- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA TIBA ASILI YA MWAFRIKA TAREHE 31/8/2018 – DODOMA.
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Ndugu wananchi,
Maadhimisho
ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yalianza rasmi mwaka 2003 baada ya Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Shirika
la Afya Duniani Kanda ya Afrika kuridhia kuwepo kwa sherehe hizo.
Maadhimisho haya hufanyika katika nchi 46 za
kanda ya Afrika ambazo ni wanachama wa Shirika la Afya Duniani tarehe 31/08 ya kila mwaka na huu ni
mwaka wa 16 tangu maadhimisho haya yafanyike.
Ndugu wananchi,
Tanzania,
imekuwa inaadhimisha maadhimisho haya kwa malengo makuu manne. Kwanza ni kufufua ari na kujenga heshima ya huduma za
tiba asili ambazo kwa mujibu wa historia zimekuwa zikikandamizwa na
kudharaulika. Kuanzia wakati wa ukoloni hadi leo na kuzifanya tiba zetu za
asili na Waafrika wenyewe kuzinyanyapaa tiba hizo. Hali hiyo imetufanya tuyumbe,
tukose dira na mwelekeo katika suala zima la kuboresha Tiba Asili katika nchi zetu.
Pili
kwa kupitia maadhimisho Waganga wa Tiba Asili wamekuwa wakihamasishwa kujiepusha
na migongano katika jamii kwa kutohusisha ushirikina
na uchawi kama chanzo cha ugonjwa. Aidha, wataalamu wa tiba ya kisasa nao
wamekuwa wakihamasishwa kushiriki katika kuendeleza na kuboresha huduma za tiba
asili.
Tatu,
maadhimisho haya yanahimiza masuala ya uboreshaji wa dawa za asili na utengenezaji wa dawa hizo kiviwanda. Aidha,
utafiti endelevu wa dawa za asili kwa
magonjwa mbalimbali unahimizwa kwa madhumuni ya kupata dawa ambazo zinaweza
kupatikana kiurahisi ili mwenye kuhitaji
aweze kuzipata.
Nne,
kwa kupitia maadhimisho haya Waganga wa Tiba Asili wanahimizwa kufanya kazi zao
kwa kuzingatia maadili ya taaluma na huduma za afya.
Ndugu wananchi,
Katika
kuadhimisha Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika kila mwaka tunakuwa na ujumbe
maalum au kauli mbiu. Ujumbe maalum wa mwaka huu ni “Utengenezaji wa dawa za asili katika Afrika”
(Local manufacturing of traditional medicine products in the African Region).
Kauli
mbiu hii inalenga kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za asili nchini. Kauli
mbinu hii inaendana na mkakati waSerikali ya awamu ya tano inayohimiza uanzishwaji wa viwanda nchini. Kwa sasa
kutoka mwezi Oktoba mwaka 2017, vituo
vitatu vya uzalishaji wa dawa vilivyopo Dar es Salaam, Moshi na Arusha vilikaguliwa na kukidhi vigezo vya
kutengeneza dawa za asili. Vituo hivyo vitatu vimetengeneza dawa ambazo
zilikidhi vigezo vya kusajiliwa na Baraza
la Tiba Asili na Tiba Mbadala. Dawa hizo ni pamoja na: (1). Ujana; (2).
Sudhi; (3). IH- Myoon; (4). Apamol; na (5). Vatari. Dawa nyingine kumi za (1). Billyd Formular Power;
(2). Vission 2; (3). JC; (4). Fiwemu; na (5). 4A9; (6) Joy Natural Herbal (7) Mshana; (8). Life; (9). Detoxcer na (10).
Low oxygen zipo katika chakato wa kusajiliwa.
Aidha,
dawa za asili zilizosajiliwa na Mamlaka
ya Chakula na Dawa (TFDA) ni (1). Ravocream; (2). Mangifera cream; (3).
Morizella® juice sweet; (4). Morizella® juice (Sugar free); zinazotengenezwa na
Taasisi ya Madawa Asili iliyo chini ya MUHAS. Pia, Mansoordaya Chemicals Ltd
inayotengeneza dawa za (1). Ayu Koff; (2); Herbal health tonic na (3).Ayu DD syrup.
Pia,
hadi tarehe 30 Julai, 2018; waganga 19,141;
vituo 221 na dawa za asili tano
zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Nawashauri
Watengeneza dawa za asili kuzingatia Sheria, kanuni, miongozo na taratibu
zinazowasimamia katika kuhakikisha kuwa bidhaa zitengenezwazo zinakidhi
usajili. Aidha, mjiepushe na matangazo
yanayokizana na sheria, kanuni, miongozo na taratibu ikiwa pamoja na
matangazo ya dawa ambazo hazijafanyiwa uthibitisho kuwa ni salama.
Ndugu wananchi,
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatambua huduma za tiba
asili kuwa tiba rasmi kwa mujibu wa Sera ya Afya. Tanzania inayo mitidawa mingi
na mingi inatumika kutibu magonjwa mbalimbali. Pia ni ukweli usiopingika kuwa dawa nyingi za kisasa hutengenezwa kutokana
na mitidawa, na elimu ya mwanzo kabisa juu matumizi ya miti hiyo kutumika kama
dawa inatokana na waganga wa tiba asili. Tanzania ina rasilimali kubwa ya
mitidawa na wapo waganga wenye ujuzi katika hilo. Hivyo basi, ni vyema wataalam wa tiba ya kisasa na waganga wa tiba
asili shirikianeni kwa lengo la kuboresha na kuendeleza huduma na dawa za tiba
asili.
Kwa
kuzingatia ukweli huo, Serikali imekuwa na itaendelea kuhakikisha kuwa tiba
asili inaboreshwa na kuendelezwa. Kuanzia sasa vyuo vyote vya afya vya Serikali
vitakuwa vinawafundisha Waganga wa Tiba Asili kwa kutumia kitabu
kilichaandaliwa na Wizara ili kuwa na uelewa wa pamoja baina ya Wataalam wa
afya wa kisasa na waganga wa tiba asili. Kwa kuanzia vyuo vifuatavyo vitaanza;
(1). Chuo cha uuguzi Mirembe, (2). Chuo cha Waganga Wasaidizi Mafinga, (3).
Chuo cha uuguzi Njombe, (4). Chuo cha uuguzi Mtwara, (5). Chuo cha Waganga
Wasaidizi Kibaha, na (6). Chuo cha uuguzi Morogoro.
Ndugu wananchi,
Fomu za usajili zinapatikana katika Ofisi za Waganga
Wakuu wa kila Halmashauri nchini. Kila Halmashauri ina Mratibu wa Tiba ya Asili na Tiba Mbadala anayesimamia namna ya kufanya USAJILI wa mganga, kituo na dawa za
asili.
Nitoe
wito kwa Waganga na Wadau wa Tiba Asili kuzingatia Sera, Sheria, kanuni,
miongozo na taratibu zinazowasimamia katika kutoa huduma za tiba asili kwa
wateja wao. Aidha, nawataka waganga kujiepusha na matangazo yanayokizana na sheria, kanuni na taratibu
ikiwa pamoja na kuondoa mabango yaliyozagaa mitaani yanayoonyesha kuwa wanaweza
kutibu na kuponya magonjwa mbalimbali kwa mfano UKIMWI.
Pia,
Waganga wa Tiba Asili acheni kutumia vifaa msivyojua matumiazi yake kwa mfano
mashine za QUANTUM. Mnawadanganya
wananchi kuwa mnafahamu matumizi ya mashine hizo. Tuliishatoa maelekezo kwa
Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kutoa elimu kwa waganga wa tiba asili na
tiba mbadala. Sheria zilizopo zitumike kuhakikisha kuwa mashine za QUANTUM haziendelei kutumika nchini.
Ndugu wananchi,
Napenda
kuwakumbusha wananchi kwamba huduma za tiba asili zinatambuliwa kwa mujibu wa
Sera ya Afya na Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, Namba 23 ya mwaka 2002. Madhumuni ya sheria hiyo ni kusimamia,
kudhibiti na kuendeleza tiba asili ya Tanzania. Vilevile, udhibiti wa maadili
ya uganga na ukunga wa tiba asili nchini umepewa kipaumbele.
Kwa
mujibu wa Sheria hiyo, Baraza la Waganga wa Tiba za Asili na Tiba Mbadala
limeundwa kama chombo cha Serikali kitachosimamia na kuratibu shughuli za
usajili wa watoa huduma, wasaidizi wa watoa huduma, vituo vya huduma vya tiba
asili na dawa za asili. Ni muhimu kwa kila mdau wa tiba asili kuzingatia Sera,
Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu zilizowekwa, kuachana na matangazo
yasiyofaa, kuacha kuweka mabango hovyohovyo barabarani, matangazo katika vyombo
vya habari ni lazima yapate kibali cha Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Ahsanteni
Comments
Post a Comment