Featured Post

MKUCHIKA ATAKA RUZUKU YA SERIKALI ITUMIKE VIZURI




NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imewataka wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Kilimanjaro kutumia vizuri fedha za ruzuku zinazotolewa na Serikali ili kuondokana na umaskini na hatimaye kuboresha maisha yao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni mstaafu George Mkuchika alipowatembelea wanufaika wa mpango huo katika Halmashauri za Wilaya ya Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Alisema amefurahi kuona wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Njoro  na Kileo katika wilaya hizo wametumia fedha za mpango huo kwa kujenga nyumba bora za kuishi, kuwanunulia watoto mahitaji muhimu ya shule ikiwa ni pamoja na kujishughulisha na ufugaji wa mbuzi, kondoo,kuku na bata.
Mkuchika aliguswa na jitihada za wanufaika wawili katika kijiji cha Njoro, Salome Athumani na Jumanne Muhamed Idafu na kuwapatia msaada wa fedha taslimu za kitanzania shilingi 300,000/= ili waweze kukamilisha ununuzi wa bati za kuezekea nyumba zao walizozijenga kupitia fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Pia Mkuchika alimpatia msaada wa fedha taslimu za kitanzania shilingi 200,000 Safiyuna Hasani wa kijiji cha Kileo ili aweze kumsomesha.
Mkuchika alisema kuwa Serikali ina lengo la kuhakikisha inawasajili wananchi wote wenye sifa ya kunufaika na fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika vijiji vyote nchini na kuongeza kuwa mpaka sasa Serikali imefanikiwa kuwafikia wanufaika wa Mpango kwa asilimia sabini tu.
Kwa upande wa wanufaika, Bi. Salome alimshukru Mkuchika kwa msaada wa kifedha aliompatia .
Jumla ya kaya maskini 144 katika kijiji cha Njoro wilayani Same zimenufaika na fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa kupata kiasi cha shilingi 91,280,000, ambapo katika kijiji cha Kileo wilayani Mwanga kaya 197 zimenufaika kwa kupata shilingi 132,719,000.

Comments