Featured Post

WAZAZI WANAWEZA KULINDA WATOTO DHIDI YA TUMBAKU




NA ALOYCE NDELEIO
Udhanifu kwamba madhara ya tumbaku na hususani uvutaji wa sigara huwa ni kwa wavutaji peke yao umekuwa hauna mashiko  kwani utafiti uliofanyika nchini Marekani umebaini hali tofauti.
Unabainisha  kwamba watu wazima wasiovuta sigara lakini walipokuwa watoto wazazi wao walivuta sigara mbele yao,wana hatari kubwa zaidi ya kufa kutokana na maradhi ya mapafu.

Watafiti wanasema kuwa kati ya watu laki moja ,watu saba hufa kila mwaka kutokana na madhara ya sigara waliyoyapata wakiwa watoto.
Watalamu wanasema kinga bora zaidi ya kuzuia watoto kutoathirika na sigara ni wazazi kuacha kuvutaji sigara kabisa, kama nyongeza ni kwamba wazazi wanaweza kuwalinda watoto wao dhidi ya matumizi ya sigara.
Wazazi wengi  hawapendi  watoto wao wawe watumiaji wa tumbaku ama sigara au ugoro kwa sababu zilizo wazi  kwamba ni matumizi yanasababisha matatizo makubwa kiafya yakiwemo saratani ya mapafu, magonjwa ya moyo na kiharusi yote yakisababisha vifo vya mapema au ulemavu.
Katika hali ambayo ni mbaya zaidi ni kwamba watoto  wanaweza kuingia kwenye mkumbo wa kuwa wavutaji waliokubuhu katika kipindi cha siku za awali za kuingia katika uvutaji wa sigara.
Miongoni mwake ni uvutaji kusababisha madhara kwa watoto katika hatua za awali kabla ya kufikia utu uzima kwa kusababisha madhara kadhaa ambayo hayawezi kurekebika  au  kugeuzwa, athari za kiafya na matatizo ya kiafya.
Kati ya vijana watano wa shule, mmoja ni mvutaji na inafahamishwa kuwa kujaribu kuvuta kunaanza watoto wakiwa  darasa la nne.
Kila siku takribani watoto 4,000 hujaribu kuvuta sigara ya kwanza na kila siku watoto 1,000 walio na umri chini ya miaka 18 huingia katika kundi la wavutaji wa kawaida.
Kutokana na  hali  hiyo zaidi ya wavutaji wapya 400,000 walio na chini ya umri huingia katika kundi la wavutaji kila mwaka na takribani theluthi moja yao  hufa  katika umri  mdogo kutokana na  magonjwa yanayohusiana na  kuvuta sigara.
Wazazi wanaweza kuchukua  hatua  za ufanisi  katika kuwalinda watoto wao dhidi ya kuanza kuvuta sigara au kuwa miongoni mwa wateja walioathiriwa na sekta ya tumbaku.
Kuwa mzazi  mzuri  na  anayetoa mchango wake  katika hali ya aina hii ni muhimu  lakini  yanahitajika mambo mengine zaidi ya  kuwaepusha watoto dhidi ya uvutaji.
Aidha wanatakiwa  kushughulikia  athari zozote zile zinazoweza kuathiri  uvutaji  nje ya kaya kwa kuhakikisha kuwa shule zinajitihadi kuepusha  na  kupunguza wimbi la vijana wanaovuta sigara na kupunguza soko la sigara kuzifikia.
Mfano  kampuni  nyingi za Marekani  zimekuwa zinatumia  takribani Dola  milioni  36 kwa siku katika kutangaza soko la bidhaa zake na zinawategemea  wavutaji  vijana kuchukua nafasi ya  wateja wao wanaozeeka  au kufariki.
Mtendaji mmoja wa kampuni ya sigara aliwahi kusema, “Msingi wa biashara zetu upo miongoni mwa wanafunzi wa shule za  elimu ya juu.”

Wazazi na jukumu la kupinga uvutaji 
Wazazi wanasema nini, wanafanya  nini na mawasiliano yao  kupitia maneno  yao na matendo yao  vina athari kubwa  kwa watoto na  hali  hiyo  inatakiwa itumike kwa  matumizi ya tumbaku  pia.
Tafiti  zinaonyesha kuwa matendo ya wazazi, tabia na maoni yao kuhusu  uvutaji  yana athari kubwa na huamua kama mtoto  aingie katika uvutaji au la.
Tafiti za hivi karibuni  zilibaini kuwa vitendo vya wazazi  kupinga uvutaji kama vile kuweka vikwazo  dhidi ya uvutaji  nyumbani  au  kukaa kwenye  maeneo  ya migahawa  yaliyopiga marufuku uvutaji  vimekuwa vinachangia  kupunguza uvutaji  miongoni mwa watoto.
Hali hiyo hususan wazazi kuchukua hatua zifuatazo katika kuhakikisha kwamba watoto  wao hawavuti au kubakia kuwa watu wasiovuta ni pamoja na “Kama  huvuti, usianze  kuvuta! Kama  unavuta acha.”
Utafiti  unaonesha kwamba watoto ambao wazazi wao  wanavuta ni dhahiri watoto hao watavuta na kuwa wavutaji  waliobobea katika umri mdogo.
Wakati wazazi  wanaacha kuvuta, watoto wao ni  dhahiri huanza kuvuta kwa nadra na inawawia rahisi kuacha kama walishaanza kuvuta.
Kama unavuta ni muhimu kushirikiana mapambano yako dhidi ya uvutaji na watoto. Watoto hudharau ni kwa kiwango  gani  huwa ni vigumu kuacha uvutaji.
Katika kuonesha ni jinsi  gani  ilivyo  vigumu  kuacha  na kufanya kuacha kuonekana si rahisi kunaweza kusaidia  kuondokana na dhana  hiyo.
Kuendelea  kujaribu  kuacha, licha ya  hali ya ugumu  inayokuwepo pia mzazi anatakiwa kupeleka ujumbe mzito wa kupinga uvutaji wa sigara.

Weka mazingira yasiyo ya uvutaji nyumbani
Mazingira yasiyo ya uvutaji nyumbani hufanya uwezekano wa watoto  kuingia katika uvutaji kuwa mdogo hata kama wazazi wanavuta.
Kwa kutoruhusu mtu  yeyote  kuvuta  katika mazingira ya  nyumbani  wazazi si tu  kwamba wanawafanya watoto wao kutojihusisha na uvutaji  bali  pia  huwafanya  kuwa na matamshi mazito ambayo wanayaamini kuwa uvutaji ni jambo  lisilopendeza, halitakiwi au halikubaliki.
Aidha mzazi  anawajibika kuwaambia watoto  wake  kuwa  yeye havuti na asilani asingependa watoto wavute na  ataudhika sana wakifanya hivyo.
Tabia za wazazi, maoni yao na hisia zao kuhusu hali ya watoto wake kuvuta kutaathiri au kutoathiri watoto hata pindi  mzazi  akivuta sigara.
Hali kadhalika wazazi wanatakiwa  kuhakikisha kuwa watoto wanapata ukweli. Kwa kuhakikisha kuwa watoto wanafahamu  madhara ya uvutaji wanaweza kuwasaidia kuwa na mtazamo  hasi kuhusu kuvuta sigara na athari zake na kwamba watoto wanaokuwa na mtazamo  huo hasi ni dhahiri haitakuwa rahisi kwao kujiingiza katika uvutaji.
Msisitizo  uwe kwenye  athari za papo hapo kwenye afya. Vijana wengi  wanakuwa na imani  potofu kuwa uvutaji  hauna madhara ya moja kwa moja kwenye afya zao na kwamba ni hadi wafikie umri wa kati ndipo wataathirika.
Hata hivyo uvutaji unasababisha athari za papo hapo na  nyingine zikinyemelea  katika kipindi  kifupi  kinachofuata ikiwa ni pamoja na kikohozi cha mara kwa mara, matatizo ya kupumua, uwezekano wa kukumbwa na maradhi na kupunguza  ufanisi katika utendaji wa kazi.
Msisitizo uwe kwenye madhara ya uvutaji katika muonekano wa maumbile. Matangazo ya sigara yanatoa taswira kuwa uvutaji una mvuto wa kupendezesha na ambao unawafanya  watoto kuwa na taswira hiyo kuwa ndio sababu itakayowafanya  wavute sigara.
Lakini katika hali halisi ni kwamba uvutaji unayafanya meno  kuwa na kutu, kutoa harufu mbaya kinywani, nguo kunuka na  jambo jingine baya zaidi ni kwamba husababisha nguzo ya usoni  kukunjamana.
Aidha ipo haja ya wazazi kuwaelewesha na kuvunjilia mbali  imani kuwa kila mtu anavuta sigara. Watoto wengi wanakadiria isivyo  idadi ya wavutaji miongoni mwa vijana na makadirio  hayo ni miongoni mwa vichocheo vinavyosababisha wao  kuanza kuvuta sigara.
Kwa mfano watoto au vijana walio kwenye umri mdogo  wanaamini kuwa asilimia 67 ya watu wazima wanavuta sigara  na kwamba asilimia 54 ya vijana hivi sasa ni wavutaji, lakini  ukweli ni kwamba ni chini ya asilimia 25 ya watu wazima na asilimia 17 ya vijana wanavuta sigara.
Wazazi pia wanaweza kuwasaidia vijana wasivute kwa kutumia   mienendo  mizuri. Kwa mfano watoto wanaofanya vizuri  kwenye masomo yao na wanaoshiriki ipasavyo kwenye  shughuli za michezo si rahisi kujiingiza kwenye uvutaji  na wazazi wanalazimika kuwashawishi na kuwaunga  mkono katika shughuli kama hizo.
Kama nyongeza kwenye hali hiyo wazazi wanaweza kusisitiza kwa kutumia njia sahihi na za ukweli  kwa kuzungumza na watoto wao  kwa kuwafanya wawe waangalifu  dhidi ya aina ya  marafiki wanaoshirikiana na watoto wao na kupenda kujihusisha  na maisha ya watoto  wao.
Kwa hali hiyo wazazi  si tu watakuwa wamepunguza njia ambazo  zinaweza kuwaingiza katika tabia  nyingine  hatarishi kama vile matumizi ya pombe, matumizi ya dawa nyingine au  kuanzisha  uhusiano wa ngono na tabia nyingine  zinazolandana na hali hiyo.

Malezi  bora  hayatoshi
Wakati wazazi wanaweza kutoa mchango  muhimu  katika kuwaepusha watoto wao dhidi ya uvutaji, watoto wanahusika  katika kukabiliana na atahri nyingine ambazo zinajitokeza nje ya majumbani mwao ambazo zinaweza kuchangia kuingia kwenye  uvutaji au la.
Jambo  muhimu  ni kwamba  kampuni  zinazotengeneza  sigara  zinatumia zaidi ya  dola  bilioni 13.1  kwa mwaka  kwa ajili ya kutafuta soko na  kufanya  promosheni  za bidhaa zake  na   shughuli hiyo ya masoko huwafikia zaidi watoto.
Tafiti za kitaaluma  zimegundua kuwa watoto wanakuwa na umakini  mara tatu  kuhusu matangazo ya tumbaku  kuliko  ilivyo kwa watu wazima. Wanaweza kushawishika kuvuta  kutokana na shinikizo la  soko  kuliko  ilivyo kwa  shinikizo kutoka kwa vijana  wengine.
Aidha theluthi  moja ya watoto walio na umri mdogo  wanajihusisha na uvutaji  kutokana na  shinikizo  linalotokana na  matangazo na promosheni  za  bidhaa za tumbaku.
Kwa ujumla  kampuni kubwa za  sigara  zimekuwa zinajaribu  kuhamisha  lengo lao na  kuunga mkono  njia ambazo  zinaweza kuzuia  kuanzishwa kwa  sheria na  sera mpya za kuzuia na kupunguza matumizi ya tumbaku miongoni mwa watoto kwa  kuliweka  na kuliboresha wazo kuwa  tatizo  hilo limo mikononi mwa wazazi.
Lakini  kuliweka  tatizo  lote  hilo  mikononi mwa wazazi  hakutapunguza  upatikanaji wa  sigara  kwa wanunuzi walio na  umri  mdogo, kupunguza  soko la tumbaku  linalowafikia  watoto, kuanzisha maeneo  yasiyotakiwa kuvuta sigara au kupunguza  na kulifikia soko na  kutumia tumbaku  wanapokuwa mbali na majumbani mwao.

Hatua zinazoweza kuchukuliwa na wazazi 
Ili kukabiliana na vigezo ambavyo vinawafanya watoto  kuingia kwenye matumizi ya tumbaku  wazazi wanaweza kuwaonesha kwa kuchukua  hatua  kadhaa.
Wazazi wanatakiwa kuwaonesha watoto wao jinsi  matangazo ya sigara  na picha nyingine  yanavyotengenezwa kwa ajili ya kuwarubini.
Kwa hali hiyo  wazazi wanaweza kupunguza  madhara makubwa yanayosababishwa na uvutaji wa sigara  na taswira chanya  ambazo  watoto wanakutana nazo kila siku kwa kuzungumza na watoto hao kuhusu uongo uliojificha ndani ya  matangazo hayo.
Aidha  uongo  huo ni kama vile kuongeza ladha, kuwa ndio  kukomaa, nzuri ni poa na jinsi gani kampuni zinavyowarubini  watoto  kuingia  kwenye  uvutaji  na baadaye kubobea katika   tabia hiyo.
Wazazi  wanawajibika pia kuyafanya maeneo ya shule  wanazosoma watoto wao  kutokuwa na  matumizi ya tumbaku.
Hili  linawezekana  kwa wazazi  kujihusisha katika shughuli  shuleni wanakosoma watoto wao kwa  kuhakikisha kuwa  shule  hizo  zinafuata  kwa  ukamilifu  sera za kudhibiti  matumizi ya tumbaku.
Wanaweza kudhibiti  matumizi  ya  tumbaku  kwa vijana kwa kuunga  mkono  mikakati ya ndani kama  vile  sheria za nchi   kwa  kuhakikisha kuwa  migahawa na  maeneo  mengine ya  umma hayahusishwi na matumizi ya tumbaku au  mikakati ya kuhakikisha sheria zinazozuia watoto kuuziwa sigara zinatekelezwa.
Vilevile  wanaweza kuiunga mkono serikali  katika kuhakikisha  kuwa  sheria  zinazozuia  soko la sigara  kuwafikia watoto zinatekelezwa.
Hata  hivyo  wazazi wanatakiwa kuunga mkono  mipango ya serikali ya kudhibiti  na kupunguza matumizi ya  tumbaku miongoni mwa watoto kama vile kuongeza kodi  jambo ambalo  linafanya kiwango cha uvutaji sigara kupungua miongoni mwa  watoto.

Comments