- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Tahadhari: Baadhi ya simulizi na picha zinaogofya
Akiwa
amekalia benchi la mbao, mtoto huyu mwenye umri wa miaka mitatu anaonekana
mwenye furaha. Anatazama kipindi cha vibonzo cha Ninja Turtle.
Ni vigumu
kuamini kwamba Comfort anadaiwa kuwa mchawi.
Hii ndiyo
sababu kwamba yeye na nduguze wakubwa wawili wanaishi katika makao ya dharura
katika mji wa Calabar, kusini mashariki mwa Nigeria.
Ni nyumba
ndogo iliyotengenezwa chini ya ardhi na iliyo na runinga. Mlango hufungwa mara
kwa mara kwa usalama wa watoto hao.
Makao hayo
ni ya muda hadi pale watoto hao watakapoanza kuishi na familia zao.
Lakini
hakuna mtu anayetaka kuishi na watoto hao wanaoitwa wachawi katika nyumba zao.
Baada ya
kipindi chake cha vibonzo kujisha, Comfort anaonekana nje na kuinua shati lake
linaloonyesha makovu ya vidonda mgongoni mwake.
Makovu
hayo yanatokana na kisu cha moto kilichotumiwa na jirani ili kumlazimu kukubali
kuwa mchawi.
Majina ya
watoto katika hadithi hii yamebadilishwa. Maelezo yamefichwa juu ya picha ili
kuwalinda
Kuelekezwa gizani
Mapema
mwezi Februari, Comfort na dadake Hope, 15, na ndugu yao mdogo, 5, Godbless
walikuwa wakiishi na bibi yao Christiana karibu na eneo la Akampka.
Wazazi wao
walifariki katika hali isiyoeleweka, na huku hilo likiwa limemefanya Christina
kuwa na wasiwasi kuhusu watoto hao aliamua kuwachukua.
Huku akiwa
na virusi vya HIV na kukosa kunywa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo,
hali ya kiafya ya Christiana ilikuwa inadorora na alikuwa akiendelea kukonda.
Huku
akiwalaumu watoto hao kwa kusababisha hali yake mbaya, Christiana aliwapeleka
katika kanisa lao kwa uongozi.
Wakiwa
kanisani, nabii mmoja alithibitisha hofu yake kwamba wasichana hao walidaiwa
kuwa wachawi.
Kwa
Christiana, hilo lilithibitisha chanzo cha kifo cha mwanawe wa kike na mkwewe,
ugonjwa wake na tabia mbaya ya watoto wake.
Muda mfupi
baadaye, jirani kwa jina Rankin alimsikia Christiana akiwashutumu watoto hao
kwa kukata kamba ya kuanikia nguo katika ua wa familia hiyo wakiwalaumu kuwa
wachawi.
Baada ya
kuzungumza na Christiana na kugundua maelezo zaidi kuhusu shutma hizo, Rankin
alirudi siku iliyofuta na rafikiye.
“Alianza
kutupiga na kutwambia kumuondoa bibi yetu kutoka kwa ulimwengu wa uchawi,"
alisema Hope.
Watoto hao
walijaribu kutoroka kupitia minazi iliokuweko, lakini walizingirwa na wanaume
hao wawili na kupelekewa katika nyumba za majirani.
Mikono yao
na miguu ilifungwa kwa pamoja na Rankin akiweka chuma motoni.
“Baadaye
walituuliza iwapo sisi ni wachawi," anasema Hope "na tukawaambia
hapana."
“Hivyo
basi alianza kutupiga mmoja baada ya mwengine akitumia chuma hicho cha moto
kuanzia alfajiri hadi mchana.”
Damu
ilimwagika ardhini huku wakilazimishwa kukiri.
“Hatimaye
tulisema ndio," anasema Hope. "Baadaye walituuliza iwapo ni sisi
tuliomuua baba yetu na mama yetu-tulisema ndio."
“Walituuliza
iwapo matatizo haya yoyte katika familia yetu - ni sisi tulioyasababisha-
tulisema ndio."
Baada ya
kutembelea kanisa lililojengwa kwa udongo ambapo watoto hao wanasema kuwa
walipigwa na kuchomwa, nabii aliyewaita kuwa wachawi hakuweko.
Badala
yake nilikutana na mchungaji Israel Ubi. Anasema kuwa hakuna hata mtu mmoja
kutoka kanisa hilo anayeweza kutoa madai kama hayo ama hata kufanya matambiko
kuwakamata watu wanaodaiwa kuwa wachawi.
“Hakuna
uchawi hapa,” anasema.
Aliposukumwa
zaidi kuzungumzia suala hilo, alikiri kwamba kanisa hilo lilikabiliana na
mashetani na majini ambapo watu wengi katika eneo la Niger Delta wanaamini kuwa
yapo katika maeneo ya bahari na miti.
Ni mjomba
wao watoto hao Sunday ambaye aliripoti kuhusu kisa hicho cha chuma cha moto kwa
polisi.
Dereva wa
teksi, ambaye anasema haamini uchawi upo alimshutumu nabii aliyedai kwamba
watoto hao ni wachawi.
“Kutokana
na hali yake ya kiafya, mamangu aliamini maneno yake. Manabii hawa ni wahalifu,
ni watu wanaoharibu maisha ya watu.”
Unyanyapaa
wa kuwataja watoto kuwa wachawi ni suala la hivi karibuni katika jimbo la Delta
, ambalo lililibuka miaka ya 1990. Kabla ya hilo, wanawake wakongwe walikuwa
wakilengwa na madai ya kuwa wachawi.
Kufikia
2008, ilikadiriwa kuwa watoto 1500 walibandikwa kuwa wachawi katika majimbo ya
Akwa Ibom na Cross Rivers kusini mashariki mwa Nigeria.
Kulingana
na utafiti tangu wakati huo, visa ambavyo vilikuwa vimenakiliwa vinashirikisha
visa vya watoto na watoto wachanga ambao walidungwa misumari vichwani,
kulazimishwa kula simiti, kuchomwa kwa moto, kuchomwa na tindi kali, kupewa
sumu na hata kuzikwa wakiwa hai.
Ripoti ya
shirika la watoto la Umoja wa Mataifa Unicef mwaka 2010 inasema kuwa ni watoto
wasioweza kujitetea kwa mfano walio na ulemavu wa maumbile na wenye magonjwa
kama vile kifafa ambao wanalengwa zaidi.
Wengine
wamebandikwa kuwa wachawi kwa kuonekana hawashughuliki sana na mambo
yanayoendelea, ni wavivu ama walio na tabia mbaya.
Sheria
dhidi uhalifu nchini Nigeria inazuia kumtuhumu mtu ama hata kutishia kumtumu
mtu kwamba ni mchawi. Na sheria ya kuwalinda watoto ya mwaka 2003 inasema kuwa
ni makosa kumpiga mtoto ama kumuumiza kwa njia yoyote.
Hata hivyo
huku sheria hiyo ikiidhinishwa katika ngazi ya kitaifa, majimbo 36 ya taifa
hilo bado hayajaidhinisha. Hii inayapatia majimbo husika haki ya kibinafsi
mbali na majukumu ya kuunda sheria zao zitakazoweza kusaidia kukabiliana na
matatizo kama hayo. Ni majimbo robo tatu pekee ya Nigeria ambayo yameidhinisha
sheria hizo za kuwalinda watoto na ni jimbo la Akwa Ibom pekee ambalo limeweka
sheria muhimu zinazohusiana na unyanyasaji wa wanaodaiwa kuwa wachawi. Sheria
yake ya mwaka 2008 imesema kiuwa wale watakaowaita wenzao wachawi watahukumiwa
hadi miaka 10 jela. Na licha ya shinikizo, Jimbo la Cross River bado
halijabadilisha sheria ya mwaka 2009 ili kuharamisha vitendo kama hivyo.
Lakini
licha ya kujaribu kutangaza kitendo hicho kuwa cha uhalifu, tatizo la watu
kuitwa wachawi linaendelea mbele ya macho ya serikali za majimbo hayo na
maafisa wa polisi wa Akwa Ibom na Cross River.
Oliver
Orok, Waziri wa maendeleo na masuala ya kijamii wa jimbo la Cross River
aliambia BBC kwamba wizara inafanya kazi kuhakikisha kuwa tatizo hilo
linaangamizwa.
“Serikali
ya Jimbo hilo kwa ushirikiano na Unicef na washirika wengine wa kimaendeleo
walipanga mkutano kuzungumzia kuhusu kufanyia marekebisho sheria, miongoni mwa
vitu vingine suala la kuwaita watoto kuwa wachawi na madhara yake, alisema
Bwana Orok.
Waziri
huyo anasema kuwa sheria ya uhalifu imefutilia mbali vitendo kama hivyo.
Hatahivyo miaka 10 baadaye hakuna mtu aliyeshtakiwa mahakamani.
Kumekuwa
na ongezeko la kampeni katika jimbo hilo ili kukabiliana na tatizo hilo.
Kulingana na Bwana Orok, fedha pia zimetolewa kujenga nyumba ya watoto waliopo
hataraini.
Ameongezea
kwamba iwapo serikali itapelekewa kesi kama hizo itakabiliana na makanisa kama
hayo na manabii wake. Wakili james Ibor anasema kwamba maafisa wa polisi
hawapati ufadhili wa kutosha ili kuweza kufanya uchunguzi kama huo.
“Kila mara
tunalazimika kuweka shinikizo kuhakikisha kufanyika kwa uchunguzi,"
anasema Ibor anayesimamia shirika moja lisilo la kiserikali mjini Calabar kwa
jina Basic Rights Counsel Initiative (BCRI). Shirika hilo huangazia visa
vinavyohusu unyanyasaji wa haki za watoto mbali na kusimamia nyumba ambayo
Comfort na nduguze wanaishi.
Ananiambia
kuhusu watoto wawili ambao walipewa sumu na baba yao ambaye aliamini kwamba
walikuwa wachawi. Alikiri kuwaua lakini hakukuwa na vifaa vya kutuma sampuli za
damu mjini Lagos ili kuthibitisha sababu za kifo za watoto hao.
Mwaka
mmoja baadaye, miili yao ipo katika chumba cha kuhifadhia maiti na baba yao
bado hajashtakiwa.
Ibor
anasema kuwa kesi zao zimekwama kwa miaka sasa.
Anasema
kuwa kazi yake imefanywa kuwa ngumu kutokana na uzembe wa maafisa wa polisi na
serikali kuchunguza masuala tata mbali na jamii na familia kuonyesha ishara za
kutotaka kutoa ushahidi.
Robo ya
kesi zinazoendelea zinahusiana na uchawi anasema. Lakini suala hilo linashirikishwa
sana na majimbo ya mashambani nchini Nigeria.
Miezi sita
iliyopoita, vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti kuhusu watoto 40 ambao
waliokolewa kutoka kwa kambi za unyanyasaji za waganga katika mji mkuu wa
Abuja.
Na Mwezi
Mei mjini lagos, mvulana mmoja alipigwa vibaya na mamake kwa kutumia kiboko.
Tunazo
sheria, alisema Ibor. ''tatizo sio sheria - tatizo ni kuzitekeleza sheria hizo
na hadi hilo lifanyike watoto wetu hawako salama''.
Na
amewalaumu baadhi ya manabii na wachungaji kwa kuleta hofu miongoni mwa wakazi
wa jimbo la Niger delta ambapo umaskini na imani za kichawi imesambaa.
Kufukuza mashetani
Jasho
linaonekana likidondoka katika uso wa msichana anayegaagaa akiwa sakafuni.
Mtu mmoja
anamshika kiunoni kabla ya kumzungusha. Lakini hii sio densi, ni mbinu ya
kumfanya mtoto huyo kuondokwa na uchawi.
Wachungaji
watatu wameunda timu ya kumponya msichana huyo mwenye umri wa miaka 15.
Kwa muda
wa dakika 30 wanamchapa kichwa chake mara kadhaa, wakimfinya masikio mbali na
kumshika tumbo.
Nguo zako
zinachomeka, kichwa chako kinachomeka tumbo lako linachomeka, walirejelea
matamshi hayo usoni mwake huku wakimpindua sakafuni.
Joy
anaenua mikono yake kujikinga. watoto wanne wamewekwa katika orodha ya
mchungaji Emmanuel kutolewa mashateni jioni hii, mdogo wao kabisa ana umri wa
miaka minane.
Nguvu
zinatoka kwa mtakatifu, anaelezea kabla ya tambiko hilo kuanza la kupunga
mapepo kuanza.
Anatupatia
nguvu kufanya kazi yetu ili kuwaokoa watoto. Unapowaombea watoto unaona mapepo
- ukizungumza nao utasikia yakizungumza.
Tunapokamilisha
shughuli hiyo mtoto anakuwa kama mwendawazimu ambaye amepona wazimu.
Mchungaji
anaelezea kwamba kanisa lake la Calabar linatoa huduma kwa jamii yote kwa
jumla.
Maombi
haya huwazuia wazazi kuwakataa watoto wao, huzuia mapepo hao kuwapoteza,
anasema.
Nani
anayejua huenda wakawaoa watoto wao wa kike, anaongezea, hivyo basi kabla ya
wewe kugundua, uchawi tunaokabiliana nao tayari upo nyumbani kwako.
Mchungaji
Eunice anazungumzia kuhusu mapepo anayomtuhumu Joy kuwa nayo.
“Ulihudhuria
mkutano wa wachawi? Wewe ni mchawi? Huwa unakunywa damu ya watu? Huwa wala
nyama ya binadamu? Huwa unauwa?”
“Nimemwangamiza
mtu mmoja pekee," Joy mwishowe anasema kwa sauti akilia.
Ni baada
tu ya msichana huyo kuzirai na kuanguka sakafuni ambapo shughuli ya kumtoa
mashetani na uchawi huaminika kuwa imefanikiwa.
Wakili
James Ibor anasema makanisa ya Kipentekosti kama hayo huwahamasisha waumini
wake kulaumu uchawi kwa masaibu yanayowakumba maishani au kwa taabu wanazopata.
Kisa hicho
cha karibuni kinahusisha mvulana aliyechapwa na wazazi wake baada ya pikipiki
ya familia hiyo kuharibika; katika kisa kingine, msichana alituhumiwa kuwa
mchawi, na kuchapwa viboko na babake baada ya babake huyo kufutwa kazi.
“Huwa
wanatumia hofu kuwadumisha waumini wao ambao kila wakati hutoa sadaka na fungu
la kumi (mchango wa kila wiki).
“Hiyo
ndiyo njia pekee ambapo wanaweza kuendelea kuwa na maana kwenye jamii na
kujipatia pesa.”
Mwaka
uliopita UN iliandaa warsha yake ya kwanza iliyoangazia uchawi, nchini Nigeria
na mataifa mengine.
Katika
ripoti baada ya warsha hiyo, umoja huo ulisema "idadi kamili ya waathiriwa
na ukatili huu haijulikani, na inaaminika kwamba visa vingi huwa haviripotiwi”.
Umoja huo
pia ulieleza mchango ambao hutekelezwa na "wajasiriamali wa kiroho"
katika kueneza na kuhalalalisha wasiwasi unaohusiana na itikadi za uchawi
katika jamii, na sana, kuwepo kwa watoto wachawi.
Kufungwa kwenye mti
Bassey
anakumbuka jinsi wasichana wawili walivyotuhumiwa na mchungaji miaka miwili
iliyopita katika kanisa la Divine Zion of God Church katika mji mdogo wa
Akpabuyo, jimbo la Cross River.
Muumini
aliyekuwa na uja uzito alikuwa amepitisha muda wake wa kujifungua kwa wiki
kadha, na wasichana hao wa miaka saba na 10 walidaiwa kuhusika na wakadaiwa
kuwa wachawi.
Mwanamke
huyo alikuwa amekwenda kwa mchungaji katika kanisa lake na kulipa pesa apewe
ufunguo. Ingawa alijifungua vyema muda mfupi baadaye, tayari madhara ya kitendo
chake yalikuwa yametendeka.
Wiki moja
baadaye, Bassey alisikia kilio cha wasichana hao alipokuwa anarejea nyumbani
kutoka shambani.
Walikuwa
wamefungwa kwenye mnazi, na walikuwa wanapigwa kwa vijiti na panga na wanaume
watatu.
Ebe Ukara,
afisa katika Kamati Tekelezi ya Haki za Watoto eneo la Akamkpa, anasema 60% ya
visa vya kudhalilishwa kwa watoto ambavyo hufikishwa katika meza yake huwa
vinahusiana na uchawi, na mara nyingi hutokana na tamko la mchungaji.
Wachungaji
hao, anasema, wanaweza kujipatia pesa nyingi sana kutoka kwa watu wanaokimbilia
kwao kuomba msaada, ingawa anasisitiza kwamba si makanisa yote ya Kipentekoste
ambayo yanahusika katika kuwatapeli waumini.
Lakini kwa
"manabii wa uongo", watoto ndio rahisi zaidi kusingiziwa. Wanaweza
kusingiziwa kwa umaskini na madhila yanayokumba familia nyingi na jamii.
Kwa
kuangalia tu mabango makubwa ambayo yametundikwa kwenye mizunguko ya barabara -
kuanzia jiji kuu la Abuja hadi kwenye Niger Delta - pombe na ukombozi wa kiroho
ndizo biashara kuu zaidi Nigeria, bidhaa zinazonunuliwa na kuuzwa.
Kila bango
linaahidi muujiza - jinsi ya kupata kazi, kumpata mchumba, kukabiliana na
kuharibika kwa mimba, utasa au ugumba, na bila shaka pia kukabiliana na uchawi.
Lakini
mabango haya pia yanaonyesha mambo mawili makuu kuhusu imani za Kipentekoste
ambazy imeenea sana nchini Nigeria tangu miaka ya 1970.
Kwanza,
aina hii ya Ukristo husisitiza zaidi ufanisi na pesa au mali tele - iwapo mtu
hajafanikiwa maishani, basi hiyo ni ishara kwamba kuna jambo ambalo haliko sawa
pahali.
Pili,
makanisa haya ya Kipentekoste huuonesha ulimwengu kama ukumbi wa vita kati ya
nguvu za Mungu na nguvu za kishetani.
Kwa hivyo,
makanisa haya ya Kipentekoste yameendeleza na kuvumisha dhana kwamba mali
inapatikana kwa urahisi, lakini kwa wengi huzuiwa kuipata na nguvu za
kishetani.
Lakini
viongozi hawa wa makanisa Nigeria si kwamba wameanzisha dini ya kipekee Afrika
au kwamba wanafuata utamaduni na itikadi za Kiafrika.
Badala
yake, wanaiga wenzao wa Marekani ambao makanisa yao hufanya kazi zaidi kama
majukwaa ya kuunda himaya za kiuchumi zaidi badala ya kuwa makundi ya kidini.
Hili
limesababisha kuwepo kwa imani mahuluti hivi, ambapo wameunganisha itikadi za
wenyeji hasa imani katika ushirikina na aina kali ya Ukristo ambayo wakosoaji
wanasema huwafanya waumini kuwa kama watumwa wa kiroho.
“Makanisa
haya ya 'uyoga' ni tatizo kubwa sana - manabii wao huongozwa na pesa,"
anasema Ukara.
Msemo huu
wa 'makanisa ya uyoga' hutumiwa kurejelea makanisa haya kutokana na hali kwamba
ni makanisa madogo madogo yenye vyumba visivyo rasmi na huchipuka popote pale
kama uyoga na kukua haraka sana.
Kwa
kiwango kikubwa huwa hayadhibitiwi na serikali.
Moja ya
makanisa hayo ni Ark of Noah (Safina ya Noah), kanisa linalopatikana Calabar
Kusini.
Nyumba ya Mungu
Ndala dogo
za aina ya Winnie the Pooh zilizo nje ya mlango ndiyo ishara pekee kwamba ibada
ya wokovu ya utakasaji inaendelea ndani.
Huku akiwa
amevalia shati la rangi ya njano, Nabii Gideon Okon anasimama huku akiwaombea
watoto watatu waliotuhumiwa kuwa wachawi.
“Mungu
huyafungua macho yangu kuniwezesha kuyaona matatizo ya watu hawa," Okon
anasema. "Hivyo ndivyo ninavyoweza kubaini nani mchawi.”
Anasema
kwamba hakuna anayewaleta watoto kwake, kwamba huwa anapata ufunuo anapofunga
na kujinyima chakula na kufanya maombi.
“Iwapo mtu
huyo yuko tayari na anataka kukombolewa na kutakaswa, basi huwa tunaanza
kujadiliana kuhusu malipo," anasema.
Okon
anasema malipo hutegemea aina ya tambiko linalohitajika kufanywa kumtakasa
mhusika.
“Walio na
nguvu na hatari zaidi kuwaua huwa ni mapepo wa baharini,” anasema. "Kwa
hao huwa natoza naira 200,000 ($556), lakini ni bei ya kuzungumza na wazazi.”
Katika
eneo la Niger Delta, mtu mwenye pato la wastani huwa na bahati sana akijipatia
pauni moja kwa siku.
Lakini
Okon, ambaye zamani alikuwa anafanya kazi katika kampuni ya ujenzi, baadaye
anakanusha kwamba huwa anawatoza watu pesa kwa huduma zake. Anasema huwa
anapokea "mchango".
Baada ya
saa kadha za maombi na nyimbo, watoto hao watatu - wa miaka kati ya 10 na 15 -
wanalazimishwa kunywa majimaji ya rangi ya kijani kutoka kwa chupa ya soda.
Ndicho
kitu cha kwanza wameruhusiwa kula au kunywa baada ya kufunga kwa lazima kwa
siku tatu.
Okon
anasema ni mchanganyiko, wa maji, mafuta ya mchikichi (mawese), mchanga, majani
na tandu saba waliokaushwa na kusagwa kama unga.
“Mungu
aliniambia viungo vinavyofaa kuvitumia," anasema.
“Huwa ni
tofauti kwa kila mhusika.”
Ni baada
ya watoto hao kutapika, ndipo inapoaminika kwamba "wameponywa"
kabisa.
Mwisho wa waovu
Sekta ya
filamu Nigeria - ambayo hufahamika kama Nollywood - inaendelea kunawiri.
Huwa
inatoa filamu zaidi ya 2,500 kila mwaka, na kuifanya kuwa ya pili kwa kuzalisha
filamu kila mwaka baada ya Bollywood ya India.
Filamu
hizi kwa kawaida huwa katika makundi matano tofauti - za mapenzi, za ucheshi,
za historia, za uhalifu na ujambazi, na za “halleluyah” ambazo huwa na ujumbe
mzito wa kidini.
Unaweza
ukazitazama katika vituo vya kupumzikia, migahawa, baa na kwenye mabasi. Huwa
maarufu sio Nigeria pekee bali pia kote Afrika, na hata nje ya bara hili.
Evil
School (Shule ya Maovu), Family of Witches (Familia ya Wachawi), School of
Witches (Shule ya Wachawi) ni mifano tu ya filamu za hivi majuzi za Nollywood
ambazo zinawaonesha watoto wakiwa kama wachawi.
Iliyozidi
zaidi ni End of the Wicked (Mwisho wa Waovu), ambayo huangazia familia ya Amadi
ambayo huishi na bibi mzaa baba - ambaye tunagundua kwamba ni mwanachama wa kundi
la wachawi.
Watoto wa
familia hiyo wanashawishika kujiunga na kundi hilo la wachawi, na kwenye filamu
hiyo wanaoneshwa wakila nyama ya binadamu na kupanga njama ya kuwaua wazazi
wao.
Filamu
hiyo ya mwaka 1999 iliandaliwa na kanisa la Liberty Gospel Church, na miongoni
mwa waigizaji alikuwa kiongozi wa kanisa hilo Helen Ukpabio aliyeigiza kama
mchungaji ambaye kwa njia ya kishujaa anawafichua wachawi hao na kuwaangamiza.
Filamu
hiyo ilizua utata na, wakati huo, ililaumiwa kutokana na kuongezeka kwa visa
vya watoto kutuhumiwa kuwa wachawi katika miaka iliyofuata.
Ilishutumiwa
kwa kufunika mpaka kati ya maisha ya uhalisia na uigizaji. Sio tu kwamba
ilimhusisha mchungaji halisi ambaye alijiigiza mwenyewe, bali pia ilianza kwa
ujumbe kwamba ilikuwa sehemu ya msururu wa makala za ufichuzi.
Wanigeria
wenyewe wamezishutumu filamu kama hizo kwa kuendeleza dhana potofu kuhusu
maisha Nigeria kte barani Afrika.
Katika
sura kwenye kitabu kilichochapishwa majuzi kuhusu athari za filamu za Nollywood
katika utamaduni, msomi Françoise Ugochukwu anakariri mtazamo wa raia mmoja wa
Nigeria aliyekuwa akilalamika katika ukumbi mtandaoni.
“Filamu za
aina hii zimeeneza picha mbaya kuhusu Nigeria...na kulifanya lionekane kama
taifa linalotatizwa na ushirikina na imani na itikadi za kale," unasema
ujumbe mmoja katika jukwa hilo. "Haijatosha kwa mataifa ya Magharibi
kuzibandika tamaduni zetu sifa za kishetani, kwamba sasa tunajitendea hayo sisi
wenyewe?
“Kwa kweli
kuna mtu anayefikiria kwamba walichofanya mababu zetu ni kuketi tu siku zote na
kufanya matambiko ya kishetani?”
Mwanasheria
James Ibor anasema ni filamu kama vile End of the Wicked ambazo sio tu
zimeendeleza dhana kwamba watoto wanaweza kuwa wachawi, bali pia kwamba watu
wanaweza kuwa wachawi kwa kula chakula kilichotiwa nguvu za kichawi.
“Mtazamo
ulibadilika kutokana na kuanza kuenea kwa filamu za Nollywood miaka ya
1990," anasema. "Ingia katika duka lolote la filamu hapa, na uchague
bila kufuata utaratibu wowote filamu 50, na nakuhakikishia kwamba 80% kati ya
utakazozichagua zitakuwa zinazungumzia uchawi na juju."
Lakini
linaloshangaza zaidi ni kwamba moja ya sababu ya filamu za Nollywood kuwa
maarufu ni kwamba huwa zinatoa jukwaa kwa Waafrika kusimulia hadithi kuhusu
maisha yao wenyewe.
Mmoja wa
waandaaji wa filamu Nollywood, Orok Atim, anasema ingawa mada ya uchawi ni
mbaya, ni suala ambalo huathiri maisha ya watu wengi Nigeria - na hivyo basi
huwa wanatarajia kukutana nayo wanapokuwa wanatazama filamu za Nigeria.
Orok Atim
ameketi mbele ya 'madhabahu' yake ya muda, akiigiza filamu yake ya karibuni
zaidi.
Ingawa
filamu hiyo anayoiandaa ni hadithi ya mapenzi (pichani), Atim huwa anapenda
sana kuandaa filamu kuhusu mambo ya kiroho na ushirikina.
Filamu
yake itakayofuata itakuwa kuhusu rafiki yake ambaye kwa sasa ni marehemu
alivyokumbana na uchawi.
“Uchawi
upo katika jamii yetu hata wa leo," anasema. "Usipoonyesha
kinachofanyika katika jamii bado utakuwa unapoteza muda wako.
“Huwa
natumia filamu zao kuelimisha, kuburudisha na kuueleza ulimwengu kwamba uchawi
upo.”
Hakuna filamu
hata moja inayowaonyesha watoto bayana kama wachawi.
Atim
anasema filamu zake huwa zinawawezesha watazamaji wake Nigeria kukabili woga
walio nao, na si kuendeleza itikadi za kichawi na ushirikina.
Kwa
kutumia ubunifu wa kompyuta, filamu zake hufanya vitu visivyoonekana kuonekana;
na huwapa watu taswira au muonekano wa kitu cha kiroho ambacho huwa hakionekani
lakini huzungumziwa sana.
Na Atim
anapinga dhana kwamba filamu kama vile End of the Wicked zinachangia katika
kuenea kwa visa vya watoto kutuhumiwa kuwa wachawi.
“[Lakini
unachokisema ni] uvumi tu wa kutaka kuua filamu za Nollywood,” anasema.
"Hakuna mtu anaweza kutoa hadithi kuhusu mambo ambayo hayapo.”
Diana-Abasi
Udua Akanimoh, anayefanya kazi na shirika lisilo la kiserikali kwa jina Way to
the Nations katika jimbo la Akwa Ibom, anasema amejionea mwenyewe madhara ya
filamu hizo zenye mada za kichawi.
“Nilikwenda
katika kanisa moja hapa Eket na mchungaji alikuwa anazungumzia jinsi ya
kuwazuia mapepo wa baharini na uchawi," anasema. "Alianza kwa kuwaambia
waumini wake kwamba alikuwa ameyaona mambo kama hayo katika filamu aliyokuwa
ameitazama majuzi.”
“Kwa
hivyo, watu wasio na habari au wasiofikiria kwa undani watakuwa wanafikiria,
'Oh, iwapo mchungaji anasema haya, basi hilo lina maana kwamba ndio ukweli’.”
Akanimoh,
ambaye husimamia jumba salama ambalo ni kimbilio kwa watoto wanaotuhumiwa kuwa
wachawi, anasema ingawa filamu hizo sio chanzo hasa cha tuhuma hizo, bila shaka
hukuza na kuendeleza utamaduni unaotumiwa kutetea vitendo kama hivyo.
Na mfanyakazi
wa kijamii Ebe Ukara anadai kwamba "watu hutazama filamu hizi na kuiga
yale wanayoyaona manabii hawa wakifanya."
Ukara
alihusika katika kuokolewa kwa Comfort na ndugu zake baada yao kupigwa na nabii
huyo na kushambuliwa kwa panga.
“Filamu
siku hizi zinafunza mambo mengi sana ambayo watu hawakuyafanya zamani,"
anasema. "Kumpeleka mtoto kanisani ukampige - hilo halikuwepo.”
Lakini
waziri Oliver Orok anasema serikali haiamini filamu za Nollywood ndizo
zinazofaa kulaumiwa. Badala yake inaamini tatizo ni "itikadi za muda mrefu
za baadhi ya jamii”.
Kufukuzwa
Charity ni
mmoja tu miongoni mwa watoto wengi wanaoishi barabarani baada ya kutuhumiwa
kuwa mchawi.
Kwa miaka
miwili iliyopita, msichana huyu wa miaka 13 amekuwa akiishi kwenye kibanda
katika jaa la taka viungani mwa mji wa Calabar.
Ndani ya
kibanda hicho, wasichana wengine wanne wa umri karibu na wake bado wamelala -
hakuna godoro, na pia hakuna vyandarua vya kujikinga dhidi ya mbu.
Maisha ni
magumu, lakini siku nzuri ninaweza kujipatia Naira 1,500 ($4) kwa kutafuta
chupa za soda za plastiki na mikebe ya chuma inayoweza kutumiwa tena kutoka
kwenye jaa hilo la taka.
“Najihisi
vyema kuishi hapa," ananong'oneza Charity. "Kurejea kuishi katika
nyumba ya mjomba wangu itakuwa ni kama kujiweka motoni.”
Baada ya
babake kufariki dunia, alikwenda kuishi na mjomba wake.
Alipojaribu
kumnajisi, alituhumiwa na mke wake kwamba alikuwa amemroga.
“Walinifunga
mikono, na kutishia kunitupa ndani ya choo," anasema.
“Waliniweka
hivyo kwa siku moja," anasema. "Kwa hivyo, ilinilazimu kusema kwamba
nilikuwa mchawi ili wanifungue mikono."
Baada yake
"kukiri", mjomba wake aliacha kumpa chakula, na akaamua kutoroka.
Jaa la
Lemna ni makao kwa watoto wa mtaani mia kadha ambao hufahamika kama skolombo -
watoto kama Charity.
Wengi wana
hadithi zinazoshabikiana - walifukuzwa au wakatoroka nyumbani baada ya
kutuhumiwa kuwa wachawi.
Makundi
kadha yasiyo ya kiserikali Nigeria kama vile Basic Rights Counsel Initiative
(BRCI) na Way to Nations hujaribu kufanya zaidi ya kuwaokoa tu watoto waliotuhumiwa
kuwa wachawi - huwa wanajaribu kuwakutanisha tena na jamaa wale wale ambao
waliwatuhumu watoto hao kuwa wachawi.
Juhudi
kama hizo huwa nadra kufanikiwa, hata kwa jamaa wasio wa karibu sana.
Tukirudi
tena Calabar, James Ibor anakabiliwa na tatizo la afanye nini na Comfort na
ndugu zake wawili.
Wanataka
kuondoka kituo chake, lakini hakuna jamaa anayetaka kuwachukua.
“Tutawafahamishaje
taarifa hizi kwa watoto hao, kwamba shangazi zao na wajomba wao hawako tayari
hata kuwaona?" anasema.
“Watoto
hawa basi wakati huo wanaweza hata wakaanza kufikiria pengine kwamba ni kweli
wao ni wachawi.”
Shukrani:
Makala hii
ilifanikishwa kupitia ufadhili kutoka kwa Pulitzer Center on Crisis Reporting.
Mwandishi,
Mpiga picha & Mpiga video: Marc Ellison
Michoro:
Ozo Ezeogu (Comic Republic)
Tafsiri:
Abdalla Dzungu na Peter Mwai
Mwandalizi:
James Percy
Mhariri:
Kathryn Westcott
Imeundwa
kwa kutumia Shorthand
Picha zote
zina Hakimiliki
Comments
Post a Comment