya redio vinavyohusu kilimo anabainisha kuwa walengwa katika vituo
vya redio za vijijini ni wakulima, hivyo nafasi hiyo
inaweza kutumiwa ili
kuwahabarisha kuhusu kilimo endelevu.
Utafiti wa mwanasosholojia huyo uliodhaminiwa na Shirika la
Misaada la Kimataifa la Canada (CIDA) na ambao umefanywa kwa ushirikiano na
wataalamu wa Kitengo cha Taasisi ya
Maendeleo vijijjini ya Chuo Kikuu wa Guelph na Mtandao wa Redio Kilimo kwa nchi zinazoendelea (DCFRN) na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kilimo na Chakula (FAO).
Washiriki wengine katika utafiti huo ni Mpango
wa Redio za vijijini kwa nchi za
Camerooon, Ghana, Mali na Uganda anaendelea kuarifu kuwa dhana nzima iliyoelekezwa kwenye utafiti ni
namna ya kuwasaidia watangazaji kufanya
kazi na watafiti na wakati huo huo
kuyachukulia mazingira ya vijijini
kufikisha ujumbe kwa walengwa ambao ni wahitaji wa matokeo ya tafiti za kilimo.
Hata hivyo anafahamisha kuwa jambo lililojitokeza kwenye utafiti huo ni kwamba watangazaji wa
Afrika wanahitaji mafunzo, vyanzo vizuri
vya habari na fursa ya kuwa pamoja na
watafiti wa kilimo.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Mtandao Redio za Kilimo,
Nancy Bennet anasema kuwa watangazaji wanaweza kutumia habari zinazohusu
wakulima ambao labda wameshajenga uzoefu
na wanyama wanaowafuga kama vile kuzungumza na kuku wanaowafuga ili kuvuta
hadhira ya wasikilizaji lakini jukumu la mtangazaji wa vijijini ni kubwa, gumu
na zito.
Anatoa mfano kuwa miaka kumi iliyopita Mali ilikuwa na vituo
vya redio za vijijini 20 lakini hivi sasa vipo vituo zaidi ya 150 vyote vikiwa
vinafanya kazi katika programu za jamii ambazo zinatoa taarifa za hali ya hewa,
hali ya ukame na taarifa za tahadhari za kuwepo kwa janga la njaa.
Anabainisha kuwa njia za zamani za mawasiliano ya redio
zinatoweka na nafasi yake inachukuliwa na teknolojia mpya kama vile redio za
intaneti na njia zingine ambazo maudhui yanayotakiwa yanaweza kuwafikia walengwa.
Hali kadhalika mipaka kati ya vituo vya redio binafsi na
redio za umma imekuwa inabadilika ambapo anatolea mfano kuwa vituo vingi vya
redio za serikali kwa sasa vimekuwa vinaendeshwa kibiashara na kwa upande wa
vituo binafsi kuwa vinaegemea zaidi ushirikishwaji wa jamii.
Mfano hai wa redio za aina hiyo upo nchini Uganda ambapo
miaka mitano iliyopita ilikuwepo redio moja tu lakini teknolojia ya kisasa
pamoja na mfumo huria wa utangazaji kumewezesha kuwepo redio zaidi ya 70 baadhi
zikiwa zinaendeshwa kwa mfumo wa jumuiya na utangazaji wake ukiwa unalenga
matukio ndani ya jamii na hata mchango wa wanawake katika uelewa wa
teknolojia ya asili.
Mkurugenzi huyo anadokeza kuwa anabainisha kuwa uthibitisho
kutoka kwa wabia wa mradi wa
ISNAR ni mapendekezo yao kuwa redio
zinaweza kufanikisha kuwaunganisha wakulima na tafiti hali kadhalika zinaweza kusaidia ubunifu
ambao utawasaidia masikini wa vijijini.
Anaarifu kuwa wanasayansi katika sekta ya kilimo wanaanza
kuona redio kama njia mojawapo ya kuwezesha kufanikisha ubunifu wao wa
kitaalamu moja kwa moja vijijini.
Anasema kuwa kimsingi ni kwamba jambo linalofanyikas ni
kuchupa kutoka juu ya mifumo ya asili ya kilimo ambayo imesahaulika kifedha na
hata kiutendaji.
Anaarifu, ‘Wanasayansi nao wameanza kubaini kwamba redio
huwasilisha mambo yao muhimu. Hata hivyo hadi sasa baadhi ya watafiti bado
wanaamini kwamba jukumu la kufikisha ujumbe au matokeo ya utafiti wao kuwa la
mtu mwingine.’
Anaendelea kuarifu kuwa watafiti wanahitaji kuhusishwa na
inatakiwa mawasiliano yawe katika mikondo miwili na si kitendo cha habari kuwa
kwenye mtiririko wa upande mmoja tu.
Redio za jamii vijijini zinaonesha njia ambayo jamii ya
maeneo husika inaweza kuhabarishwa na jamii
hiyo yenyewe kuhabarisha pia
kuhusu miundombinu ambayo wanasayansi na wakala wengine wanaweza kutumia
kuboresha mazao ya kilimo na ufugaji na huduma nyingine za kijamii.
Comments
Post a Comment