Featured Post

AMANI CENTRE WAOKOA WATOTO 1200 WALIOKUWA WAKIISHI KATIKA MAZINGIRA HATARISHI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Kituocha Amani (Amani Center for Street Children ) Meindert Schaap akizungumza wakati wa mahafali ya 12 ya wanafunzi wa Darasa la Saba waliokolewa na kituo hicho kutoka mitaani.

Mgeni rasmi katika Mahafali hayo ,Mratibu wa Elimu kata ya Karanga,Mercy Mandia akikabidhi zawadi kwa baadhi ya Wanafunzi walihitimu Darasa la Saba waliooklewa kutoka Mitaani na kupata msaada wa Elimu kutoka katika kituo hicho.
Mzazi Mwakilishi wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho ,Editha Cyril akitoa neon la shukrani kwa msaada mkubwa uliotolewa kwa watoto hao.
Mtoto Getrude Salutary ,mmoja wa Wahitimu wa Darasa la Saba waliokuwa wakilelewa katika kituo hicho akisoma Risalambele ya mgeni rasmi,kushoto kwake ni mwanafunzi mwenzake ,Michael Salutary.
Kikundi cha Vijana wa Sarakasi wakionyesha umahiri katika mahafali hayo.
Watoto wanaolelewa katika kituo hicho wakionesha vipaji vyao katika uchezaji wa Muziki.
Watato hao wakionesha umahiri katika uchezaji wa ngoma za Asili.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii, Kanda ya Kaskazini
WATOTO 1,200 waliokuwa wakiishi katika mazingra hatarishi mitaani wameokolewa na shirika lisilo la kiserikali la  Amani (Amani Center for street Children) na kusaidia upatikanaji wa elimu kwa watoto hao na baadae kuwaunganisha na familia zao.
Watoto waliookolewa wakiwa katika umri tofati tofauti ,walichukuliwa na kituo cha Amani kutoka katika mitaa ya mikoa ya  Singida,Moshi na Arusha ambapo mwaka huu watoto 31 kati ya kundi hilo wamehitimu elimu ya msingi baada ya kupata msaada wa kituo hicho.
Akizungumza wakati wa mahafali ya 12 ya kuwaaga wanafunzi hao ,Mratibu wa Elimu wa kituo cha Amani Brenda Mzava alisema licha ya kuwaunganisha familia zao baada ya kuwalea watoto hao kwa muda mrefu, kituo bado kinaendelea kuwafuatilia na kuwasaidia hadi hapo watakapoweza kujiendeleza.
“Kama baadhi yetu tunavyojua watoto hawa walikuwa kwenye mazingira hatarishi na magumu ya mtaani kabla ya kuokoloewa na shirika la Amani, kwa kuwatoa mtaani,kuwapatia huduma na haki za msingi ikiwemo huduma za afya na elimu bora, siyo kazi rahisi hususani kwa motto aliyekuwa mtaani kwa muda mrefu.”alisema Mzava.
“Kazi hii haikuwa rahisi lakini kwa ushirikiano wa jamii pamoja na serikali hususani Manispaa ya Moshi kupitia shule ya Msingi Shirmatunda na Magereza jambo hili limewezekana hatimaye watoto 31 waliokuwa mtaani wamefanikiwa kuhitimu elimu ya msingi.”aliongeza Mzava.
Alisema kama shirika wanajivunia watoto hao kwa kuweza kuhitimu elimu yao ya msingi na kuwa ni mafanikio makubwa kwa shirika naTaifa kwa ujumla na kwamba ushirikiano uliopo kati ya shirika la Amani ,jamii na taasisi za Serikali ni wa pekee kwani unaogozwa na uwito pamoja na kujitolea.
“Kwa namna moja au nyingine tumewawezasha watoto hawa waliohitimu darasa la saba na wale tunaondelea kuwalea katika kituochetu kujenga msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye kielimu.”alisema Mzava.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mratibu wa Elimu kata ya Karanga Mercy Mandia alilipongeza Shirika la Amani kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwaokoa watoto toka kwenye mazingira hatarishi ya mtaani kisha kuwaweka sehemu salama na kuwapatia huduma za msingi ikiwemo Elimu.
”Niwapongeze shirika la Amani kwa kazi nzuri kwa kufanya watoto tunaoita wa mitaani kuwa  watoto tena hasa kwa kuwapatia huduma za msingi kama malazi ,Chakula ,huduma za Afya,Elimu pamoja na mchakato mzima wa kuwarudisha kwenye jamii,”alisema Mandia.
“Nijitihada nzuri naomba kuahidi serikali kuanzia ngazi ya Mtaa,Kata,Manispaa pamoja na Mkoa kwa ujumla tutafanya kazi bega kwa bega kuhakikisha kazi hii inafanikiwa kwa kiasi kikubwa”aliongeza Mandia.
Mandia alitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa kituo hicho ,Meindert Schaap pamoja na wafanayakazi wote kwa kazi nzuri wanaoifanya yakufundisha ,kutunza,na kulea kiroho na kimwili watoto hao na kwamba Mungu ataibariki kazi hiyo na kukumbuka jitihada za kituo hicho.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Amani ,Meindert Schaap alisema ni faraja kubwa kuona idadi kubwa ya watoto waliotoka mitaani wanaelekea kwenye mafanikio makubwa hasa baada ya baadhi yao kuhitimu elimu ya Msingi.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake , Joyce Faustine Ngada aliyekuwa akisoma shule ya msingi Magereza alikishukuru kituo cha Amani kwa kuwaokoa kutoka mazingira hatarishi ya mtaani na kuwaleta kituoni ambapo wamefanikiwa kupata huduma mbalimbali za msingi ikiwemo Elimu.
“Mimi nilichukuliwa nyumbani Bukoba na kuja kufanya kazi za ndani Moshi,baada ya kufika Moshi nilijikuta nafanya kazi tofauti ya ile niliyo ahidiwa wakati natoka nyumbani kwani nilijikuta nafanya kazi ya Baa”alisema Joyce.
Alisema kupitia muelimishaji mtaani wa Amani (Street Educator) alifanya nae mahojiano na kwamba awali alikuwa akimdanganya lakini nilipogundua anania njema ya kutaka kumuokoa alitoa ushirikiano na kuweza kutoka kwenye kazi ya kuuza Baa na kupelekwa katika kituo cha Shirika la Amani .
Amani Centre for Street Children ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 2001 na kusajiliwa  baada ya kupewa namba NGO/0766 likifanya kazi ya kuwaokoa watoto wanaoishi mtaani kwa muda wote,katika miji ya Moshi,Arusha na Singida.
Mwisho .

Comments