Featured Post

WAVUVI WATUMIA MIPIRA YA KONDOMU KUIMARISHA USALAMA WAO MOMBASA




Abdalla Seif Dzungu na Anthony Irungu BBC Swahili
Miezi mitatu iliopita wavuvi sita katika pwani ya Kenya huko mjini Mombasa walipatwa na janga kubwa baada ya boti yao kuzama nyakati za usiku.
Wanne kati yao waliaga dunia baada ya wimbi kubwa kuwapiga muda mfupi baada ya ajali hiyo ya boti swala lililowafanya kutengana.

Kulingana na Matano Jafar ambaye ni mmoja wa manusura wa janga hilo yeye na mwenzake walilazimika kuogelea kwa takriban saa 11 hadi ufukweni mwa bahari.
''Ilikuwa mwendo wa saa tano usiku baada ya kumaliza kuvua ndani ya bahari hindi wakati boti yetu iliokuwa imetubeba ilipopinduka ghafla.Tulikuwa wavuvi sita na tukaanza kupeana moyo kwamba tuogelee polepole hadi ufukweni, lakini kwa ghafla kuna wimbi kubwa lilitupiga na kututawanya''.
Matano ambaye ni mvuvi na muogeleaji wa kujitolea anasema kuwa baada ya ajali hiyo wenzake wanne waliangamia huku akisalia na mwenzake mmoja ambaye walisaidiana kuogelea hadi ufuoni.
Na tangu tukio la kisa hicho mvuvi huyo na wenzake wametilia mkazo swala la mawasiliano hatua iliowalazimu kuvumbua mbinu mpya ya kulinda usalama wao.
Nilipowatembelea wavuvi hawa katika ufukwe wa bahari wa Nyali mjini Mombasa mwendo wa saa kumi na mbili alfajiri, nilikutana nao wakiandaa nyavu zao pamoja na boti lao ili kuanza safari ya muda mrefu ndani ya bahari hindi.
Lakini kitu kilichonuvitia zaidi ni hatua yao ya kugawana mipira ya kondomu miongoni mwao!
''Sisi hutumia mipira hii ya kondomu ili kulinda simu zetu kutoingia maji wakati tunapokuwa baharini tukiendelea na shughuli zetu za uvuvi'', alisema mmoja ya wavuvi hao.
Mvuvi huyo anasema kuwa wanapoingiza simu zao za mkononi katika mipira hiyo zinasalia kuwa salama na ni rahisi wao kuzungumza na wateja wao walio nchi kavu mbali na kuitisha msaada wakati wa hatari baharini.
Ni msimu wa kusi ambapo wavuvi hushauriwa na serikali kutofanya uvuvi kutokana na bahari iliochafuka na mawimbi makali.
Hatahivyo ufukara unawashinikiza wavuvi hao kuendelea na safari zao za uvuvi.
''Hatuwezi kuketi nyumbani kwa sababu ya tahadhari iliotolewa na serikali kwamba bahari ni chafu, sisi tuna familia zinazotutegemea, nani ataziangalia iwapo tutasalia nyumbani?'', Matano anauliza.
Katika jamii za kihafidhina kama hii inayoishi pwani ya Kenya, mipira ya kondomu hushirikishwa na tendo la ngono.
Hivyobasi ununuzi ama hata ubebaji wake ni swala linalozungumzwa kwa siri kubwa kutokana na kazi yake.
Kwa wengi ni mwiko kuonekana na kinga hiyo , hatua inayoweza kuwashangaza wengi unapopatikana ukitembea na mipira ya kondomu ambayo hazijatumika mfukoni.
Kulingana na wavuvi hawa swala la wao kuelekea nyumbani wakiwa wamebeba paketi za mipira hiyo limekuwa la kawaida.
''Kwa sasa wake zetu wamezoea kwamba wakati mwingi sisi hutumia mipira hii kuzuia simu zetu za mkononi kuingia maji tunapokuwa baharini. Lakini kitambo ilikuwa vigumu kuelezea unapokamatwa na mipira hii ambayo mara nyingi husahaulika katika mifuko lakini tulikuwa tukiwaelezea kwa umakini hadi wanaelewa''. alisema mvuvi huyo.
Huku harakati za kutaka kujipatia kipato kwa wavuvi hawa masikini zikiendelea , wasiwasi wao sio tu kiwango cha samaki wanachovua mwisho wa siku lakini kuendelea kufanya uvumbuzi utakaowahakikishia usalama wao.


Comments