Featured Post

MAJALIWA: DAWA YA KUUA VILUILUI ITUMIKE KUTOKOMEZA MALARIA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa mikoa yote nchini waendeleze kampeni ya kutokomeza ugonjwa malaria kwa kutumia dawa ya kuua viluilui vya mbu.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Agosti 29, 2018) alipofanya ziara katika kiwanda cha kutengeneza dawa ya kuua viluilui vya mbu kilichopo katika wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Amesema nchi inakabiliwa na matatizo makubwa ya ugojwa wa malaria, hivyo ni vema viongozi wa mikoa wakatokomeza viluilui vya mbu kwa kuwa dawa inatengenezwa nchini.
Waziri Mkuu amesema kiwanda hicho cha Labiofam ni cha pekee barani Afrika kwa kuwa na uwezo wa kutengeneza dawa za aina hiyo.”Tutumie fursa hii kutokomeza maralia nchini.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kutumia vyombo vya habari  kwa kuandaa vipindi vya kuelimisha umma kuhusu dawa wanayozitengeneza.
Amesema wananchi wanatakiwa kuelimishwa juu ya umuhimu wa kutumia dawa hiyo kwa ajili ya kuua viluilui katika maeneo ya makazi yao ili kuutokomeza ugonjwa wa maralia nchini.
Naye,Meneja Uzalishaji wa kiwanda hicho, Bw. Aggrey Ndunguru amesema dawa zinazotengenezwa kiwandani hapo zina uwezo wa kuua viluilui vya mbu tu na haina madhara kwa binadamu.
Amesemma dawa hiyo ambayo ipo katika ujazo tofauti tofauti inaweza kuwekwa kwenye makaro ya vyoo, maji yaliyotuama pamoja na katika matanki ya maji ili kuua viluilui.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu alifuatana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarest Ndikilo na maafisa wengine wa Serikali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 29, 2018.

Comments