Featured Post

MSHIKAMANO WA BINADAMU, MISITU NI WA KUFUNGAMANA, KUTEGEMEANA



NA ALOYCE NDELEIO
Usimamizi  misitu Tanzania  unajumuisha taasisi nyingi  kutokana na kutegemewa na kufungamanishwa pia na ufugaji wa nyuki na hivyo  kuwepo uzalishaji wa asali.
Serikali ina mawakala kadhaa ambao ni pamoja na Huduma za Misitu (TFS) Mbegu za Miti (TTSA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI), Chuo cha Misitu Olmotonyi (FTI), Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora (BTI), Chuo cha Viwanda vya Misitu, Moshi (FITI) na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF).
Moja ya mikakati ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika Bajeti yake ya mwaka huu 2018/19 ni maandlizi ya kupandisha hadhi Wakala wa huduma za Misitu Tanzania kuwa Mamlaka ya Misitu Tanzania.

Lengo likiwa ni kuimarisha usimamizi wa misitu ya asili inayomilikiwa na Serikali Kuu, Halmashauri za Wilaya na Serikali za Vijiji. 
Malengo mengi huwa na ufanisi kwa kuangalia mwenendo wa historia wa rasilimali.Historia  inaonyesha kuwa binadamu alikuwa anaishi kwenye maeneo  yaliyo na misitu.
Hilo ni jambo lisilopingika, lakini  muhimu ni kwamba katika maisha hayo chanzo kikuu cha mahitaji yake kilikuwa ni mazingira hayo yaliyokuwa yanamzunguka.
Hata hivi sasa kuna makundi ya wanajamii wanaoishi na kukusanya matunda kutoka misituni na hata kujipatia vyakula kwa kuwinda ndani ya mazingira yanayozizunguka ambayo ni misitu.
Licha ya kwamba binadamu ameshapiga hatua ya maendeleo utegemezi wake kwa misitu umekuwa mkubwa, kuliko  hata ilivyokuwa zama hizo za kale za kuwinda na kukusanya matunda katika misitu.
Jamii  inakabiliwa na changamoto kubwa hivyo kwamba binadamu anatakiwa kujenga taswira yake ya ubinadamu juu ya maliasili misitu.
Hali hiyo ni kutokana na sababu kuwa misitu imekuwa inampatia nishati, chakula na dawa pamoja na kuwa ndiyo chanzo kikuu cha malighafi nyingine za miti kwa ajili ya ujenzi na matumizi mengine.
Hata hivyo mchango wa misitu katika kilimo, uhifadhi wa bioanuai, kulinda vyanzo vya maji na kuboresha athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa ni mara chache zinaeleweka miongoni mwa jamii.
Umoja wa Mataifa  mwaka 2000 ulikadiria kwamba takribani watu bilioni 1.6  duniani kote ikiwa ni pamoja na jamii ya watu maskini angalau walikuwa wanapata chakula, mapato au mahitaji ya dawa moja kwa moja kutoka kwenye misitu.
Kati ya watu hao takribani milioni 70 ambao ni wenyeji wa maeneo yanayozunguka misitu walitegemea misitu kwa kiwango kikubwa kuendeshea maisha yao.
Jamii maskini za vijijini katika Afrika wanategemea misitu  iliyopo na hata hivyo mazao ya misitu na hususani magogo ambayo yamekatwa tu yanachangia kwa  asilimia mbili mauzo ya nje ya  nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hali kadhalika misitu imekuwa inazalisha wastani wa asilimia sita ya pato la ndani la ukanda huo kiwango ambacho ni mara tatu ya wastani duniani.
Nchi 18  za Afrika  zikiwemo Ghana na Cameroon ni miongoni mwa nchi  24  duniani ambazo zimekuwa zinategemea misitu kwa asilimia kumi au zaidi katika uchumi wake.
Japo wataalamu wa mazingira na makundi yanayopigia kelele kuhusu uhifadhi wa mazingira wamesababisha  mtazamo wa kimataifa kuingia kwenye  hali isiyo endelevu.
Hali kadhalika uvunaji usio halali katika nchi za Afrika ya Kati na Afrika Magharibi takribani nusu ya mazao yote ya mbao kutoka misitu ya Afrika inatumika ndani kama nishati.
Licha ya kupoteza eneo kubwa la misitu bado nchi  za ukanda huo zimekuwa si waagizaji wa bidhaa zinazotokana na mbao.
Mtazamo wa jamii kuhusu misitu asili kama hifadhi ya ardhi ambayo haijatumika na kwamba ni salama wakati hali inapokuwa mbaya haueleweki.
Mtaalamu wa masuala ya misitu Christian Lambrechts anasema, “Watu wanaitegemea misitu kwa ajili ya kupata mazao fulani ambayo hawawezi kuyanunua katika soko la aina yoyote ile …hawana fedha …hawawezi kwenda katika maduka ya dawa wanaingia misituni  kutafuta dawa hizo kutoka kwenye mimea.”
Matumizi  ya aina hiyo ya misitu ni jambo lisiloepukika katika maeneo  yaliyo na kiwango kikubwa cha umaskini  na hata hivyo hayasababishi  uharibifu  yanapokuwa ni matumizi endelevu.
Lakini idadi kubwa ya watu wanapoingia kwenye msitu  kwa ajili ya kupata chakula na nishati inakuwepo athari kubwa ya kupunguza au kudharau hadhi ya misitu.

Misitu ithaminiwe, si miti
Kubadilisha njia ambazo serikali na watu wanavyothamini misitu ni  muhimu kwa uhai wake. Japo soko linaweza kupima thamani ya mashamba ya miti na mipango ya kuotesha miti inayolenga kupata njia mbadala  za mbao na nishati ni sahihi kupima thamani ya misitu ya asili ambayo  imekuwa inatoa vitu mbalimbali lakini havionekanai kwenye thamani za  kiuchumi.
Moja ya manufaa ambayo hayashikiki au kuonekana na mfano  yanajidhirisha kutokana na uhusiano uliopo katika ya misitu na uchumi.
Chai ni moja ya mazao yanayolimwa kwenye ukanda wa Nyanda za Juu  Kusini mwa Tanzania ambako kuna mashamba ya zao hilo ambalo linaiingizia jamii mapato.
Lakini kwa kuangalia kwa kina mashamba ya zao hilo ni kwamba yapo katika eneo lililozungukwa na misitu ya asili, hii ni kutokana na  sababu kuwa chai huhitaji hali ya hewa ya unyevunyevu na joto la wastani  ili  iweze kumea vizuri na hali hiyo unyevunyevu inatolewa na misitu.
Kutokana na  hali hiyo  kurekebisha hali ya hewa, kukusanya na kutoa  unyevunyevu wakati wa msimu wa joto na ukame, misitu huwa inaunda mazingira  ya hali ya hewa  inayotakiwa kwa ajili ya mavuno bora ya chai ambayo inasindikwa katika viwanda vya ndani na hata  kuuzwa nje ya nchi.
Kwa misingi  hiyo ni kwamba kama hakuna misitu ni dhahiri kuwa hakutakuwepo mavuno ya zao la chai. Hivyo ikilinganishwa gharama ya kuhifadhi misitu na neema inayotokana na mashamba ya chai kunaweza kuzifanya fedha zinazopatikana kwenye mashamba hayo zitumike kuwekeza  katika uhai wa misitu na kutoa msukumo kwa miongozo ya Serikali  na udhibiti wa vyanzo vya  misitu.
Tanzania inategemea misitu kwa ajili ya nishati ya umeme. Zaidi ya asilimia 70 ya umeme unaozalishwa kwenye mabwawa vyanzo vya maji yake ni maeneo ya misituni.
Kutokana na hali hiyo inakuwa vigumu kukokotoa hasara inayotokana na  kupotea kwa misitu. Kama ni kuchukua misingi ya kulipia gharama  zinazotokana na huduma inayotolewa kutoka katika misitu basi sekta ya kilimo, nishati, maji na nyingine nyingi zingetakiwa kufanya hivyo.
Hali hiyo inaonesha dhahiri kwamba ipo haja ya kuwa na sekta au kitengo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi misitu; lakini misitu inapoyumba au kupungua ndipo sekta binafsi na serikali hubaini kuwa huduma zilizokuwa zinatolewa na misitu hazipo tena, na haziwezi kupatikana bure, hivyo ni lazima zilipiwe kama huduma nyingine.

Jumuia zijijenge kimazingira
Ni dhahiri kuwa hakuna sekta binafsi inayoweza kulinda baadhi ya maeneo ya misitu bali sekta hizo zinaweza kuishauri Serikali mikakati mbalimbali ya kuhifadhi misitu.
Aidha maofisa wa misitu wanaweza kuwa na vidokezo muhimu  vinavyohusu maendeleo ya kiuchumi na misitu na hivyo Serikali kuwa inaungwa mkono na ngazi za juu za maamuzi katika nyanja husika.
Baadhi ya misitu hutoa aina mbalimbali za huduma na kutokana na hali hiyo ni muhimu kutafuta njia sahihi zinazoendana na uendelevu wa misitu.
Misitu  ya asili inahifadhi hewa nyingi ya kaboni, inaboresha hali  ya hewa vizuri zaidi na imesheheni aina nyingi na tofauti za bioanui  kuliko miti iliyooteshwa au maeneo ya misitu ambayo miti yake imeoteshwa upya.
Hata hivyo kuhifadhi upya misitu na biashara inayotokana na mazao ya misitu  ni muhimu katika kupata vyanzo mbadala vya bidhaa za mbao na kuwa na kinga kati ya binadamu na miti ya enzi za kale.
Hali hiyo inamaanisha kuwa watu wanaweza kuzalisha kiasi cha kutosha kutoka kwenye ardhi waliyo nayo na hivyo kuwa hawahitaji kuingia katika misitu kutafuta mahitaji kama hayo.
Hivyo wanaweza kuanzisha mipango ya kilimo-misitu katika ardhi yao na   hivyo kuboresha ardhi na huduma nyingine zinazopatikana katika ardhi wanayoitumia kwa ajili ya kilimo.

Comments