Featured Post

MSD MULEBA YAPELEKA HUDUMA ZAKE MKOANI GEITA



NA DOTTO MWAIBALE, MULEBA
BOHARI Kuu ya Dawa Tanzania (MSD) kituo cha Muleba  kimesogeza huduma zake za usambazaji dawa mkoani Geita ili kuwapunguzia safari ndefu ya kwenda kupata huduma hiyo Kanda ya Mwanza.
 
Hayo yalibainishwa juzi na Kaimu Meneja wa Mauzo wa Kituo cha Wilaya ya Muleba, Wasante Nyihirani wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wapo ziarani mkoani Kagera kuangalia taratibu za usambazaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye vituo vua kutolea huduma za afya mkoani Kagera.

"Zamani Mkoa wa Geita ulikuwa ukipokea dawa kutoka Kanda ya Mwanza lakini wadau wengine na serikali ikiona ni vema kuwasogezea huduma karibu ili kuwapunguzia gharama za usafiri na kupata dawa kwa wakati," alisema Nyihirani.

Alisema katika mkoa huo wilaya zilizonufaika na uanzishwaji wa kupeleka dawa 
mkoani Geita ni Wilaya ya Mbogwe DC na Bukombe DC ambazo nazo imekuwa zikitoa huduma katika maeneo mengine ya mkoa huo.

Alisema kuanzishwa kwa kituo cha mauzo cha Muleba kumewapunguzia mzigo Kanda ya Mwanza ambayo ilielemewa kwa vile ilikuwa ikihudumia mikoa ya Kagera na Geita.

Alisema kituo hicho cha Muleba hivi sasa kinatumia majengo ya Halmshauri ya wilaya hiyo ambayo yalikuwa yakitumika kama hospitali na kuwa MSD iliyafanyia ukarabati mkubwa kulingana na mahitaji yao.

Alisema katika majengo hayo wametenga eneo la kuhifadhia dawa baada ya kuzipokea, eneo la kuhifadhi dawa za kawaida, zilizokwisha muda wake, usambazaji kabla ya kwenda kwa mteja na eneo la kuhifadhia dawa zinazo hitaji baridi.

Nyihirani aliongeza kusema kuwa kituo hicho cha Muleba kina hudumia wilaya 10 nane zikiwa za mkoa wa Kagera na mbili za mkoani Geita.


Comments