Featured Post

WAZIRI ANAYEMKERA DKT. BASHIRU KWA KUMILIKI EKARI 1,000 HUYU HAPA



AGOSTI 30, 2018, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (pichani), alisema kwamba kuna waziri mmoja wa serikali ya sasa ambaye anamiliki ekari 1,000 na kwamba atamwita ili kumuuliza alizipataje.
Dkt. Bashiru alisema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa Baraza la Umoja wa Wanawake CCM (CWT) ambapo alisema sakata hilo alikutana nalo mkoani Morogoro wakati akizungunza na wananchi kuhusu masuala ya migogogo ya ardhi.

“Nilikuwa Morogoro akatajwa Waziri mmoja ana ekati 1,000. Wananchi wananiuliza wanataka kujua amezipataje, na mimi nitamuita aeleze amezipataje? Hatuwezi tukawa na viongozi ndani ya chama kinachojitambulisha kama chama cha wanyonge halafu baadhi yetu wanapora ardhi ya wanyonge,” Dkt. Bashiru alieleza bila kumtaja jina Waziri huyo na badala yake alieleza kuwa atamtaja muda ukifika.
Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kwamba, waziri anayetajwa kumiliki ekari 1,000 za ardhi ni Luhaga Joelson Mpina, anayeongoza Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi.
Gazeti la Raia Mwema lilikwishaandika mwezi Machi 2018 kuhusu suala hilo katika habari hii hapa: 

NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi katika Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, Luhaga Mpina, ameingia katika mgogoro na wananchi wa kijiji cha Dala, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro baada ya kutwaa kwa njia ya utata ekari 700, na kufanya amiliki jumla ya ekari 1,000 kijijini hapo.
Tayari Waziri Mpina amekwishafanya malipo ya shilingi milioni 35 kati ya milioni 50 za mauzo ya kiwango hicho cha ardhi, huku wanakijiji wakija juu wakisusia fedha hizo kwa miezi kadhaa sasa na kumwelekezea tuhuma kadhaa.
Hata hivyo, Waziri Mpina anasema hakuna ukiukwaji wowote wa taratibu huku akitaka ufafanuzi wa kina kuhusu suala hilo utoke kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Sudi Mpili, ambaye gazeti hili lilifanikiwa kumpata, naye akikiri baadhi ya kasoro lakini kwa ujumla, akisema waziri hana kosa lolote.

Madai ya wanakijiji
Mwandishi wa gazeti hili alifika katika kijiji cha Dala, kushuhudia eneo hilo lenye utata, kuzungumza na uongozi wa kijiji pamoja na wananchi, na katika mazungumzo hayo miongoni mwa wananchi walieleza masikitiko yao kutokana na ubabe wa waziri huyo, wakidai amekuwa akisaidia na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro dhidi yao.
Katika mazungumzo yake na Raia Mwema – Jumatatu, Mwenyekti kijiji cha Dala, Boi Lubegete, alisema kwa mara ya kwanza Mpina alifika kijijini hapo na kuomba apatiwe ekari 300 lakini akitumia watu tofauti ili kukwepa ‘mkono wa sheria’ unaoelekeza kwamba kijiji hakina uwezo wa kuidhinisha ama kuuza ekari zaidi ya 50, na kwa kuwa alikuwa akihihitaji ekari 300, ilibidi awe na watu wengine watano, naye akiwa wa sita.
“..Akaja na majina sita, mikutano mikuu ikaidhinisha heka hizo 300 kwa watu hao tofauti lakini lengo ni kuwa eneo lote la ekari 300 ni lake. Baadaye akaja kwa mara nyingine ‘akatumia’ jina la kampuni anaitwa MP-Son, akaomba ekari 700 kwenye halmashauri ya kijiji mbali na zile 300, alipoomba halmashauri ilipendekeza apewe lakini kwa vile wao si wa mwisho lazima suala hilo kwanza lifikishwe kwenye mkutano mkuu wa wanakijiji. Akatoa ahadi ya kwamba tarehe 16 mwezi wa sita mwaka jana (2017) angefika nasi tuliandaa mkutano lakini hakufika.
“Kuanzia hapo mikutano imekuwa ikiandaliwa na kuahirishwa na imekuwa hivyo karibu mara tatu, ilipofika mwezi wa tisa mwaka jana, tukapeleka mapendekezo yale kwenye mkutano mkuu, wananchi katika mkutano huo wakasema lazima aje mwenyewe ili pamoja na mambo mengine wajue kwamba yale masharti ya mwanzo ya kumpa ekari 300 (alitakiwa alipe 5000 kwa kila mwaka kwa kila ekari kama ada) hayatekelezi na sasa anataka tena ardhi, wakataka wajue sababu.
“Tarehe 5 mwezi wa 11, mwaka jana (2017), Mpina akamtuma ndugu yake akajitambulisha kuwa ni msimamizi wa shamba, huyu alileta barua ya kuomba kuanza kusafisha lakini halmashauri ya serikali ya kijiji ikasema hapana… hatuwezi kukupa idhini kwa kuwa tayari wananchi walikwishakataa kutoa ekari hizo 700, na vile vile wananchi hao kupitia uongozi waliamua kugawana eneo hili ili waendelee na shughuli zao za kilimo. Hapo ndipo ulipoanza mzozo mkubwa, uongozi wa wilaya ukapiga marufuku wananchi kuendelea na shughuli zao eneo hilo na ukasema ni eneo la Mpina, ni shamba la Mpina,” alieleza Mwenyekiti huyo wa kijiji.
Alipoulizwa kuhusu hatua walizokwishakuzichukua kuhusu suala hilo, alisema ni pamoja na mamlaka ya kijiji kusitisha shughuli za Mpina katika eneo hilo na wakati huo huo wananchi kuendelea na kilimo kwenye eneo husika, hata hivyo, anasema yote hayo ni kazi bure, kwani Mpina akisaidiwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro amekuwa na nguvu zaidi yao.
“Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ulituvunja nguvu, walikuja hapa kijijini kutupatia maagizo wananchi wasiende kule shambani kwa kuwa tayari ni eneo la Mpina. Wananchi walikuwa tayari wanafanya kilimo cha mpunga, mashamba yao yakavamiwa na kuharibiwa, na Mpina akapanda mazao yake. hali ni mbaya,” alisema mwenyekiti huyo, huku akiweka bayana kwamba, uongozi wa kijiji umezisusia fedha kiasi cha shilingi milioni 35 zilizokwishawekwa kwenye akaunti ya kijiji cha Dala katika Benki ya NMB tangu mwaka jana kwa kuwa eneo hilo halijauzwa kwa Mpina au mtu mwingine yoyote, milioni hizo 35 ni sehemu ya shilingi milioni 50 zinazotakiwa katika hicho ‘kinachoitwa’ mauzo ya ardhi hiyo.
Akielezea zaidi mgogoro huo, mkazi mwingine wa kijiji cha Dala, aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Zuwewe, ambaye ni mjumbe wa halmashauri ya serikali ya kijiji, alisema; “Alikuja Luhaga Mpina kuomba maeneo kwa ajili ya kilimo sehemu inayoitwa Kivumba, awali, aliomba ekari 300 kupitia watu tofauti, kila aliyeomba alikuwa apewe ekari 50, kipindi hicho eneo hilo lilikuwa ni pori, masharti yalikuwa ni pamoja kulipia ‘kodi ya pango’ ya shilingi 5000 kwa kila ekari, ilikuwa mwaka 2009 lakini tangu wakati huo hadi sasa hakulipa, na kila tunavyomdai ilikuwa vigumu kulipa hizo shilingi 5000. Baadaye akaja akasema aongezewe ekari 700. Uongozi, tukasema uje uonane na wananchi.
“Tukapeleka suala hili kwa afisa mtendaji ili amlete Mpina, akaja mwakilishi wake tukakutana ofisi ya kata, tukamweleza matatizo yetu, tukasema tatizo letu ekari 300 za mwanzo hazijapimwa. Tukaenda kukagua na mwakilishi wake, kukagua eneo na kujua kama kuna kipande cha kumwongeza halafu pia kujadili suala la makubaliano ya ekari 300 za mwanzo.
“Kabla hatujaondoka, mtendaji wa kijiji na mwenyekiti akaongea na mwakilishi wake huyo, akamwambia kufika kule shamba tumetumia gharama ambazo ni pamoja na kukodi mapikipiki, vipi hata ‘maji ya kunywa’?  Ikabidi yule bwana na uongozi wa kijiji wakae pembeni wakatupa ‘maji ya kunywa’.
“Mtendaji na mwenyekiti wa kijiji akasema, mnaonaje tukiwezeshana lakini kila mtu aandike jina, cheo na saini yake. Tukafanya hivyo, tukapata posho zetu na gharama za pikipiki, tuliporudi baada ya siku mbili tatu hivi, yale majina yakatengenezewa muhtasari kwa sababu yalikuwa na saini zetu, wakaandika tumekubali aongezwe ekari 700 na saini zipo, wakaandika kwamba halmashauri ya kijiji ilikaa tarehe hiyo kukubaliana.”
“ Sasa tulipokutana na wananchi wakakataa. Mheshimiwa (Mpina) alipopata taarifa hiyo akaja akiwa na mkuu wa wilaya, pamoja na mkurugenzi wa wilaya na katibu tarafa. Alipokuja na mwenyekiti wetu akafungua mkutano, mkuu wa wilaya alikuwa msemaji, akasema tumekuja hapa si kwa vyeo vyetu, waziri kaja kama mkulima, tumekuja si kubomoa bali kujenga. Wakahoji kwa nini muhtasari ule unakataliwa wakati wahusika wamesaini, kila mwenye saini akahojiwa kuwa …hii saini si yako?
“Lakini kila tulipotaka kunyoosha mkono kujieleza, hatukupewa fursa hiyo. Tumenyoosha mikono hakuna kuchaguliwa kuongea, Mpina akasema mtake msitake halmashauri ya kijiji imenipa eneo, sisi tulinyoosha mikono kutaka kuhoji, mbona halmashayuri haina uwezo wa kutoa ekari zaidi ya 50 lakini tukashindwa kuhoji mambo kama hayo, mkutano ukafungwa wakaondoka, ule mkutano ulifanyika tarehe 18, mwezi wa tatu, 2018. Ulikuwa mkutano wa ndani sio wa wananchi, wajumbe tulipotoka tukamwita mtendaji wa kijiji na mwenyekiti, tukamwamba mtendaji tupe ule muhtasari unaosemwa tumependekeza apewe ekari 700, tulipouona ule muhtasari tukabaini haukuandikwa kwa hati (handwriting) ya mtendaji wa kijiji, vile vile tukamwambia orodha hii umeipata wapi, wakati tulisaini shambani si kwa madhumuni hayo? Tukaamuulizanani kaandika muhtasari huu, akasema mwakilishi wa Mpina, yeye alikuwa na kazi nyingi hivyo amesaidiwa.
“Basi, baada ya hapo ukafanyika mkutano mkuu wanakijiji wakawa wakali hadi wakatuita sisi wezi, tukapelekwa polisi ambao nao walitumia busara kutuliza hasira za wanakijiji,” alisema.
Lakini mwanakijiji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Lusekelo Charles Mwamwaja, alisema “…nakumbuka mwaka 2009 alikuja Mpina kuomba mashamba ekari 50, alikuja na watu watano, kila mmoja alitaka ekari 50, tulijua ni Mpina ila sheria inambana ndio maana akawa na watu hao.
“Tulikuwa na makubaliano kila ekari alipie shilingi 5000 lakini hakuna chochote alichokamilisha, tulichosikia mwaka jana ni kwamba mashamba yameuzwa kwa Mpina, na pesa imeshaingizwa katika akaunti ya kijji cha Dala, imetolewa milioni 35 bado milioni 15. Taarifa ya kuuza shamba tumepewa na katibu wa kijiji katika kikao cha wanakijiji, wanakijiji tuligomea, tukasema tunachotaka aje Mpina tufanya naye mazungunzo, mkataba wa kwanza hakutimiza masharti, sasa anataka anunue kabisa. Na baadhi ya wanakijiji wamekosa mashamba ya kulima, sasa ameshauziwa na pesa imeingia. Kila tulipomtaka aje, hakufika.”
Mwananchi mwingine kwa jina la Rehema Charles ambaye ni mjumbe wa halmashauri ya kijiji, alisema; “….sisi kwa nafasi yetu kama wajumbe tuna masikitiko makubwa kwa sababu, alishakuja kijijini, sisi halmashauri tumeingia katika uongozi mwaka 2014. Siku hiyo tulikubaliana tukaangalie kama ardhi ipo, tukaenda kuzungumza, tukakuta eneo ni kubwa kwa kutazama kwa macho, tukaangalia pori lingine analotaka la ekari 700 tukasema lipo, lakini lipimwe rasmi kwanza, halafu eneo hili la nyongeza lifike kwa wananchi waamue, lakini kabla ya hapo ya  hayo kufanyika, hilo eneo likalimwa kwa ubabe, tukajiuliza idhini ya kulima imetoka wapi? Tukaandika kusikitikia hilo suala kwamba hata halijafika mkutano mkuu, baada ya kutoka huko kila mtu akapewa elfu 30, tukajiorodhesha majina yetu, tukashangaa, hatukukaa kikao lakini tunaambiwa ni muhtsari wa kikao cha uamuzi. Tukashangaa, ametengeneza muhtasari kwa kutumia karatasi ya malipo ya posho.
“Kuna mchezo tumechezwa bila sisi kujua, hatuna ridhaa ya kuuza mali ya kijiji. Tukimwita Mpina hataki kuja, tukaandika kumtaka asiendelee na kilimo lakini hasikii, wananchi tuliwapa maeneo lakini akaenda kuyaingilia na kuvuruga na ameweka ulinzi mkali.
“Tayari milioni 35 ameingiza kinyume cha sheria kwenye akaunti bila kukubaliana nasi, hatujui nani alimpa akaunti, sisi halmashauri hatuna namba za akaunti, akaunti ya kijiji tunaitambua lakini kuingizwa kwa pesa hatujui, hatukushirikishwa kama halmashauri ya kijiji,” alisema.
Mwanakijiji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Nia Hamis Kitata ambaye ni mmoja ya walioharibiwa mazao yao, alisema; “Matarajio yetu sisi wakulima ni mashamba, mavuno ndio maisha yetu. Naomba Rais Magufuli utusaidia, huyu waziri wako anatusumbua.”
Naye Adolfina Elias, ambaye ni mjumbe wa halmashauri ya kjiji cha Dala, alisema wamekwishaonyeshwa taarifa ya benki ikionyesha kuwa shilingi milioni 35 zimekwishaingizwa kwenye akaunti. Alisema taarifa hizo wamezipata kutoka uongozi wa halmashauri ya wilaya.

Waziri Mpina, Mkurugenzi
Waziri Mpina alipotafutwa na mwandishi wetu, moja kwa moja alitaka suala hilo aulizwe mkurugenzi, akisisitiza kuwa majibu ya mkurugenzi huyo yanajitosheleza.
Katika maelezo yake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Sudi Mpili alisema; “Malipo ya shilingi milioni 35 yamefanyika kwenye akaunti ya kijiji, akaunti hii ilitolewa na mwenyekiti wa kijiji, ambaye alikuwa na mawasiliano na Waziri Mpina, ushahidi wa mawasiliano yao upo.”
“Urafiki wa Mpina na kijiji ulianza siku nyingi, mwanzo kabisa walikubaliana ili apate ekari 300 ni lazima awe na watu wapewe vipande vipande kwa kuwa kijiji hakiwezi kutoa ekari zaidi ya 50.”
“Katika utaratibu wa kawaida, kama ni ardhi inayozidi ekari 50 ni kwamba serikali ya kijiji ndio inapendekeza, kisha suala hilo linafika kwenye mkutano mkuu wa kijiji na baadaye Baraza la Madiwani na baada ya hayo, kwenda kwa Kamishna wa Ardhi. Sasa hili la ekari 700 halijapitia hatua hizo, liliishia ngazi ya serikali ya kijiji. Kwa hiyo suala la umilikashaji wa ardhi halijakamilika,”
“Suala la pili ukiondoa hilo la umiliki, ni suala la kumruhusu kutumia ardhi. Katika ili la kumruhusu, serikali ya kijiji ilikaa kikao wakaandaa muhtasari kuruhusu aendelee kutumia eneo hilo kwanza. Tulifanya kikao, tukauliza kila mmoja wakakiri hadi saini zao, kwa hiyo muhtasari ule ni sahihi,” alisema na kusisitiza kuwa bado umiliki wa ekari hizo 700 haujafanyika.


Comments