- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI WETU
Iliporipotiwa katika vyombo vya habari kuwa gari la wagonjwa la
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime lililotakiwa kusafirisha mgonjwa kutoka
Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwenda Bugando jijini Mwanza, kukamatwa likiwa na
kilo 800 za mirungi ilionesha kuwepo vyombo vya umma vinavyotumika katika
uhalifu.
Gari hilo, lenye
namba DFPA 2955, inadaiwa kuwa lilikuwa likipiga ving’ora kama limebeba
mgonjwa. Hali hiyo inamaanisha kuwa bado baadhi ya wanajamii ni viziwi kwa
madhara ya dawa za kulevya na vikwazo kwa umma katika mapambano ya
kuzitokomeza.
Kwa ambao
hawazifahamu wanaweza kuchukualia taswira hii kwamba unapita mjini
au uko kwenye basi unaona mtu anachambua aina fulani ya
majani kama vile mtu anayechambua majani ya matembele lakini
baadhi ya sehemu anazitupa na nyingine anaweka mdomoni anatafuna.
Hali hiyo alikutana nayo mwandishi mmoja Abdullah bin
Abdul Kadir kutoka Malaysia mwaka 1854 alipotembelea Yemen na
kuona utamaduni huo wa ajabu wa kutafuna majani akasema, “Niliangalia
tabia hii ya ajabu katikati ya mji na kushangaa kila mtu anatafuna majani
kama mbuzi.”
Iwapo utaona tukio la aina hiyo basi ufahamu
kinachotafunwa ni aina fulani ya majani ambayo ni dawa za kulevya, ambayo
ni mirungi.
Mirungi ina majina mengi ambayo ni pamoja na Jaad
(Somalia), Miraa (Tanzania na Kenya); majina mengine ni pamoja na mbaga,
magoka, veve, gomba, na kashamba.
Inaaminika kuwa chimbuko la mirungi ni Ethiopia na
inaaminika ilisambaa na kuenea maeneo mengine ya milimani Afrika
Mashariki na Yemen. Wengine wanaamini kuwa ni Yemen na baadaye
ulisambaa na kuingia kwenye maeneo ya Ethiopia.
Kwa mujibu wa tathmini za kibotania inaelezwa
kuwa chimbuko ni Yemen na kutoka maeneo hayo ukasambaa hadi nchi za
Kenya, Somalia, Malawi, Uganda, Tanzania, Arabia, Congo, Zimbabwe, Zambia na
Afrika Kusini.
Abdullah bin Abdul Kadir alibainisha kuwa watu waliokuwa
wanatafuna mirungi hiyo baadhi walipokuwa wanatema mate yalikuwa ni
kijani akalazimika kuuliza, “Ni faida gani anayoipata mtu anapotafuna
majani hayo?”
Alijibiwa, “Hakuna anayejua…hiyo ni hali
tuliyoizoea Lakini ni jambo linalotugharimu, tumekua na kujikuta
tukiingia kwenye hali hiyo… lakini wale wanaotumia majani haya
wanalazimika kutumia siagi na asali vinginevyo wataugua.”
Kilimo
cha mirungi
Tabia ya kutafuna mirungi inaelezwa kuwa ni kama kutumia
kitu cha kuchangamsha mwili kama ilivyo kwa wanywaji wa kahawa na mara nyingine
majani yake hukaushwa na kutumiwa kwa kuchanganya kwenye chai.
Matumizi ya mirungi yamejikita maeneo ambayo
inalimwa kwa sababu ni majani mabichi tu ndiyo hutoa aina
hiyo inayodaiwa ‘kuchangamsha mwili’ kuliko majani makavu.
Kusambaa kwa mirungi Afrika Mashariki kunatokana na
kutengenezwa kwa miundombinu ambayo imewezesha na kurahisiha
usafirishaji wake kutoka nchi moja hadi nyingine.
Mirungi ni aina ya inayostawi kwenye hali ya unyevu nyevu
na milima yenye urefu kati ya mita 4000 hadi 9000 na kwa
upande wa Tanzania imekuwa inapatikana kwenye maeneo yenye uoto wa
asili katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga. Lakini kiasi
kikubwa cha mirungi inayotumika nchini inatoka nchi jirani ya Kenya.
Kilimo cha Mirungi ni maarufu nchini Yemen
na kimekuwa kinatumia sehemu kubwa ya ardhi
inayofasa kwa kilimo na inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya maji ya nchi
hiyo yanatumika kwa ajili ya kumwagilia mashamba yake na mazao
yamekuwa yanaongezeka kutoka asilimia kumi hadi 15 kila mwaka.
Matumizi ya maji ni makubwa hivyo kwamba maji ya
ardhini ambayo yanapatikana kwenye Bonde la Sanaa yanaelekea
kukauka, na kuwafanya maofisa wa serikali kufikia hatua ya kuwahamishia
wakulima wa eneo hilo ukanda wa pwani ya Bahari ya Sham.
Moja ya sababu za kuendesha kilimo cha
mirungi nchini Yemen ni mapato makubwa yanayopatikana kutokana na
kilimo chenyewe.
Baadhi ya tafiti zilizofanywa mwaka 2001
zinakadiria kuwa mapato yanayopatikana kwa kulima mirungi ni
takribani riale milioni 2.5 kwa hekta moja na kama matunda
yake yaklikusanywa huingiza kipato cha riale
takribani 570,000 kwa hekta.
Hilo limesababisha wakulima kuendeleza kilimo hicho
badala ya kilimo cha mazao mengine kama kahawa na matunda.
Kati ya mwaka 1970 na 2000 eneo lililokuwa
linalimwa mirungi liliongezeka kutoka hekta 8000 hadi hekta 103,000
na hayo ni makadirio tu kwani idadi halisi inaweza kuwa kubwa
zaidi.
Idadi ya Watumiaji
Inakadiriwa kuwa mamilioni ya watu ni watumiaji wa
mara kwa mara wa mirungi. Watumiaji wakubwa wanatoka nchi za Sudan
na Madagascar na katika eneo la kusini magharibi mwa Ghuba ya Arabia
hususani Yemen.
Nchini Yemen asilimia 60 ya wanaume na asilimia 35 ya
wanawake wanatumia mirungi na wamekuwa wanaitafuna kwa muda mrefu wa
maisha yao.
Kupigwa marufuku kilimo cha mirungi mara nyingi
limekuwa ni jambo linalopigwa vita na viongozi wa dini kwa kutumia
vigezo vya maandiko ya Koran kwamba ni
marufuku kitu chochote kinachodhuru mwili kutumiwa. Nchini Somalia
asilimia 61 ya watu wake wanatumia mirungi.
Watafiti wanakadiria kuwa takribani asilimia
70 hadi 80 ya raia wa Yemen wenye umri kati miaka 16 na 50 wanatumia
mirungi.
Miongoni mwa watafiti Dk. Ali Al-Zubaidi anakadiria
kuwa kiasi cha fedha zinazotumika ambazo zinatumiwa na
familia zimeongezeka kutoka reale bilioni 14.6 mwaka 1990 hadi
kufikia reale bilioni 41.2 mwaka 1995.
Watafiti pia wanakadiria kuwa familia
zinatumia takribani asilimia 17 ya mapato yake kwa ajili ya mirungi
(lakini idadi kamili inaweza kuwa zaidi).
Moja ya athari kubwa za kiuchumi ni kwa tabaka la
chini ambalo hujikuta likitumia fedha nyingi inazozipata
kununulia mirungi badala ya chakula.
Mapambano
dhidi ya mirungi
Marufukudhidi ya matumizi ya mirungi
hukumbana na vikwazo kwa mfano Somalia Baraza la Mahakama ya
Kiislamu ambalo lilikuwa linashikilia sehemu kubwa ya nchi hiyo
mwaka 2006 lilipiga marufuku matumizi hayo wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan
jambo lililosababisha upinzani mkubwa kwenye mji wa Kismayu.
Hali ikawa hivyo nchini Kenya Novemba 2006 wakati
serikali ilipopiga marufuku usafiri wa anga kwenda Somalia kutokana
na sababu za kiusalama hali iliyoibua upinzani mkubwa kutoka kwa wakulima
wa mirungi.
Kutokana na hali hiyo Mbunge wa Ntonyiri, wilaya ya
Meru Kaskazini alifahamisha kuwa ardhi ya eneo hilo
imekuwa inatumiwa kwa kulima mirungi na tani 20 zenye thamani ya
dola 800,000 zilikuwa zinasafirishwa kwenda Somalia kila siku. Hivyo
kupiga marufuku usafiri wa anga kwenda Somalia ilikuwa
ni kuharibu uchumi wa eneo hilo.
Ushindi kwa serikali ya mpito ikisaidiwa na majeshi ya
Ethiopia mwishoni mwa Desemba 2006 kulifanya biashara ya mirungi
kurudi kama kawaida katika barabara za Mogadishu japo wafanyabiashara wa
Kenya walisema kuwa biashara haikufikia kiwango
kilichokuwepo awali kabla ya kupigwa marufuku.
Kudhibiti
matumizi
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani mwa 1965 ya timu ya
wataalamu kuhusu kutegemea uzalishaji wa mihadarati ilibainisha,
“Kamati imefurahishwa kuona kuwa Azimio la Baraza la Uchumi na Jamii ni
vizuri matumizi ya mmea huo yakadhibitiwa.”
Kutokana na hali hiyo mirungi haikuwekwa kwenye kundi la
mihadarati lakini mwaka 1980 Shirika hilo liliweka matumizi ya
mirungi yanaweza kusababisha utegemezi wa kisaikolojia.
Madhara ya mirungi ni mengi lakini
baadhi yake ni matatizo ya kisaikolojia kama vile ukatili, mtu
anakuwa na tabia hiyo na jingine ni kukosa hamu ya kula.
Mtumiaji anaweza kukabiliwa na vidonda vya tumbo,
sanjari na vidonda mdomoni, kukosa choo kunakuambatana na kupungukiwa maji
mwilini.
Madhara mengine ni kukumbwa na shinikizo la
damu na kukosa hamu ya kufanya mapenzi, kupungua kwa nguvu za
kiume, mwili kuwasha, maumivu makali ya kichwa na kuharibikiwa kwa ini.
Mbaya zaidi mirungi husababisha mtumiaji kukosa
usingizi kwa muda mrefu hivyo kuongeza uwezekanowa kupata
ajali hususani kwa madereva wanaofanya safari za mbali na
wanafunzi kushindwa kuelewa masomo darasani.
Comments
Post a Comment