Featured Post

SHS. MILIONI 550/= ZA CAF ZAYEYUKA YANGA


Siku Yanga ilipocheza na Gor Mahia jijini Dar.


* Yalala 1-0 Kigali Rayon ikipenya hatua ya mtoano

NA DANIEL MBEGA
NDOTO za Yanga kuzoa Dola za Kimarekani 239,000 (takriban shilingi milioni 550) kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ziliyeyuka jana baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji Rayon Sport jijini Kigali, Rwanda.

Yanga ilikuwa inahitaji ushindi katika mchezo huo wa mwisho wa Kundi D la Kombe la Shirikisho ili ifikishe pointi saba na kushika nafsi ya tatu, ambayo ingeiwezesha kunyakua donge hilo.
Kunyakua fedha hizo kungeiwezesha Yanga kuondokana na ukata ambao umeisababisha timu hiyo kuyumba kwa kipindi kirefu sasa.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, timu ambayo inashika nafasi ya pili au ya tatu kwenye makundi anazawadiwa Dola 239,000.
Hata hivyo, timu hiyo sasa itaambulia Dola 150,000 tu (takriban shilingi milioni 345) kwa kule kufuzu kwenye hatua hiyo ya makundi.
Bao la Mrundi, Bonfilscaleb Bimenyimana la dakika ya 19 ndilo lililozima ndoto za Yanga kunyakua mamilioni hayo ingawa ilitawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa huku ikimiliki mpira kwa asilimia 54 kwa 46 na ikipiga pasi za uhakika kwa asilimia 77 dhidi ya 71 za Rayon.
Rayon sasa imefikisha pointi 9 na kushika nafasi ya pili nyuma ya vinara USM Alger ambayo jana iliitungua Gor Mahia kwa mabao 2-1 na sasa zinasubiri kupangiwa timu katika hatua ya mtoano ambayo ni ya robo fainali.
Kabla ya mechi za jana, Gor na USMA ndizo zilizokuwa na nafasi ya kusonga mbele kwa kuwa na pointi nane kila moja huku Rayon ikiwa na pointi sita na Yanga pointi nne, lakini bahati ikawaangukia Wanyarwanda ambao sasa wanakabiliwa na kibarua kigumu kuuendea ubingwa.
USMA iliogopa kutoka sare na Gor Mahia kwani ingeweza kujiweka katika mazingira magumu kufuatia ushindi wa Rayon, lakini mabao ya Mcongo, Prince Vinny Ibara Doniama dakika ya 36 na Amir Sayoud dakika ya 81, yaliihakikishia uongozi wa kundi hilo huku bao la Gor Mahia likifungwa na Jacques Tuyisenge dakika ya 83.
Yanga sasa wanarejea nyumbani Tanzania kuelekeza nguvu zao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kwani mwakani hawatashiriki tena michuano ya Afrika.
Na watakwenda moja kwa moja mkoani Kigoma kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Singida United Septemba 5 Uwanja wa Lake Tanganyika, kabla ya kupewa ratiba mpya ya mechi zao zijazo za Ligi Kuu.
Yanga ilifuzu katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kuitoa Wolaita Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1, ikiwa imeingia hatua ya mtoano baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Bingwa wa Kombe la Shirikisho ataondoka na kitita cha Dola 625,000 (zaidi ya shilingi bilioni 1.44) wakati mshindi wa pili atakusanya Dola 432,000 (karibu shilingi bilioni 1).

Comments