Featured Post

MAJALIWA AAGIZA, DAWA YA VIUADUDU VYA MAZALIA YA MBU ITANGAZWE ILI KUKUZA SOKO LA NDANI NA NJE



NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Kassimu Majaliwa ametaka kampeni ya kupambana na ugonjwa wa malaria iendane pamoja na kuitangaza dawa ya viuadudu vya mazalia ya mbu, inayozalishwa na kiwanda cha Tanzania Labiofarm Product Ltd, Kibaha mkoani Pwani.

Amesema hatua hiyo itasaidia  kutokomeza mazalia ya mbu na kupunguza dawa inayozalishwa kwa wingi kiwandani hapo.
Majaliwa aliyasema hayo ,mjini Kibaha alipotembelea kiwanda hicho, kuangalia uzalishaji na changamoto zinazokikabili.
Alielezea, bado dawa hiyo haijatangazwa vya kutosha hali ambayo inasababisha vita dhidi ya ugonjwa huo kuwa ngumu.
“Msisubiri viongozi wakuu waje ndio muwatumie, tumieni vyombo vya habari, kujitangaza na kutoa elimu juu ya dawa hii ambayo inaangamiza mazalio ya mbu,” alisema Majaliwa.
Alisema ,pia wanapaswa kutoa elimu kwenye taasisi za elimu kama vile shule za msingi,sekondari na vyuo ambako inaweza kutumika kwa kuwekwa kwenye maji ya kunywa kwenye matanki na visima.
“Mbali ya kusaidia wananchi na ugonjwa huo pia soko la ndani ni kubwa endapo kutakuwa na itaratibu mzuri wa kujitangaza kwani dawa hii inanunuliwa nje ila huku ndani soko bado liko chini ,” alisema Majaliwa.
Hata hivyo, Majaliwa alielezea, uwekezaji wa kiwanda huo ni mkubwa na ni umiliki wa serikali kwa asilimia 100 na hii inaendana na dhana ya nchi kuwa uchumi wa kati unaoendana na viwanda.
“Ugonjwa wa malaria hatari kwani ukienda kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati wagonjwa wengi ni wa malaria ,”
“Hivyo ni wakati wa kuweka mikakati imara ya kukabili ugonjwa huu hatari unaoua ” alisema Majaliwa.
Awali mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo alisema , vifo vilivyotokana na ugonjwa wa malaria ni asilimia 28.6 mwaka 2015 na mwaka 2016 vilipungua na kufikia asilimia 15.7 na mwaka 2017 vilishuka na kuwa asilimia 9.6.
Alifafanua, katika mapambano ya ugonjwa huo Mkoa wa Pwani ulitoa vyandarua 877,297 kwa kaya, mashuleni vyandarua 59,494 na kwenye kliniki vilitolewa vyandarua 48,120.
“Awamu ya kwanza halmashauri tisa za mkoa huo zilichukua lita 4,960 na awamu ya pili halmashauri zilizorudi ni mbili Kibaha na Rufiji zilichukua lita 80,000,” alisema Ndikilo.
Ndikilo alibainisha ,halmashauri Tisa zilinunua lita 2,320 na bajeti iliyopangwa kwa mwaka 2018-2019 zimetengwa milioni 181.2 kwa ajili ya kununua dawa hiyo na wafanyabiadhara wa Maili Moja walinunua lita 300 na kuzigawa kwa wananchi bure.

Comments