- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Sehemu ya watumishi wa Mgodi wa Dhahabu
wa MMG wakisikiliza maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini,
Doto Biteko (hayupo pichani) katika kikao chake na uongozi na watumishi hao.
Afisa Usalama wa Mgodi wa Dhahabu wa MMG,
Stephen Wambura akiwasilisha kero yake mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Doto
Biteko (hayupo pichani)
Sehemu ya raia wa kigeni waliokuwa
wakifanya kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa MMG pasipokuwa na vibali vya kazi
nchini.
Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa MMG uliopo
wilayani Musoma mkoani Mara.
…………………
Abaini raia wa kigeni 10 wasio na vibali vya kazi waliokuwa
wamejificha ndani ya mgodi
Atoa wiki moja mikataba ya ajira kwa wafanyakazi
Na Greyson Mwase,
Musoma
NAIBU Waziri wa Madini, Doto Biteko leo tarehe 29 Agosti,
2018 amefanya ziara ya kushtukiza katika Mgodi wa Dhahabu wa MMG unaomilikiwa
na kampuni ya Waarmenia uliopo katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara.
Mara baada ya kuwasili katika mgodi huo na kupata maelezo ya
namna ya uendeshaji wa mgodi huo kutoka kwa Meneja Uendeshaji, Sezgey Sazgyyan aliendelea na ukaguzi wa mgodi na kubaini ukiukwaji wa kanuni za usalama migodini ikiwa ni pamoja na
watumishi kufanya kazi katika mazingira
hatarishi pasipokuwa na vifaa vya
usalama mgodini.
Mara baada ya kutoa maelekezo, Naibu Waziri Biteko alifanya
kikao na uongozi wa mgodi pamoja na wafanyakazi wa mgodi huo lengo likiwa ni
kusikiliza kero mbalimbali pamoja na kuzitatua.
Akitoa maelezo kuhusu idadi ya wataalam wa kigeni na wa
kitanzania katika mgodi huo wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mgodi
huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 Afisa Utumishi wa mgodi huo, Rose Masanja alisema mgodi mpaka sasa una
wafanyakazi 126 wa kitanzania ambao ni pamoja na vibarua kutoka katika vijiji
vilivyopo pembezoni mwa mgodi na wataalam watatu kutoka nje ya nchi.
Mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Naibu Waziri Biteko
alimbana Masanja na kumtaka kutoa taarifa sahihi kuhusu idadi ya wataalam wa kigeni wanaofanya kazi
kwa kuwa taarifa zote anazo kiganjani mwake kabla ya kufanya ziara katika mgodi
huo.
Mara baada ya kauli ya Naibu Waziri Biteko, Masanja alieleza
kuwa kuna wafanyakazi wa kigeni takribani 10 wasio na vibali vya kazi na
wamejificha ndani ya vyumba na kuelekeza kwenye vyumba walivyojificha.
Naibu Waziri Biteko akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma,
Vicent Anney, Meneja Uendeshaji wa Mgodi huo, Sezgey Sazgyyan alielekea kwenye vyumba walivyojificha na
kufanya msako na kubaini watumishi wa kigeni wasio kuwa na vibali wamejificha
kwenye vitanda.
Aidha, Biteko alibaini baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo
waliokuwa wamefungiwa chooni kwa takribani masaa matatu na uongozi ili kuficha
aibu ya kutokuwa na vifaa usalama migodini.
Biteko alimwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Vicent Anney
kuwachukulia hatua za kisheria wafanyakazi hao ambapo bila kusita Mkuu wa
Wilaya huyo alielekeza Ofisi ya Wilaya ya Uhamiaji kufika muda huohuo
kuwakamata na kuwafikisha kwenye ofisi hizo kwa ajili ya kutoa maelezo.
Katika hatua nyingine, Biteko alisikiliza kero mbalimbali za
watumishi wa mgodi huo ambapo alielezwa kuwa watumishi wamekuwa wakifanya kazi
katika mazingira ya shida ikiwa ni pamoja na kukosa huduma zote muhimu kama
maji salama na matibabu.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake, Afisa Usalama wa Mgodi huo, Stephen Wambura alisema watumishi wa
kitanzania wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira yasiyo salama bila kuwa na
mikataba ya ajira na pale alipokuwa akiushauri uongozi wa mgodi kutatua
changamoto hizo alikuwa akiambulia matusi.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, tunashukuru sana kwa kufanya ziara
katika mgodi huu kwani tumekuwa tukifanya kazi kama watumwa huku tukikosa
huduma muhimu hali inayohatarisha usalama wa afya zetu,” alisema Wambura.
Naye Zuwena Swedi ambaye ni muuguzi wa kituo cha huduma ya
kwanza cha mgodi huo aliongeza kuwa amekuwa akifanya kazi katika mazingira
magumu ikiwa ni pamoja na kutopewa muda wa kutosha kupumzika hasa ikizingatiwa
kuwa ni mama wa mtoto mchanga.
Wakati huo huo akihitimisha kikao hicho, Naibu Waziri Biteko
alitoa wiki moja kwa uongozi wa Mgodi kuhakikisha umesaini mikataba na
watumishi.
Alisema kuwa Serikali inawakaribisha wawekezaji kufanya
shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini, hivyo wawekezaji
wanaowekeza nchini wanatakiwa kufuata sheria na kanuni za utafiti na uchimbaji
wa madini.
“Ni lazima wawekezaji wakahakikisha kuwa wanafuata kanuni na
sheria za madini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watumishi wa kitanzania
wanafanya shughuli za utafutaji na uchimbaji madini katika mazingira yaliyo
salama kwa afya na kupata stahiki zao kwa wakati,” alisisitiza Biteko.
Alisema kuwa, katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini
inaongeza mchango wake kwenye pato la taifa, serikali imeboresha sheria na
kanuni za madini ambazo zitakuwa na manufaa kwa watanzania na wawekezaji kutoka
nje ya nchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mara, Vicent Anney akizungumza katika
kikao hicho aliwataka watumishi wa mgodi kutoa taarifa zozote za ukiukwaji wa
sheria na kanuni za nchi na madini na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
ipo tayari kwa ajili ya kuwatetea.
Pamoja na ziara katika mgodi huo, Naibu Waziri Biteko
alifanya ziara katika machimbo ya wachimbaji wadogo yaliyopo katika eneo la
Ikungwi, Musoma Vijijini na kuwataka
wachimbaji hao kutotumia zebaki katika uchenjuaji wa madini.
Comments
Post a Comment