Featured Post

TFS: WATAKAOTUMIA NYUNDO BANDIA KUSHTAKIWA KWA UHUJUMU UCHUMI



NA TIGANYA VINCENT, RS TABORA
WAFANYABIASHARA wa Mazao ya Misitu wameonywa kuacha tabia ya kughushi kwa kutumia nyundo bandia kwa ajili ya kuweka alama kwenye magogo waliyovuna ili wasikumbwe na makosa ya uhujumu uchumi.

Onyo hilo limetolewa na Meneja Msaidizi wa Mipango na Matumizi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Magharibi, Anthony Mbugha, kwa wadau wa mazao ya misitu ambapo amewataka wawe waadilifu ili kujiepusha na makosa yanayoweza kuwasababisha wakashtakiwa kama wahujumu.
Alisema kimsingi nyundo zinazotumiwa na TFS zina alama tofauti na zile za kughushi ambazo baadhi ya watu wasio waaminifu wamekuwa wakitumia ambalo ni kosa.
Mbugha alisema kuwa, ni kosa kubwa kughushi nyaraka za serikali hata kutoa kopi na kwamba kibali cha usafishaji mazao ya mistu kinatakiwa kiwe halisi.
Aidha, Meneja huyo Msaidizi aliwaonya wafanyabiashara wa mazao ya misitu kuacha tabia ya kupasua magogo katikati ili yaonekana kama mabanzi kwa ajili ya kutaka kukwepa kulipia vibali na kodi mbalimbali wanazopaswa kulipa.
Alisema atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kama mfanyabiashara anayekwepa kulipia vibali na kukwepa kodi zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Msitu.
Mbugha alisema mabanzi mara nyingi yanajulikana na gogo lao linajulikana na kuongeza kwamba, ni vema wafanyabiashara wakaacha udanganyifu ili wafanye kazi zao katika mazingira yasiyo na mashaka.
Katika hatua nyingine, TFS imewataka wafanyabiashara hao wa mazao ya misitu kutoa taarifa Polisi pindi wanapotendewa vitendo ambavyo ni kinyume cha Sheria ya Mistu wanapokamatwa kwa kosa la kukutwa na mazao ya mistu ambayo hayana vibali.
Kauli hiyo imetolewa juzi na mjini hapa na Meneja wa Kanda ya Magharibi wa  TFS, Valentino Msusa, wakati wa mkutano wa siku moja wa wadau wa mazao ya misitu mkoani hapa.
Alisema kimsingi watu wanapokamatwa na mazao ya misitu ambayo hayana vibali wanatakiwa kupelekwa Polisi kwa ajili ya kuandaa taratibu za kuwapeleka mahakamani na siyo kupewa adhabu yoyote.
Msusa alisema, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiwapaka watumishi wa TFS matope bila kutoa ushahidi wapi walitendewa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na kuonyesha kama wameripoti Polisi.
Alisema vitendo vya kukwepa kodi na tozo mbalimbali zinazotokana na mazao ya mistu ni kuhujumu rasmimali za taifa kwa maslahi binafsi.
Aliongeza kusema kuwa, mwisho wa wafanyabiashara hao kutoa magogo yao msituni ni mwezi huu wa Agosti.
Alisema baada ya hapo Kikosi cha Doria kitaanza kupita katika maeneo yote ya misitu na kuwakamata wote watakaokutwa ndani na kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Comments