- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA ALOYCE
NDELEIO
Wizi wa fedha za
umma pamoja na rushwa ni matendo yaliyosambaa katika taasisi nyingi za umma
nchini licha ya serikali kuwa na mikakati kadhaa ya kupambana na rushwa.
Katika
kudhihirisha hilo Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali katika
moja ya ripoti zake ilisema kwamba maofisa watatu waandamizi wa serikali katika
Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) wafunguliwe mashtaka kutokana na
kuingia mkataba wenye utata wa kukodi ndege ambao uliizamisha nchi kwenye deni
la dola milioni 41.
Hali hiyo
ilimaanisha kuwa furaha ambayo jamii imekuwa nayo hususani baada ya kuwasili
kwa ndege mpya iliyonunuliwa na serikali aina ya Boeing Dreamliner
787-8 haikuwa ni bure bali ni ishara ya kuona majeraha yalisababishwa na
baadhi ya watu yameanza kupata tiba.
Kukithiri kwa
rushwa kumesababisha kuwepo kwa mikakati si tu kwa Tanzania bali kwa
Afrika ambapo Jumatano iliyopita Julai 11 ilikuwa ni siku maalum
iliyotengwa na Umoja wa Afrika kuadhimisha mapambano dhidi ya rushwa.
Sikui hiyo
inatokana na maamuzi ya ya Mkutano wa Wakuu wa Nnchi za Umoja wa Afrika
uliofanyika Addis Ababa Ethiopia Julai3 hadi 7, 2017, kwa kutambua uzito wa
tatizo la rushwa na hivyo kuamua mwaka 2018 kuwa mwaka wa mapambano
dhidi ya rushwa
Tanzania
iliungana na nchi nyingine za Afrika kuiadhimisha siku hiyo maalum ya
mapambano dhidi ya rushwa kwa kutafakari athari za rushwa kwa maendeleo
ya taifa na kujipanga zaidi kupambana na kadhia hiyo.
Mikataba na
makubliano ya kimtaifa ya kuzuia na kupambana na rushwa ni mambo
yanayotambuliwa na Tanzania kuwa ni tatizo linalohitaji nguvu ya pamoja
kulikabili.
Kwa kipindi
kirefu sasa rushwa imechukuliwa kama utamaduni ndani ya jamii na
wamekuwepo watu ambao wamekuwa wakiendesha maisha yao kupitia ulaji
rushwa licha ya kuainishwa kuwa ni miongoni mwa maadui wakubwa wa maendeleo, na
wakiwa wanalitambua hilo.
Hata hivyo
wamekuwepo watu walio na ushauri kuhusu mienendo inayotakiwa ili kupambana na
mambo kama rushwa kwa kuwa madhila yake yanaeleweka kuwa si kwa mtu mmoja bali
ni kwa umma kwa ujumla.
Michelle Obama
ambaye ni mke wa Rais wa 44 wa Marekani, Barrack Obama aliwahi kuainisha baadhi
ya mambo ambayo Afrika inatakiwa kuwa nayo aliposema kwamba
inahitaji viongozi wanaofanya mambo sahihi hata wakati
wanapokuwa hawaonekani mbele ya macho ya wananchi, na kuongeza kuwa
inahitaji viongozi ambao watakataa kuvumilia mabaya wanayofanyiwa wengine.
Hata hivyo ili
kufanikiwa katika hilo alisema kwamba kunahitaji kuwa na msukumo wa
kimaadili na huo hauwezi kupandikizwa ndani ya mtu bali
unastawishwa kupitia uaminifu wa kuyatambua maadili.
Alisema,
“Kujadili mifano halisi ya maisha moja kwa moja kunaleta uwazi katika kuonesha
madhara ya rushwa. Miongoni mwa mambo ambayo yanamgusa moja kwa
moja binadamu kwa mfano ni masuala ya tiba. Hoja ni kwamba nani
atakayependa mama yake atibiwe na daktari ambaye alikuwa anafanya mambo
kwa kuhadaa alipokuwa akisoma?
“Hali hiyo
inamaanisha kuwa ili kupata huduma kwake ni lazima atakuhadaa mpaka
umpatie rushwa. Kwa hiyo ni gharama kiasi gani inatumika katika kuitafuta
rushwa pamoja na udanganyifu ndani ya jamii?
“Kama
tukiuvumilia udanganyifu hivi sasa miongoni mwa vijana je, ni kwa namna
gani tutaweza kusimama na kupambana na rushwa hapo baadaye?
“Kama unataka
kuongoza lazima uwe na msukumo wa kimaadili ulioufanya kumea na
kustawi ndani mwako, na hivyo kukuwezesha kuwafanya wengine
kuutafuta msukumo huo.”
Katika vipindi
tofauti vya uongozi wa hapa nchini kila awamu iliyoingia madarakani
imekuwa ikitangaza rushwa kuwa ni adui namba moja na kwamba mapambano
yataendeshwa kwa kutumia kila aina ya silaha kuitokomeza.
Hata hivyo kadri
muda unavyosogea rushwa imeenea na kuathiri kila sekta ya
uchumi. Rushwa imeongezeka kiasi kwamba imekuwa ndio aina au mtindo
wa maisha ya kila siku na kuwa jambo la kawaida katika jamii.
Mapambano dhidi
ya rushwa kwa Tanzania hayakuanzwa na utawala uliopo sasa licha ya kwamba
awamu hii inaonesha kuendesha mapambano hayo kwa nguvu kubwa zaidi na kufikia
hatua ya kulinganishwa na mapambano yaliyokuwa yakiendeshwa katika awamu ya
kwanza.
Lakini awamu zote
zilizotangulia zimechangia kwa kiasi kikubwa kupambana na rushwa
ambayo imekuwa ikisambaa kama saratani.
Miaka ya hivi
karibuni Taasisi ya Kimataifa ya Tansparency (TI) iliiweka Tanzania kwenye
kiwango cha asilimia 39.1 kwenye vidokezo vya rushwa kwa asilimia
100; lakini wachambuzi wa masuala ya rushwa waliona kuwa vidokezo hivyo
vilishindwa kutoa taswira halisi ya madhara ya rushwa katika maisha ya
kila siku kwa jamii.
Nafasi hiyo ya
Tanzania kwa vigezo vya CPI ilionesha kuwa ina afadhali kuliko Uganda na
imefanya vizuri kuliko Kenya.
Katika kupambana
na rushwa Serikali iliunda Tume ya Warioba ambayo ilichapisha
ripoti yake ambayo ilitathmini hali ya rushwa Tanzania mwaka 1996,
viongozi waliofuta walichukua mikakati mbalimbali kupambana na rushwa ikiwa ni
pamoja na kupitisha sheria ya kupambana na rushwa na kuanzisha taasisi za
kudhibiti hali hiyo.
Taasisi ya
Kupambana na Kutokomeza Rushwa (Takukuru) ilianzishwa ikiwa ni matokeo ya
mikakati hiyo. Kila awamu imekuwa ikifanya shughuli zake za
kupambana na rushwa na hata baadhi ya maofisa wa serikali wamefikishwa
mahakamani na kufunguliwa mashtaka kutokana na tuhuma za rushwa.
Umma kwa jumla
unaweza kwa kiasi fulani ukawa uliridhishwa na mapambano dhidi ya rushwa lakini
uhalisia ulionekana zaidi kwa watoa au wapokeaji rushwa ndogo kuliko
ilivyokuwa kwa wala rushwa kabambe.
Hata hivyo kwa
hivi sasa kumekuwepo na viashiria kuwa mapambano hayo yameanza kujikita kwa
wala rushwa kabambe na wakwapuaji mahiri.
Hali hiyo
inatokana na kile kilichojengeka kama utamaduni uliojikita ndani ya
jamii kwamba katika maisha ya kila siku ni mara chache watu hukwepa hali
hiyo kwani wanaona kuipokea rushwa ni kama sehemu ya utamaduni.
Kutoka kwa
wafanya biashara jijini Dar es Salaam hadi kwa hakimu Tabora, trafiki
Kilimanjaro, dereva wa basi Mwanza na mwalimu wa shule ya msingi Arusha
rushwa imekuwa ni janga kwamba imeshaathiri kila mmoja.
Mkazi wa Dar es
Salaam yuko radhi kutoa mlungula ili kupata matibabu ya upendeleo
anapotafuta huduma ya tiba. Analazimika kufanya hivyo kwa
sababu anaona ni kupoteza muda kufuata mlolongo wa kirasimu
uliopo katika hospitali za umma. Anapata dawa ambazo awali alielezwa hazipo.
Hivyo mfano huu unatoa picha mbaya kwa nchi ambapo asilimia kubwa
wanaishi kwenye lindi la umaskini.
Kuna kila dalili
kwamba mwanga upo hivi sasa kwamba maadili yakizingatiwa suluhisho la kuwa na
jamii isiyosujudia rushwa na kuvikataa vitendo nuru ya ustawi katika jitihada
zake za maendeleo itakuwa inang’aa.
Comments
Post a Comment