- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA ALOYCE NDELEIO
MIONGONI mwa mikakati inayojionesha na kupewa kipaumbele na
serikali ni pamoja na kuhakikisha jitihada za kujinyanyua kiuchumi zinakuwa na
ufanisi ili kuondokana na utegemezi wa misaada.
Hali hiyo ni pamoja na kuzitumia rasilimali zilizopo
nchini kuinua uchumi pamoja na
kuanzisha nyenzo za kuufanya uchumi huo
uwe endelevu ka kuwa na uchumi wa viwanda.
Lakini hoja moja
inafanya au kuonesha kuwa jamii ilisokomezwa katika usingizi kwa
kutegemea misaada na papo hapo wanaotoa misaada
kuwa na upeo unadhihirisha kuisoma jamii namna ambavyo inajiendesha.
Hoja ni kwamba hivi Tanzania ya leo ingekuwa katika hali
gani kama wahisani wanaoipa misaada toka ipate uhuru wasingekuwepo? Swali hili
na mengine ambayo yamekuwa yakiuumiza vichwa vya watu linatokana ‘kilio’ ambacho kimetolewa hivi
karibuni na viongozi waandamizi wa serikali.
Wahisani nao kwa kugundua matendo yanayofanywa na nchi kuwa
hayana tija waliamua kuikatia Serikali misaada ya shilingi trilioni moja kutokana na kashfa ya
IPTL pamoja na kitendo cha fedha kuchotwa katika Akaunti Maalum ya Tegeta
Escrow, zaidi ya sh bilioni 200, zilizohifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hali hiyo ilisababisha serikali kusema, “Hawa wahisani mara
nyingi wamekuwa na sababu mbalimbali na hata huko nyuma walishawahi kufanya
hivyo, lakini safari hii wanasema wamekata misaada yao kutokana na kashfa ya
IPTL na wanasema wanasubiri ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), ije, hili ni jambo linalonisononesha sana kwa sababu uamuzi huo
utaathiri watu wengi.”
Hoja inayoibuka hapa ni kwamba machungu ya kutegemea
misaada hapo ndipo yanapoanza kuonekana. Hadi miaka ya karibuni
ilifahamishwa kuwa toka mwaka 1961 Serikali za Tanzania [Bara na Zanzibar]
zimeomba, kupokea na kutumia mikopo na misaada toka nje ya nchi inayozidi jumla
ya Dola za Kimarekani bilioni 20 (zaidi ya Shilingi milioni 26,000).
Hiyo ni taarifa ya utafiti uliofanywa na wataalamu watatu
waandamizi katika Benki ya Dunia ambayo inaonesha kwamba katika kipindi cha
miaka 26 tu (1970-1996), Tanzania ilipewa jumla ya dola milioni 16,632
(shilingi 21,621.6 bilioni) na wafadhili mbalimbali wa nje. Fedha hizo ni zaidi
ya asilimia 80 ya jumla ya mapato yote ya Tanzania ya fedha za kigeni kwa kipindi
hicho.
Mtiririko wa misaada na mikopo kwa Tanzania ulikuwa
unaongezeka kutoka dola milioni 37.7 mwaka 1970 hadi kufikia dola milioni 1,158
mwaka 1992 na kushuka tena kidogo hadi dola milioni 830 mwaka 1996, inasema
ripoti hiyo.
Inakadiriwa kwamba kati ya 1970 na 1980, Tanzania ilikuwa
inapata misaada (sio mikopo) mingi kupita nchi yoyote miongoni mwa nchi
zinazopokea misaada ya Jumuiya ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Kiuchumi na
Maendeleo iitwayo kwa Kiingereza Organization for Economic Co-operation & Development
(OECD). Kamati maalumu ya OECD inayogawa misaada ilitaarifu kwamba Tanzania
ilikuwa inapata asilimia 8.3 ya jumla ya misaada yote ya OECD katika kipindi
hicho cha muongo mmoja (1970-80).
Tunaarifiwa kwamba utafiti wa wataalamu hao wa Benki ya Dunia
ulifanywa katika nchi 10 za Afrika zilizopata uhuru takribani miaka 50
iliyopita na ambazo zimepokea misaada na mikopo mingi ya nje. Nchi hizo ni
Tanzania, Uganda, Kenya, Zambia, Ethiopia, Nigeria, Ghana, Cote de’ Ivoire,
Mali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika mtazamo mwingine ni kwamba Tanzania imekuwa na
‘bahati kubwa ya kupendwa’ na wafadhili kwani hata wakati sera za serikali
kuhusu maendeleo zilipokuwa mbaya na kuwachukiza (1985-90), baadhi yao bado
waliendelea kuipa misaada.
Katika kipindi hicho Tanzania ilipata misaada zaidi ya mara
mbili ya ile iliyopewa Ghana ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa ndio nchi ya
Afrika inayosifiwa na wafadhili kwa kufanya vizuri mageuzi ya kiuchumi.
Kabla ya 1970, Serikali ya mwanzo ya Tanzania chini ya
Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa imefanikiwa kuvutia sana wafadhili wa nje na
kupewa misaada na mikopo mingi ili
kutekeleza sera zake za maendeleo chini ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kujenga nchi ya usawa na
msisitizo wake katika kujitegemea vilivutia sana viongozi wa nchi za Ulaya
Kaskazini (Scandinavia) waliokuwa wameegemea kwenye siasa za Ujamaa wa Kijamii
(Social Dermocrats). Hata kiongozi maarufu wa Ujeumani wakati huo Willy Brandt
na Waziri Mkuu wa Canada walivutiwa sana na Ujamaa wa Tanzania, inasema ripoti
hiyo.
“Benki ya Dunia ilizidisha mara mbili mikopo kwa Tanzania
kati ya 1973 na 1977 kwa sababu Bwana Robert McNamara aliyekuwa rais wake
wakati huo alikuwa anatekeleza sera ya ukuaji sawa kiuchumi iliyokuwa inashabihiana
na mikakati ya maendeleo ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Nyerere,” inasema
sehemu ya ripoti hiyo.
Hata hivyo, Benki ya Dunia na wafadhili wengine walianza
kupingana na sera za Ujamaa wa Tanzania ilipokaribia mwaka 1980. “Kulijitokeza
ushahidi kwamba licha ya mipango mizuri chini ya Azimio la Arusha hakukuwa na
mafanikio ya Ujamaa wala Kujitegemea na hivyo misaada toka nje ilikuwa
inafujwa,” inasema ripoti ya Watafiti wa Benki ya Dunia.
Misaada kwa Tanzania imekuwa inatoka katika nchi zipatazo 50
wakati mikopo mingi inatoka Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa
(IMF), Benki ya Maendeleo kwa Afrika (AfDB) na Umoja wa Ulaya (EU). Wafadhili
wakubwa wa misaada (isiyo mikopo) kwa Tanzania ni nchi nne za kaskazini mwa
Ulaya (Skandinavia) ambazo ni Sweden,
Norway, Denmark na Finland).
Nchi hizi zimetoa zaidi ya asilimia 30 ya misaada yote
iliyofika Tanzania kati ya 1970 na 1996. Sweden peke yake imetoa nusu (asilimia
15) ya misaada iliyotolewa na nchi za Scandinavia. Nchi hizo ndio zimekuwa na tabia
ya ung’ang’anizi wa kutoa misaada hata wakati sera za serikali zilipowachukiza
wafadhili wengine.
Wafadhili wengine wakubwa kwa Tanzania ni nchi za Ujerumani
na Uholanzi ambazo zimetoa asilimia nane ya misaada. Wafadhili wengine maarufu
ni Canada, Uingereza na Marekani. Nchi hizo zilitoa asilimia sita ya misaada
yote kwa Tanzania katika kipindi cha 1970 – 96.
Pamoja na nchi wafadhli misaada mingi kwa Tanzania imekuwa
inatoka katika Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNDP), Shirika la Umoja
wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) na asasi tanzu ya Benki ya Dunia (IDA).
Leo hii wahisani hao wameonesha makali yao na huenda ni kwa
kuona kuwa misaada inayotolew kuwa haiwafikii walenga. Hiyo ni sehemu tu
je, wakifunga milango kabisa tatasononeka kiasi gani?
Je, hatuwezi kutumia rasilimali zetu kujitegemeza badala ya
kutegemea hisani? Kama wahisani hao wanachukizwa na ukwapuaji mbona baadhi
wanaonesha kutochukizwa na hali hiyo?
Hapa ndipo panatakiwa kuzimuliwa kwamba tunaweza kutumia
rasilimali zetu na kujitegemea na kuachana na utegemezi wa misaada kwani
misaada hiyo ni nguo ya kuazima haiwezi kuisitiri nchi.
Comments
Post a Comment