WAKULIMA wa korosho katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wamepongeza juhudi za serikali
za kuwapelekea kwa wakati dawa za kupuliza mashamba yao na kwamba zimekuja
kipindi ambacho miti ya zao hilo inahitaji kutibiwa.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake kwenye uzinduzi wa kampeni ya
matumizi ya dawa za kutibu mikorosho uliyofanyika katika kitongoji cha Bawa,
mkazi wa kijiji cha Gezani, Mbwana Mwaroho aliishukuru
serikali kwa kuwaletea dawa hizo kwa wakati kwa kuwa kipindi hiki ndicho
ambacho mikorosho inaanza kutoa maua na wanahitaji dawa.
Mwaroho alisema suala la upatikana wa dawa limekuwa changamoto
lakini kwa sasa Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikileta dawa hizo kwa wakati.
Akizindua
kampeni hiyo Meneja wa Bodi ya Korosho tawi la Tanga, Ugumba Kilasa
aliwataka wakulima wa zao hilo kulima kisasa badala ya kuendelea na kilimo cha
mazoea ambao hauna tija.
Alisema kampeni hiyo itafanyika kwenye Wilaya za Mkinga, Pangani na
Muheza na kwamba lengo ni kuhamasisha matumizi ya dawa ili kukabiliana na
milipuko ya magonjwa ya miti ya mikorosho na hivyo kuwafanya wakulima kubadilisha
maisha yao kupitia zao hilo.
Aliwataka wakulima kutumia dawa kwa usahihi kwa maelekezo ya wataalamu hali
ambayo alidai kuwa itawanufaisha na kubadilisha maisha yao kwa kutumia kilimo.
Alieleza kuwa kwa kuwatumia wataalamu zao hilo litawabadilisha kimaisha na
hivyo kwenda sambamba na mpango wa serikali wa kumfanya mkulima kuwa na
maendeleo kwa kulima kitaalamu na kuvuna kwa wingi na gharama nafuu.
Kilasa alisema kuwa jumla ya lita elfu 20 za dawa ya maji na tani 60 za
dawa ya safa ya unga zimeshapokelewa na kwamba lengo ni kutaka zitumike muda
huu kwa kuwa ni kipindi cha mikorosho kutoa maua na ambacho wadudu waharibifu
hukitumia kuyashambulia.
Naye Mratibu wa zao la Korosho Wilaya ya Mkinga, Nzaro Kijo alieleza zoezi hilo
kuwa litafanyika katika mashamba ya mfano na kwamba dawa kwa ajili ya wakulima
zimehifadhiwa kwenye ghala la Gezani ambako matangazo na taratibu za
upatikanaji zimeshawekwa.
Kijo aliwataka wakulima ndani ya Kata 22 za Wilaya hiyo kutumia fursa
hiyo kutibu mazao yao ili kuyanusuru na magonjwa na kuongeza pato ambalo sasa
limeshuka kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa ya miti ya
mikorosho.
Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Korosho Mkoa wa Tanga,
Mashi Sopa aliwahakikishia wakulima wa zao hilo usalama wa mazao yao na kwamba
chama hicho kimejipanga kukabiliana na changamoto ya walanguzi wa korosho.
Comments
Post a Comment