- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA
ALOYCE NDELEIO
DHANA
ya kukosoana ni jambo endelevu ndani ya jamii katika mambo yanayohusu ustawi
wake na nyanja inayoonekana kuwa na ukosoaji mara nyingi ni uwanja wa
siasa.
Mara
nyingi kunakuwepo kutofautiana katika dhana hii kutokana na upande mmoja kuuona
upande mwingine kuwa haufahamu jambo linalolengwa na mara nyingine kuonekana ni
kukiuka kanuni au kuipotosha jamii.
Inawezekana
kuwa kinachotokeza katika hali hiyo ni kutoonekana kwa hoja katika ukosoaji
au malengo ya ukosoaji huo yakiwa ni kudhoofisha mitazamo chanya inayoonekana
ndani ya jamii yenyewe.
Kimsingi
wanaoingia katika ukosoaji wamekuwa ni wawakilishi wa wanajamii na hivyo pale
ukosoaji unapokuwa haulengi mkondo chanya husababisha taswira
ya kuzigawa jamii.
Msingi
mama wa kukosoana ni kurekebishana, kusahihishana, kuelekezana na hitimisho
linalofikiwa ni kukubaliana hivyo kwamba yanayokosolewa kuingia katika
mkondo ulio sahihi, wenye tija na maridhiano kwa jamii yote.
Makubaliano yanapofikia
hitimisho sahihi huonesha uwepo demokrasia na mambo mengi yakiwemo
michakato, mipango na mikakati hufanyika kwa ufanisi na maendeleo hupatikana.
Mtazamo
kama huo ndio unaowafanya baadhi ya wanasiasa kusema kuwa kama hakutakuwepo
kukosoana iwe ndani ya vyama au taasisi kunasababisha uwepo usimamizi wa
kiimla katika chama au taasisi yenyewe.
Lakini
wapo ambao wanatumia kukosoana kujenga taswira ya kukashifiana ama baina ya
viongozi wenyewe au makundi ya wanajamii kutokana na kutofautiana kiitikadi.
Hilo linaibua uadui wa kifikra ambao unakwaza dhima nzima ya kuiletea jamii
maendeleo.
Katika
kuonesha kuwa kauli hizo zina ukweli ndani yake Baba wa Taifa Hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alisema katika Kitabu cha Maongozi , “Lakini
kuna mambo mawili ya lazima katika demokrasia; ukiyakosa hayo demokrasia
hakuna. La kwanza ni kwamba kila mtu lazima aweze kusema kwa uhuru
kabisa, na maneno ya kila mtu lazima yasikilizwe.
“Hata
kama mawazo ya mtu huyu hayapendwi kiasi gani, au walio wengi wanamdhania
amepotoka kiasi gani, si kitu. Kama mtu anapendwa kwa wema wake, au hapendwi
kwa visa vyake, hayo si kitu. Kila Mtanzania, kila mtu kijijini, kila mjumbe wa
Halmashauri ya wilaya, kila Mbunge n.k. lazima aweze kusema kwa uhuru
bila hofu ya vitisho – ama katika mkutano ama nje ya mkutano.”
Andiko
hilo lililotoka kabla ya mfumo wa vyama vingi linasadifu mazingira ya
sasa, ni mawazo endelevu ambapo aliongeza, “Watu wenye mawazo
tofauti, hata wakiwa wachache, lazima wawe na haki ya kutoa mawazo yao
katika majadiliano bila ya hofu ya kusumbuliwa; mawazo yao na
yashindwe katika hoja za majadiliano, sio kwa vitisho au mabavu.
“Majadiliano
yenyewe yatakayoleta uamuzi lazima yawape nafasi watu
kusema kwa uhuru kabisa. Na hata baada ya kuamua jambo watu
wawe na uhuru kuendelea kulizungumza jambo hilo.
“Maana
wale wachache wenye mawazo tofauti lazima wafahamu kuwa kama
wanayo mawazo yenye maana, na kama wakiyaeleza mawazo hayo vizuri,
wanaweza kubadili mawazo ya wale wengine walio wengi.”
Katika
ukosoaji ambao umekuwa unafanyika miongoni mwa wanasiasa walio wengi
uchache wa walio na mawazo hata kama yana maana umekuwa hauwekwi
kwenye mizania kuangalia tija yake, na kama ni kukubalika hakuwi ni moja
kwa moja kwani kufanya hivyo ni kumpaisha mkosoaji badala ya kumridhisha.
Kitabu
hicho kinaendelea, “Kadhalika wale walio wengi lazima wawe
tayari kuyashikilia mawazo yao mpaka wale wachache
waridhike kuwa uamuzi uliofanywa juu ya jambo lile ulikuwa sawa.
Majadiliano lazima yaruhusiwe kuendelea, kwa uhuru kabisa. Hiyo ni
sehemu ya maana ya uhuru wa mtu binafsi.”
Hata
hivyo alibainisha,“Lakini ile lazima ya uhuru wa mazungumzo haiwezi
kuzuia uamuzi kufanywa. Kuna wakati utafika mazungumzo
yakatike na kitendo kifuate; ama sivyo hatutafanya kazi yoyote ila
kubwata tu. Uamuzi ukishafanywa lazima ukubalike kuwa ni uamuzi wa watu wote;
na wote, hata wale waliokuwa wakipinga, hawana budi kushiriki
kutimiza jambo lile.
“Kwa
hiyo, jambo la pili katika demokrasia ni kwamba sheria
ikishapitishwa lazima kila mtu aitii sheria ile, pamoja na wale
walioipinga na wasiotosheka na hoja zilizotolewa
kutetea sheria ile. Isitoshe, mara sheria ikipitishwa kuikubali peke yake
hakutoshi, lazima kila mtu aitetee.”
Kukosoana
ni kuimarisha mshikamano ndani ya jamii kwa kuuweka katika mazingira sahihi,
licha ya kwamba walioegemea katika uhafidhina huwa na mawazo ya kiimla hivyo
kuwa vigumu kukubaliana na hilo kwani kwa kiwango kikubwa huwa
hawashauriki.
Lakini
wakati ukosoaji unapofanyika baina ya wanajamiii lazima kuangalia pia vigezo
vingine vikiwemo vya kitaaluma na kifundi ambapo wataalamu wa masuala ya
kitaaluma na kiufundi wanatakiwa kufanya mabadiliko, badala ya kudhani
kuwa wanafahamu vilivyo bora.
Hata
hivyo ni lazima wapambane kuelewa uhalisia wa watu maskini. Hilo
linawezekana kwa kuwashirikisha wanasiasa maswali hayo ili nao wayatafakari kwa
kuwa ni wawakilishi wao.
Ili
kupata suluhisho katika masuala ya kijamii makundi hayo lazima yawe tayari
kuwasikiliza, kufahamu uelewa wa watu maskini, vipaumbele vyao na shughuli zao;
baadaye watumie uelewa wao wa kiteknolojia kushughulikia yale yanayowakabili
maskini, iwe katika ngazi ya mitaa, taifa au ngazi nyingine ya juu.
Ni
lazima wajiulize kila mara ni kitu gani kinafanyika ndani ya kaya na jumuia,
hivyo kwamba sera kuu na ndogo ziwe zinapanga namna zitakavyoshughulikia
kuwasaidia wanawake, wanaume au watoto kuyaona matamanio yao. Ushiriki katika
sera za kupanga maamuzi ni lazima ziwe na msingi mpana.
Kujiuliza
maswali hayo kunaweza kutokana na hoja za ufafanuzi kutoka kwa maskini
ambapo wakati wanapozungumza kuhusu hali nzuri wanabainisha mitazamo ya
malighafi, kijamii, kimaumbile, kisaikolojia na kiroho, usalama na uhuru wa
kuchagua na kutekeleza.
Hali
ya aina hiyo inamaanisha kuwa pale ambapo kukosoana na kukubaliana
kunachangia ustawi wa jamii tofauti na mtazamo kwamba kukosoana na
kujengeana uadui.
Aidha
taswira inatakiwa kutoa dira chanya kwa kufanya pande zote kufungamana na
kufanikisha malengo ya kijamii katika mfumo wa demokrasia.
CHANZO: FAHARI YETU
Comments
Post a Comment