Featured Post

KUNGURU WEUSI HATARI KUSHINDA INZI, PANYA




NA ALOYCE NDELEIO
WAMESHAZOELEKA kama wanyama wa kufugwa. Wanaongezeka idadi kwa kasi kuteketeza ndege wa jamii nyingine katika mazingira waliyoshamiri. Hao ni kunguru weusi ambao karne moja iliyopita hawakuwepo kabisa hapa Afrika Mashariki.
Fikiria kuwa umeingia kwenye bustani baa moja katikati ya jiji la Dar es Salaam na kuna viti vya plastiki unaagiza supu na soda. Unapokuwa unasubiri ulichoagiza anaangaza kwenye mandhari ya bustani, barabara na nyumba za karibu.

Unaiona bustani ya nje ya baa hiyo kuwa inavutia. Inabidi kukaa kwenye kona ili kukwepa sauti kali ya muziki unapigwa kwenye baa hiyo.  Mbele yake unaowaona wateja wapatao 12 waliokaa kuzunguka meza tofauti kwa vikundi vya watu watatu au wanne hivi wakinywa supu na vinywaji mbalimbali.
Katika meza moja wanaondoka na nyingine ikabakia na vyombo vya chakula na chupa za soda, ambavyo vilitumiwa na wateja wale. Wahudumu watatu wanaohudumia wanaonekana kutingwa na kazi na kuchelewa kuleta ulichoagiza.
Pale tayari kunguru weusi watatu wameshajikaribisha wakila mabaki ya vyakula kwenye vibakuli na sahani. Haraka haraka mhudumu anaviondoa vyombo vile na kuvirudisha katika jiko la baa.
Kunguru wanaruka na kutua juu ya mti ulio karibu na baa, hawachezi mbali, unapata picha ya jina la riwaya ya James Hadley Chase; ‘The Vulture Is A Patient Bird’.
Mhudumu analeta supu na soda baada ya dakika 15 hivi, hapo unaona wateja kwenye meza nyingine wakiondoka, kunguru nao wanajikaribisha.
Hapo ndipo unaona hamu ya supu uliyonayo ikianza kutoweka. Unapoiangalia supu yenyewe ndani ya bakuli unaona kitu cheusi ambacho hakikufanana na nyama ya ng’ombe iliyochemshwa. Unapokichota  kwa kijiko unagundua kwamba ni inzi aliyekufa.
Unaposhika bakuli la supu kwa nje unagundua halikuwa na joto la kutosha kuua wadudu wa maradhi. Unamwita tena mhudumu na kumweleza kwamba supu ile haina na joto la kutosha.
“Samahani kaka, tunaweza kukupashia moto hadi ichemke kama unapenda. Wateja wengine huwa hawapendi supu ya moto sana mpaka mteja aseme!” anajibu mhudumu na unamjibu, “Sawa nichemshie tena ipate joto la kutosha kuniunguza ulimi”.
Mhudumu anaondoka na bakuli la supu juu ya sahani na kurudi jikoni. Unakunywa soda haraka na kumaliza. Unamfuata mhudumu unampa 500/- za soda ile. “Mbona umeamka, hutaki tena supu?,” mhudumu anakuuliza.
Unamjibu; “Hapana nataka kununua gazeti hapo nje nitarudi sasa hivi. Endelea kuchemsha hadi ipate joto sawasawa”.  Unatoweka!.
Unavuka barabara na kutembea kama mita 15O  kwa mbele unaona nyumba yenye duka la vinywaji baridi na pameandikwa: “Karibuni. Tunatoa huduma za chakula hapa”. 
Kuna meza tatu na viti vya plastiki kama nane hivi. Unakukaribishwa kwa bashaha, “Karibu  kaka, tuna supu ya kuku wa kienyeji, ng’ombe, samaki na soda”.
Unaagiza, “Tafadhali naomba nipatie supu ya kuku lakini iwe ya moto sana,” na  kuulizia msalani na unajibiwa, “Zunguka mlango wa pili kushoto kwako halafu nenda moja kwa moja hadi uwani. Utaona milango iliyoandikwa.”  
Unaingia eneo pana kidogo la wazi unaliona karo lenye vyombo vya chakula. Unawaona kunguru weusi wapatao saba wametanda juu ya karo hilo wakidonoa mabaki ya vyakula katika vyombo. Wote wanaruka mara unapoingia na kutua juu ya mwembe uliokuwa nyuma ya uwa wa eneo hilo.
Unaingia msalani, unatoka baada ya dakika mbili unakuta kunguru wale wamesharudi katika starehe yao juu ya vyombo kwenye karo. Wanaruka kurudi kwenye mti.
Unarudi sehemu ya mbele ya nyumba na unaletewa supu kwenye kibakuli cheupe juu ya sahani safi. “Karibu sana kaka. Huhitaji kitu kingine?”  Unaagiza maji na kujaribu kusahau uliyoyaona huko uwani. Unakunywa supu ya moto na unaiona ni tamu.
Hakuna kunguru anayeonekana karibu bila shaka wanastarehe kwa uhuru zaidi huko uwani. Unagundua vyombo vilivyotumiwa na wateja vilikuwa vinakusanywa na hatimaye kupelekwa uwani kuoshwa katika karo ulilokuta kundi la kunguru wakistarehe.
Unapoondoka sehemu hiyo unagundua kwamba takriban kilomita mbili toka ulipokuwa kulikuwa na hospitali kubwa iliyolaza wagonjwa wa kipindupindu.
Ukiwa kwenye kituo cha basi ghafla unaona kitu kimedondoka toka angani yapata mita tatu hivi mbele ya kundi la wasafiri waliokuwa kituo.
Kitu hicho kinazingwa na inzi mara moja. Unagundua ni mzoga wa panya uliodondoshwa na  kunguru mweusi.
Upande wa pili wa kituo cha mabasi unaona wauza matunda aina ya nanasi na tikiti-maji yaliyokatwakatwa vipande vidogo na kuviweka kwenye sinia.
Wateja wanakula bila wasiwasi, vumbi linatimka pamoja na upepo wa jua kali. Pia yupo muuzaji maji baridi yaliyo katika vifuko vya plastiki. Karibu kuna soko dogo la wazi, unabaini linalisha pia kunguru wengi weusi.
 Jua ni kali unasogea kivulini chini ya mti ndogo lakini ghafla unasikia tone zito limekudondokea begani. Loh! kunguru kanya, kinyesi kimedondokea kwenye shati lako jeupe! Unasikitika unashindwa kupanda daladala  unarudi sehemu uliyokunywa supu unaelekea uwani kujisafisha kinyesi cha kunguru.
Mazingira haya yanatia hofu lakini ndio hali halisi katika maeneo mengi ya watu wa vipato vya kati na chini waishio jijini Dar es Salaam.
Wakazi wa jijini Dar es Salaam wanakaribia milioni sita sasa, nusu yake wanaishi katika makazi holela. Mengi hayana huduma bora za kijamii kama uzoaji taka ngumu, mitaro ya maji taka na maji ya mvua.
Mara kwa mara wataalamu wa afya ya jamii wamekuwa wakihimiza wakazi wa jiji kuweka mazingira yao safi kwa kuharibu mzalio ya inzi na mbu. Lakini hata mazalia yote ya wadudu wabaya yangeteketezwa bado jiji halitakuwa salama kabisa kiafya kutokana na uchafuzi wa kunguru weusi.
Ukweli unaonekana wazi kwamba kunguru weusi ni wasambazaji wa uchafu kwa masafa marefu na kiwango kikubwa  kuliko inzi na panya.
Kunguru weusi wanakula mizoga ya panya wanaokufa au kuuwawa katika makazi ya watu na kutupwa majalalani. Huruka na mizoga hiyo, huidondosha popote wanapokuta ‘kitoweo’ kingine cha kudokoa. Wanabeba uchafu kwa miguu na midomo yao.
Hutumia midomo kudokoa mabaki ya chakula kwenye vyombo vya kulia na kupikia kwenye makaro na kuacha uchafu huo. Wanatua juu ya nguo zilizoanikwa nje kwenye kamba na kuzichafua kwa vinyesi wanavyobeba na miguu yao toka majalalani. Wanatoa vinyesi vyao popote wakiwa wanaruka au wametua sehemu fulani.
Kunguru weusi wanaingia katika maeneo ya hospitali na kuzoa taka hatari zinazoweza kuambukiza maradhi mengi. Kunguru weusi wanakula vifaranga vya kuku na kinda wa ndege wengine. Ni waharibifu wa mazingira.
Kila mwaka milipuko ya kipindupindu haikosi kutokea jijini Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wanasahau au wanadharau madhara ya kunguru weusi. Panya, mbu na inzi ndio wanatajwa kila mara katika orodha ya viumbe hatari kwa afya ya mazingira.
Wanafunzi hufundishwa shuleni, adui wakubwa wa afya ya mazingira ni mzalia ya inzi na mbu. Lakini mbu na inzi wanaweza kuteketezwa kwa dawa za kupuliza pamoja na usafi wa mazingira.
Panya hali kadhalika anadhibitiwa na paka, mitego au sumu hivyo ni adui rahisi kuteketezwa.  Kazi ipo kwa kunguru.
Ilishazoeleka kwamba kunguru weusi si rahisi kuwatega kwa sumu kwani hawatakula mzoga wenye sumu. Wanaweza kutegwa na mitego na kunaswa hai lakini si kuuwawa kwa sumu.  Aidha inajibainisha kwamba maradhi ya homa ya matumbo (typhoid) yameongezeka sana jijini Dar es Salaam na yanatoa roho watu wengi yanapochangayika na malaria.
Homa ya matumbo kama kipindupindu ni maradhi yanatokana na mazingira machafu.  Vimelea vya maradhi haya hustawi zaidi katika vinyesi na mizoga ya panya, paka, mbwa na wanyama wengine wa kufugwa wanapogogwa na magari.
Kunguru weusi husambaza vimelea hivyo wanapotua juu ya mizoga hiyo na hatimaye juu ya vyombo vya chakula, meza za kulia na nguo za binadamu zilizoanikwa baada ya kufuliwa.
Je, Dar es Salaam iendelee kuteswa na maradhi ya kuambukiza kwa sababu ya kunguru weusi ambao hawakuwepo karne moja iliyopita?
Kunguru weusi ni spishu ngeni vamizi ambao wamesababisha kunguru wa asili wana mabaka meupe kutoweka.  Hawa pia wameangamiza ndege wengine kama njiwa, tetere, shorwe na mbayuwayu kwani makinda na mayai yao huliwa na kunguru weusi.
Wizara ya Maliasili na Utalii iliendesha zoezi la kuwaangamiza kunguru weusi katika mikoa ya ukanda wa pwani kwa kutumia sumu tulivu aina ya DRC 1339. 
Jumla ya kunguru 41,487 waliuwawa Jijini Dar es Salaam kwenye zoezi moja. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo tangu mradi wa kudhibiti kunguru weusi uanze Julai 2010, hadi Septemba 2012, kunguru weusi 807,961 wameshauawa kwa kutumia sumu hiyo na mitego katika Mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Pwani na Tanga.
Taarifa hiyo inasema kuwa japo sumu hiyo haina madhara makubwa kwa binadamu, wananchi hasa watoto, wanatakiwa kutochezea mizoga ya kunguru ambao watakuwa wamekufa kutokana na sumu hiyo.
Kunguru weusi wanauwawa kwa lengo la kupunguza idadi yao ili wasiendelee kusababisha kero kwa wananchi kwa kupokonya chakula na vitu mbalimbali. Aidha, kunguru wamekuwa wakieneza vimelea vya magonjwa mbalimbali kwa binadamu na kuku. Hata hivyo wanabakia kuwa ni spishu hatari kwa mazingira na afya na inatakiwa uteketezaji wake uwe endelevu. 

Comments