Rais John Magufuli akitoa heshima za mwisho katika jeneza lenye mwili wa King Majuto.
NA MWANDISHI WA BBC, TANGA
HATIMAYE mwili wa muigizaji wa vichekesho Amri Hamza Athumani
maarufu kama Mzee King Majuto umezikwa leo Ijumaa nyumbani kwake huko Donge, Tanga
nchini Tanzania.
Kabla ya kuuhifadhiwa kaburini, mwili huo ulisafirishwa juzi
usiku hadi Tanga ambapo ulisimamishwa njiani kuwapa mashabiki fursa ya kutoa
heshima zao za mwisho.
Dua ya kuaga mwili wa marehemu huyo aliyefariki Jumatano
usiku akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam
ilifanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Rais wa Tanzania, Dkt John
Magufuli.
Leo ibada ya mazishi ilianza mwendo wa saa sita mchana
katika Msikiti wa Nuruguda uliopo karibu na nyumbani kwake.
Baadaye mwili wake ulizikwa Kijiji cha Kiruku yalipo
mashamba yake nje kidogo ya Jiji la Tanga.
Mwili ulipowasili nyumbani kwa Mzee Majuto mwendo wa saa
moja unusu usiku jana, kuliibuka vilio huku wanawake wengi wakizimia.
Mwili ulisimamishwa katika vijiji 14 na mashabiki wakitaka
kutoa heshima ya mwisho.
Akiwa kama mfalme wa tasnia ya maigizo ya uchekeshaji nchini
Tanzania na Afrika Mashariki, Mzee Majuto aliweza kujizolea umaarufu mkubwa
kupitia namna ambavyo alikuwa akiigiza na kuwa miongoni mwa watu wenye mvuto
mkubwa miongoni mwa wasanii.
Afya ya Mzee Majuto ilizorota zaidi mwanzoni mwa mwaka 2018
ambapo awali alipelekwa nchini India kwa matibabu baada ya Rais wa Tanzania
John Magufuli na wapenzi wa sanaa ya Mzee Majuto kumchangia ili kunusuru uhai
wake kabla ya baadaye kurejea nchini Tanzania.
Awali alidaiwa kuugua ugonjwa wa henia na baadaye tezi dume.
Januari mwaka huu, Mzee Majuto alifanyiwa upasuaji wa tezi
dume katika Hospitali ya Tumaini jijini Dar es Salaam.
Kidonda cha upasuaji wa henia kiliendelea kumtatiza na
alilazwa kwa mara nyingine katika hospitali hiyo katikati ya mwezi Aprili.
Mei 4, mwaka huu mwigizaji huyo alisafirishwa kwenda India
kupata matibabu katika Hospitali ya Apollo, jijini New Delhi.
Juni 23, mwaka huu alirejea nchini Tanzania baada ya kupata
matibabu yaliyokuwa yakigharamiwa na Serikali na moja kwa moja alipelekwa
Muhimbili kwa ajili ya uangalizi kabla ya kuruhusiwa kuondoka na kisha
kurudishwa tena Julai 31 hospitalini hapo.
Historia yake ya
uigizaji
Wiki chache zilizopita taarifa za uongo za kifo chake
zilisambaa mitandaoni kabla ya familia yake kukanusha mara kwa mara.
Majuto aliyezaliwa mkoani Tanga kaskazini mwa Tanzania mwaka
1948 alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka tisa.
Amecheza kwa mafanikio makubwa kwenye tamthiliya kama vile
Mama Ntilie, Kondakta na nyinginezo nyingi zilizompa umaarufu mkubwa.
Kabla ya kifo chake tayari alikwisha wasamehe baadhi ya
waandaaji na wasambazaji ambao inasemekana walikuwa wakimdhulumu mamilioni ya
fedha baada ya waziri anayehusika na sanaa nchini Tanzania, Dkt. Harisson
Mwakyembe, kutishia kuwashitaki watu hao.
Atabaki kuwa nembo ya tasnia ya uigizaji wa vichekesho
nchini Tanzania hata baada ya kifo chake.
Risala za rambirambi
Rais Magufuli aliwaongoza Watanzania kutuma risala za
rambirambi.
Alisema King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na
wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo
alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi
za Chama na Serikali katika kuhimiza maendeleo.
"King Majuto alikuwa kielelezo cha safari ndefu ya
sanaa kwa nchi yetu, kwa muda wote amedhihirisha kipaji, ujuzi na uwezo wa hali
ya juu katika uigizaji na uchekeshaji na hivyo kuwa kipenzi cha Watanzania na
wasanii wenzake, hatutasahau ucheshi wake, upendo na uzalendo kwa nchi yake
wakati wote wa uhai wake," amesema Rais Magufuli.
Kiongozi huyo wa nchi alimjulia hali msanii King Majuto
alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Tumaini jijini Dar es Salaam Januari 31,
2018.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, ambaye pia
ni Mbunge wa Kigoma-Ujiji, Zitto Kabwe, amesema: "Nimepokea taarifa ya
msiba wa Mzee Majuto kwa masikitiko makubwa sana. Tumshukuru Mola kwa uwezo
wake na kuwaombea wafiwa kwa Mola awape subra."
Msanii maarufu wa Bongo Fleva Naseeb Abdul akijulikana zaidi
kama Diamond Platnumz, ameandika kuwa Mzee Majuto ni mfalme ambaye ataishi
mioyoni mwa wengi daima.
Msanii Ali Kiba naye ameandika: "Ewe Mwenyezi Mungu
hakika Mzee Wetu Amri Bin Athuman (King Majuto) yuko katika dhima yako na kamba
ya ujirani wako, basi mkinge na fitina ya kaburi na adhabu ya moto nawe ndiwe
mstahiki wa utekelezaji na ukweli msamehe na umrehemu hakika Wewe ni mwingi wa
kusamehe, mwingi wa kurehemu. Amin."
Comments
Post a Comment