- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI WETU
KISWAHILI ni moja ya
lugha kuu tatu maarufu miongoni mwa jamii za Afrika ambapo nyingine ni pamoja
na Kihausa na Kiarabu. Hata hivyo, Kiswahili kimekuwa kinapata umaarufu na hata
kukubalika kuliko ilivyo kwa Kihausa na
Kiarabu kote Barani Afrika na hata miongoni mwa nchi nyingine nje ya bara la
Afrika. Kutokana na hali hiyo, Kiswahili
kinaonekana kuwa moja ya lugha kubwa ndani ya Afrika.
Inakadiriwa kuwa idadi ya watu wanaozungumza Kiswahili kwa
sasa inafikia milioni 110 na katika uzungumzaji wake. Kiswahili ni lugha
inayozungumzwa na kufundishwa miongoni mwa Waafrika wenyewe, Mashariki ya
Mbali, Ulaya na Marekani.
Mada iliyowasilishwa na Dk. Sigalla Huruma wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam hivi karibuni kwenye Mkutano wa Jamii Anuai inabainisha kwamba
miongoni mwa jamii za Afrika Mashariki, Kiswahili kimeibuka kuwa lugha ya
Afrika Mashariki katika mazingira ya kawaida.
Kwa mfano, nchini Uganda, Kiganda kinatumika zaidi na hata
hivyo kimeshapoteza umaarufu kutokana na kujikita zaidi miongoni mwa kabila la
Baganda.
Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambako kuna lugha za
kienyeji zaidi ya 120 serikali ya nchi hiyo imependekeza lugha kuu za taifa
ziwe nne ambazo ni Choking, Chilumba, Lingala na Kiswahili. Miongoni mwa lugha
hizo nne Kiswahili ndio kimekuwa kinapata umaarufu na kinakua zaidi na kwa
haraka miongoni mwa jamii za nchi hiyo.
Aidha Kiswahili hakipanuki tu miongoni mwa jamii bali pia
kinapanuka kama lugha ya biashara na katika mkondo huo inaelezwa kuwa tangu
mwaka 1959 kimetokea kuwa daraja lililowaunganisha viongozi wa harakati za
ukombozi Afrika.
Washiriki kwenye harakati hizo walitoka miongoni mwa nchi
zilizozungumza Kifaransa na zilizozungumza Kiingereza. Aidha wanaharakati hao
waliweza kuwasiliana kwa msaada wa wajumbe kutoka kila upande ambao walikuwa
wanakifahamu Kiswahili na hivyo
kuwatafsiria wenzao.
Dk. Huruma anabainisha kuwa madai kwamba Kiswahili sio tu
lugha ya Taifa ya Tanzania na Kenya bali ni lugha ya Afrika Mashariki na Kati
ni ya kweli na inakubalika hivyo.
Wasomi wengi ndani ya Afrika Mashariki na Kati na hata nje
wanabainisha ukweli kwamba Kiswahili kinazungumzwa na kueleweka Mashariki na
Kati na sehemu nyingine duniani na wanabainisha ukweli kwamba ni lugha ambayo
katika Afrika ina mchango muhimu kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia,
hivyo inafaa kutumika si kama lugha rasmi Afrika Mashariki na Kati pekee bali
katika bara lote la Afrika.
Kwa mfano wataalamu wa lugha ya Kiswahili kama Mulokozi,
Ryanga na Chacha wanatoa mifano halisi inayoonesha kwamba Kiswahili kinatumika
Afrika Mashariki na Kati katika majadiliano na mihadhara ya kisiasa, kiuchumi
na kijamii.
Zipo nchi zaidi ya 11 katika eneo la Afrika Mashariki na
Kati ambako Kiswahili kimepanuka na kinazungumzwa
kueleweka. Katika msingi wa aina hiyo
nchi hizo ambazo zinaunda kundi la nchi
zinazozungumza Kiswahili ni pamoja na
Burundi, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Malawi, Msumbiji,
Rwanda, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe
Kwa jinsi Afrika Mashariki ilivyo ni muhimu kuweka wazi
kwamba mfumo wa kisiasa na kiuchumi katika Afrika kama vile Umoja wa Afrika na
Jumuia ya Afrika Mashariki kimsingi hauwezi kufanikiwa na kuwa na ufanisi kwenye malengo yake kama
hakutakuwepo na kupewa kipaumbele kwa masuala ya utamaduni na lugha ambavyo
vitakuwa ni gundi ya kushikamanisha umoja.
Ushiriki wa watu wa kawaida kwenye mijadala na maamuzi
kuhusu masuala muhimu yanayoathiri maisha yao kunaweza kuwa njia moja nzuri ya kufanikisha Kiswahili kuwa na lugha
ya pamoja. Katika hali hiyo ni muhimu kusema kuwa mawasiliano ya lugha moja
yanaweza kuimarisha hali ya mshikamano na undugu.
Kutokana na baadhi ya nchi za Afrika kuegemea au
kutegemea kwenye lugha za kigeni au kwa
maana nyingine lugha za kikoloni kwa
namna moja kumesababisha athari kwenye mawazo na hivyo kuathiri maamuzi makubwa
ambayo yanazihusu.
Kiswahili kuingia
Gabon
Hivi karibuni serikali ya Gabon imefikia uamuzi wa
kuanza kufundisha Kiswahili kwenye shule
zake kuanzia shule za msingi, hivyo kuiomba Tanzania kubuni na kuanzisha
mitaala inayofaa kuanzisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchini humo.
Rais Ali Bongo Ondimba wa nchi hiyo alimwomba Rais wa
Tanzania wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete kumpatia mwalimu binafsi wa
kumfundisha lugha ya Kiswahili ikiwa ni jitihada zake za kuonesha mfano wa
kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wananchi wake.
Kutokana na hali hiyo Gabon inakuwa ni nchi nje ya nchi
zinazounda Jumuia ya Afrika Mashariki kuazimia lugha hiyo kufundishwa
mashuleni.
Katika mazingira hayo ni dhahiri Kiswahili kunapanuka kwa
kasi na itakuwa ni nchi ya 12 kutumia Kiswahili kama moja ya lugha muhimu ya
mawasiliano barani Afrika.
Changamoto za sasa
Zipo changamoto kadhaa ambazo Kiswahili kimekuwa
kinakubaliwa kama lugha ya taifa.
Changamoto ya kwanza ni katika elimu. Kumekuwepo majaribio ya kupendekeza
Kiswahili kiboreshwe zaidi na kutumiwa kama lugha ya kufundishia katika elimu
ya sekondari na hata elimu ya juu.
Changamoto inayokikabili ni kwamba vyanzo na utaalamu wa kutafsiri
vitabu vya msingi na hususani kwenye masomo ya sayansi katika ngazi hiyo kwa
sasa hali hiyo inabakia kuwa ni tatizo.
Changamoto nyingine ni kutokana na ukweli kwamba hivi
sasa jamii inaishi kwenye dunia
iliyojikita kwenye utandawazi kiuchumi na kiteknolojia ambapo Kiingereza
kinabakia na kuendelea kutumiwa sana hususani kwenye biashara na kuwafanya
wanaopinga matumizi ya Kiswahili kutumiwa katika ngazi za elimu kutumia kigezo
hicho kukatisha tamaa maendeleo yake.
Zipo sababu za kijamii zaidi na hususani wimbi la sasa baada
ya kuhurishwa kwa huduma za kijamii
kuanzia miaka ya 1990 ambapo mfumo wa elimu nao haukupitwa na hali hiyo.
Kuanzishwa kwa shule binafsi kuanzia ngazi ya shule za awali
hadi msingi, sekondari na hata vyuo kumesababisha kuibuka kwa shule nyingi binafsi ambazo zinatumia Kiingereza
kama lugha ya kufundishia.
Katika mazingira hayo imekuwepo tabia miongoni mwa wazazi
hivi sasa wakiongozwa na wasomi kuchukulia kuwa kujua kuzungumza Kiingereza
kama kigezo muhimu kwa maendeleo ya kitaaluma ya watoto.
Jambo la aina hii sio tu kwamba linawanyima watoto haki ya
kujifunza lugha bali pia inamomonyoa fursa za kujifunza na kuzoea utamaduni ambao unapatikana na kuimarishwa
kupitia lugha yenyewe.
Kisiasa ni kwamba kuwepo mabadiliko kwenye umuhimu wa kuunganisha utambulisho wa uasilia kunaakisi
mabadiliko ya kisiasa, kwa mfano
kuanzishwa kwa sera mpya za kiliberali na siasa za mfumo wa vyama vingi kwa
Tanzania uasilia umekuwepo kwa kuhisi kuongezeka kwa mabadiliko japo
utekelezaji wake sio kwa kiwango
kikubwa.
Utandawazi na fursa ya
kupanuka
Lugha ya Kiswahili kama zilivyo lugha nyingine duniani
imepitia kwenye mikono mbalimbali kuanzia chimbuko lake, kukua na inaelekea
kwenye kukomaa kutokana na kutumiwa na watu wengi duniani hivi sasa.
“Nina uzoefu na lugha ya Kiswahili na nimesikia kwamba
Kiswahili kinakua na kupata umaarufu
mkubwa kama lugha ya kimataifa na hilo ni juu yenu watu mnaozungumza Kiswahili
kuhakikisha kuwa umaarufu wake unaongezeka”
Kauli hiyo ilitolewa na Meya wa zamani wa jiji la London,
Ken Livingston kwenye mahojiano na
Mtanzania mmoja ambaye alitaka kufahamu mambo ambayo anayafahamu kuhusu
Tanzania.
Kiswahili kama lugha ya taifa imeweza kuibuka na kuwa
hivyo kutokana na sababu za kiutamaduni
ambazo zilikuwepo kabla na ambazo
zilisababisha kuyaweka makundi ya watu pamoja.
Biashara ilikuwa pia ni kichocheo kwa baadhi ya watu
kujifunza lugha, lakini sera za kikoloni pia ziliendelea kuboresha au
kukuza lugha ambayo imeendelea
kuimarisha umoja miongoni mwa makundi mbalimbali ya jamii.
Baada ya uhuru serikali ilikuwa makini kwenye kukuza lugha
na hivyo kuifanya lugha ya taifa na sera kadhaa, hatua na taasisi zilianzishwa
kuunga mkono maendeleo ya Kiswahili.
Katika mazingira hayo ni dhahiri kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alitoa mchango mkubwa na wa aina yake kwa kutumia
Kiswahili kujenga taifa imara licha ya kuwa na makundi mengi ya kikabila na ya
kidini.
Kwa namna ambavyo Afrika Mashariki ilivyo wimbi la sasa hivi
la utandawazi kupitia biashara huria, kukuza uwekezaji kutoka nje, ushirikiano
wa kiuchumi miongoni mwa nchi na kanda za bara la Afrika ambazo zinatoa fursa
kuendeleza, kupanua na kupenyeza Kiswahili katika maeneo mbalimbali kama
ilivyokuwa kwa Tanzania.
Ukweli ni kwamba moja ya sababu zilizowezesha maendeleo ya
Tanzania kuanzia kwenye karne ya 19 ni biashara na leo hii pamoja na mambo
mengine utandawazi kwa ujumla umejikita kwenye ushirikiano wa kiuchumi hivyo
basi ipo haja ya kukiingia kifua Kiswahili katika mkondo wake wa kupanuka.
Ushirikiano wa kiuchumi kati ya sekta mbalimbali za
kiuchumi, mashirika na nchi lazima kuongozwe na wapanga sera wetu (kisiasa) kwa
kukitumia Kiswahili kama lugha rasmi ya biashara.
Zipo njia nyingi ambazo zinaweza kutumiwa katika kufanikisha
hatua ya Kiswahili kutumiwa kama lugha rasmi ya biashara kama vile shule au
vyuo vya biashara kuhakikisha kuwa Kiswahili kinajumuishwa kama lugha ya
biashara.
Aidha njia nyingine ni kuyafanya matangazo kuwa kwa
Kiswahili, nembo za bidhaa iwe ni lazima kuandikwa kwa Kiswahili, mawasiliano
ya kibiashara na misamiati ya kisheria kwenye biashara itafsiriwe na kutolewa
kwa Kiswahili pamoja na mambo mengine mengi ambayo yanahusiana na biashara yawe
kwa lugha hiyo.
Hivi sasa hakuna ambaye anafikiria kuwa Kiswahili kinaweza
kuwa ni lugha ya kimataifa lakini hoja ni kwamba ni kwa kasi gani kinaweza
kuendelezwa, kupanuliwa na kukiwezesha katika hatua za kujenga utambulisho kwa
watu wote wanaozungumza Kiswahili.
Katika sekta hii ya kiuchumi ni dhahiri sekta ya utalii
inaingia moja kwa moja kwamba inaweza kukikuza Kiswahili kutokana na kuhusisha
idadi kubwa ya watalii kutoka nje ya nchi. Hali hiyo inawezekana kupitia
utambulisho wa tamaduni mbalimbali zilizo nchini.
Kutokana na watalii wengi kupendelea kufahamu tamaduni za
sehemu wanakotalii hiyo ni moja ya fursa ambapo Kiswahili kama sehemu ya
utamaduni kinaweza kuenezwa kwa kasi nzuri.
Hali hiyo inatokana na jinsi kauli ya Meya huyo wa zamani wa
jiji la London kusema kwamba ni juu ya wanaozungumza Kiswahili kuhakikisha kuwa kinapanuka na moja ya
njia ni kupitia sekta ya utalii.
Kwenye ulingo huu wa utandawazi imeshajidhihirisha kuwa
Kiswahili kinapanuka kutokana na kutumika kwenye vyombo vya habari vya
kimataifa vikiwemo vituo vya redio vya Sauti ya Ujerumani, BBC, Redio ya
Kimataifa ya China, Redio VaticanRedio Japan na Sauti ya Amerika.
Malema iwe lugha ya
Afrika
Licha ya kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Afrika (AU), Kiongozi
wa Chama cha Watetezi wa Uhuru wa kiuchumi (EFF) cha Afrika Kusini, Julius
Malema, ametoa wito wa kupitishwa kwa lugha moja itakayotumika barani Afrika,
huku akipendekeza lugha inayofaa kutumika iwe ni Kiswahili.
Malema aliyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari
ulioandaliwa na EFF, ambapo aliongelewa mambo mbalimbali ikiwemo ujumbe wa Rais
wa Marekani Donald Trump kwenye mtandao wa Twitter kuhusu marekebisho ya sheria
ya ardhi Afrika Kusini.
"Tunatakiwa kuanzisha lugha moja ambayo itatumika
kwenye bara zima. Kwa mfano Kiswahili, kinaweza kukuzwa ili kitumike barani
kote," alisema Malema.
Lugha ya Kiswahili ni lugha inayotumika sana barani Afrika,
ambapo kinatumika sana Afrika Mashariki na Kati. Ni lugha rasmi kwa nchi ya
Tanzania na Kenya.
Comments
Post a Comment