Featured Post

UFISADI WA SASA UMEZIDI ULIOFANYWA NA WAKOLONI



NA MWANDISHI WETU
“Bara la Afrika twalilia ukombozi; Ukoloni mbaya na ubaguzi wa rangi; Mataifa hayo ya Ulaya ndio Afrika kuivamia; mababu zetu zamani walikataa; Ukoloni waliukataa; mabeberu walitesa. Ni vugumu kweli kusahau hayo waliyowatendea.”
Huo  ni wimbo ambao ulikuwa unatumika kama kiashiria cha kuanza kwa kipindi cha ‘Ukombozi wa Afrika’  kilichokuwa kinatangazwa na Redio Tanzania Dar es Salaam enzi hizo kituo cha redio kikiwa kimoja.

Ni katika kipindi hicho Balozi wa Tanzania kwenye Baraza la umoja wa Mataifa Dk. Salim Ahmed Salim, Waziri wa mambo ya Nje wakati huo John Malecela na wawakilishi wengine kutoka vyama vya ukombozi vya Afrika  walikuwa wakisikika wakielezea hali ya harakati za ukombozi wa Afrika na hususani nchi zilizokuwa zinatawaliwa kama Namibia, Zimbabwe Msumbiji, Guinea Bissau na harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Wawakilishi hao walinguruma kweli kweli hadi nchi hizo zilipopata uhuru wa bendera na kuondoka kwa wakoloni hao.
Baada ya uhuru wa nchi nyingi zoezi lililobakia mikononi mwa viongozi ilikuwa ni kuzijenga nchi zao kiuchumi ili kujipatia uhuru wa kiuchumi zikifuata mirengo tofauti ikiwemo ya ujamaa.
Lakini tofauti kubwa ilibakia kuwa nyingi ziliendelea kuwa tegemezi kwa nchi zilizokuwa zinazitawala katika nyanja mbalimbali na hata kufikia hatua ya kutegemea zaidi misaada kutoka kwao.
Lakini jambo lililojibainisha ni kwamba misaada iliyokuwa inatolewa na ambayo hadi hivi sasa inatolewa imekuwa inatia shaka kama inatumika  ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa namna moja au nyingine.
Aidha imekuwa inaonekana kuneemesha wale  wanaoipokea kwamba sehemu kubwa inashia mikononi mwa wachache na kuacha sehemu kubwa ya jamii ikiendelea kusota kwenye lindi la umaskini.
Lakini kinachoudhi zaidi ni kwamba miongoni mwa nchi nyingi umekuwepo ukwapuaji wa fedha zilizokusudiwa kwa  ajili ya maendeleo na hata  kudumaza miakakti ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Ukwapuaji huo ni wa rasilimali zikiwemo za maliasili na ndio maana Septemba 17, 2007 aliyekuwa Rais wa Benki ya Dunia, Robert Bruce Zoellick na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Ban Ki-moon walitoa taarifa ya pamoja kwamba wanaunda mfumo wa ushirikiano ili kusaidia nchi zinazoendela kuweza kuokoa raslimali (hususan madini na pesa) zinazoibiwa na kuhamishiwa katika nchi tajiri zilizoendelea.
Taarifa yao ya pamoja ilisema  kiasi cha rasilimali zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 40 huhamishwa kila mwaka na mafisadi katika nchi maskini na kupelekwa kufichwa katika nchi tajiri.
“Hakutakiwi kuwepo na sehemu salama kwa wezi wanaoibia maskini,” alisema Zoellick kwa Kiingereza, wakati akiwasilisha mpango huo na Ki-moon makao makuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.
Zoellick alisema inakadiriwa kuwa harakati za mafisadi, wezi, wa kimataifa na wakwepa kodi na watoa rushwa dunia nzima zinaleta hasara ya Dola trilioni moja hadi trilioni sita kila mwaka  kwa nchi zinazoendelea.
“Pesa hizo zinatosha kutokomeza umaskini”, alisema Zoellick na kuongeza kwamba Afrika ndio mhanga mkubwa wa ufisadi huo kwani wastani wa asilimia 25 ya pato la kila taifa (Dola bilioni 148) huporwa kifisadi na kuhamishiwa nchi zilizoendelea. 
Alisema kila Dola milioni 100  zinazopotea zingeweza kutoa chanjo kwa watoto milioni nne au kutoa maji safi ya bomba kwa kaya 250,000 au kugharimia dawa za kurefusha maisha kwa waathirika wa VVU na Ukimwi zaidi ya 600,000.
Mpango wa Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa tayari ulishaanza na unaitwa kwa Kiingereza: The Stolen Asset Recovery initiative (StAR). Unalenga kuziwezesha taasisi za fedha katika nchi zinazoendelea kufuatilia pesa zilizoibiwa na kuhamishiwa ng’ambo kwa njia za kifisadi kama wizi wa kughushi na ufuaji pesa haramu.
Ofisi ya Umoja wa Matifa inayopambana na mihadarati na uhalifu wa kimataifa iitwayo kwa Kiingereza UN Office on Drugs and Crime (UNDCO) ndio kinara wa mpango huo. Mkurugenzi wa UNDCO, Antonio Maria Costa aliasa kwamba mpango huo umekuja wakati shughuli za taasisi za fedha zinazidi kuwa tata kutokana na maendeleo ya teknolojia za habari na mawasiliano. 
Naye Ngozi Okonjo-Iweala, aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Nigeria wakati wa serikali ya Rais mstaafu Uluseguni Obasanjo (1999-2007) na ambaye katika utawala wa Rais mstaafu Goodluck Jonathan alishikilia wadhifa huo pia  alipongeza mpango huo kwa kusema utasaidia nchi kama Nigeria zenye mafisadi sugu.
Mwaka 2005 Ngozi Okonjo-Iweala aliiwezesha Nigeria kuokoa kiasi cha Dola za Marekani milioni  505 zilizoibiwa kifisadi wakati wa utawala wa Sani Abacha (1983-1998) na kufichwa katika benki za Uswisi.   
Mwaka 2006 Nigeria ilipokamilisha pambano la miaka mitano na kurudisha Dola milioni 500 toka Uswisi ilibainika kwamba Sani Abacha, alikuwa amepora  Dola bilioni tano kutoka Nigeria katika kipindi cha miaka yake ya utawala (1983-98).
Huko visiwa vya Philippines serikali zilizotawala baada ya kung’olewa Dikteta Ferdinand Marcos ulitumia miaka 18 kuweza kurudisha nyumbani Dola milioni 624 toka benki za Uswisi zilizokuwa zimefichwa na familia ya Marcos.
Habari za wanasiasa na wafanyabiashara mafisadi (au wala rushwa kabambe) kuibia nchi zao kuweka pesa zao katika benki zilizo nje ya nchi zao si mpya.
Viongozi madikteta na mafashisti waliowahi kutuhumiwa ni pamoja na Jenerali Manuel Noriega wa Panama (1983 -1989), Anastasio Somoza wa Nicaragua (1967-1979) na Hayati Jenerali Augusto Pinochet wa Chile (1973-1998).
Wengine ni Hayati Jenerali Mohamed Suharto wa Indonesia (1968-1998), Hayati Ferdinand Marcos wa Ufilipino (1965 to 1986), Joseph Estrada wa Ufilipino (1998-2001), Jean-Claude Duvalier (Baby Doc) na baba yake Francois wa  Haiti (1971-86).
Viongozi wa Afrika waliofanya ufisadi wa kutisha ni Hayati Joseph Mobutu Sese Seko wa Zaire (sasa D.R. Congo) (1965–1997) na  Hayati Jenerali Sani Abacha wa Nigeria (1993-1998).
Madikteta na mafashisti hawa walishirikiana na marafiki, jamaa na ndugu wa karibu kuibia serikali walizoziongoza na kufungua akaunti za siri. Pesa nyingine walizitumia kununua mali zisizohamishika na kufungua kampuni za siri katika nchi za ng’ambo.
Hapa Tanzania wananchi walishtushwa sana miaka ya hivi karibuni baada ya aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Miundombinu, Andrew John Chenge kutua Dar es Salaam akitokea China na kusema bilioni 1.5/= ziligunduliwa kwenye akaunti ya kificho ya benki moja huko visiwa vya Jersey, Uingereza ni “vijesenti”  na kwamba kila mtu ana viwango vyake.
Ingawa kauli ya Chenge ilichukiza wananchi wengi hususan makabwela lakini alisema ukweli ambao viongozi wengi wamekuwa wanaogopa kusema.
Chenge alionesha sura yake halisi mbele ya jamii tofauti na kundi kubwa la mafisadi, majambazi, mafuska na majangili wenye kuvaa ngozi ya kondoo wakati ni mbweha.
Hapa  kinachoweza kutokeza ni utata au usiri unaokuwepo kwa viongozi kutaja mali zao hii ina maana kwamba kusita kutaja mali huko kwa viongozi ni lazima kuna walakini ambao unaweza kuelezwa kuwa kuna mali wanazomiliki ambazo zimepatikana kwa njia zisizo halali.
Kwa tathmini makini, Chenge alichosema ni kwamba: “Jamani msione hizi pesa ni nyingi, wenzangu (wa viwango vyangu) katika utumishi Serikalini na akina “bangusilo” wao wana “viji-Shilingi”, “viji-Dola”, “viji-Pauni” na “viji-Yuro” kibao” katika benki nje ya nchi.
Hata kumbukumbu za Bunge zinaonesha wazi kwamba lugha ya Chenge ni ya “vijisenti”. Mfano ni majibu yake kwa Wabunge Februari 12, 2004 akiwa Dodoma:  “Niseme tu hapa Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina utajiri mkubwa sana wa madini. Kwa taarifa tu za utafiti uliofanywa, mkienda hapa Ofisi yetu ya Madini hapa, ukiomba wakuonyeshe geological data iliyopo kwa nchi nzima, utasema kweli tunachofanya sasa hivi ni kidogo mno.
“Lakini narudia kwamba Watanzania hatuwezi kuendelea kila siku tunasema, tuna potential nzuri sana. Hatuwezi kuishi kwa kula potential. Madini haya lazima tuyatafute kokote yalipo, tuyapate, tuyachimbue, tuyasafishe, tuya-process na kisha tuweze kuyauza na tutumie mafao yanayotokana na mauzo hayo kwa faida ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake...
“Lakini madini yaliyopo siyo madini ya dhahabu peke yake au almasi au vito, yapo madini mengi sana, madini ya vyuma, mkaa wa mawe na odium, unaweza kusema uranium na mengine yote mpaka kule maeneo ambayo yana madini mengi tunayafahamu lakini kwa leo mimi nasema tunaboresha maeneo haya...”
Chenge ambaye ameacha mabenki yote hapa Afrika na kupeleka “vijisenti” vyake huko Kisiwa cha Jersey, tena katika benki ya kificho  maarufu Off-Shore Bank kwa sababu za wazi anatoa kauli hiyo ‘nzuri’ kwa maana kwamba maliasili zinatakiwa zilete maendeleo.
Taarifa za uhakika zinasema sifa kubwa ya Off-Shore Bank ni “usiri wa chanzo cha mapato” na hifadhi ya majina ya wenye akaunti. Tena Off-Shore Bank hufunguliwa katika visiwa na wateja wake wengi ni wahalifu wa kimataifa, wafanyabiashara haramu kama kusafirisha mihadarati, silaha, magaidi na viongozi mafisadi.
Lakini likiangaliwa suala la rasilimali na mikataba ambayo imekuwa inaingiwa ni kwamba si ajabu unawawezesha wanaoingia mikataba hiyo  kujipatia ‘vijisenti’ ambavyo vitaendelea kuwaneemesha zaidi na wanakovihifadhi kunaweza kuwa ni huko huko kwa waliotiliana saini mikataba hiyo.
Katika hatua hiyo ni wazi kuwa ni dhahiri kuwa ukombozi uliokuwa unaliliwa na baadae kupatikana uhuru kukiwa na kilio cha kupinga kunyonywa na wakoloni hivi sasa imekuwa ni kunyonyana wenyewe  na katika mazingira mengine ukwapuaji unaofanyika unaweza kuhitimishwa na mtazamo, “Hata wakoloni hawakufanya ufisadi wa kiwango hiki kinachofanywa na viongozi walio wengi hivi sasa”.
Kutokana na mtazamo huo inaweza kujengeka dhana kuwa wanajamii walio wengi ndani ya Afrika leo wanaweza kuwa  viongozi wao wamevaa viatu vya utawala wa kikoloni. 


Comments