- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA ALOYCE NDELEIO
Michezo ya kuigiza licha ya kwamba haipo
kwenye mihtasari ya masomo mara nyingi inatambuliwa kama sehemu muhimu
inayowawezesha wanafunzi kuongeza uwezo wao wa kuelewa kutambua na hata kuwa na
kiu ya kufikiri zaidi.
Ukweli unabakia kwamba maendeleo
na mbinu za kijamii zinaweza kufikishwa kwenye hadhira yoyote
ile kupitia njia ya michezo ya kuigiza au tamthiliya.
Tamthilia zinawajumuisha wanafunzi kushiriki
kwenye kuchunguza na kutafiti masuala kupitia ushirikiano na muingiliano na
wengine na kushirki kwenye kuendeleza na kuwasilisha mawazo.
Aidha nyanja hiyo huwapa wanafunzi hususani
walio kwenye ngazi ya sekondari utambuzi na uelewa wa namna ambavyo sanaa za
maonesho kwenye ukumbi zinavyotumika kama njia ya mawasiliano na kujieleza.
Hali kadhalikaufanisi kwenye kufundisha kuigiza
kunasaidia kuibua shauku ya kupenda michezo na maonesho na hivyo
kuongeza ubora kwenye uzoefu wa kiutambaduni na kijamii.
Mahitaji ya kuwa na ufanisi kwenye stadi za
mawasiliano yamekuwepo kwa miongo mingi kutokana na kwamba kusoma na
kuandika kulishathibitisha ufanisi. Aidha kwa upande mwingine ni kwamba
maendeleo ya taifa katika kuzungumza na kusikiliza lugha ya taifa
kumekuwa na msisitizo kwenye umuhimu wa malengo ya matumizi ya lugha
yenyewe.
Kutokana na hali hiyo michezo ya kuiga
inakuwa na fursa ya kuwasilisha ujumbe na kuwafikia si tu wale wanaosoma
shuleni bali pia kwa wanajamii wengine kwenye ngazi zote za elimu na inatoa
fursa ya kuendeleza stadi zote hizo.
Malengo la elimu kwenye michezo ya
kuigiza
Michezo ya kuigiza shuleni
huchangia kwa njia tofauti maendeleo ya kijamii na mtu
binafsi kwenye kujifunza.
Katika hatua zote zile za mchezo hutoa
fursa kwa wanafunzi kuingia kifikra kwenye ulimwengu mwingine kwa
kuyachukua masuala mbalimbali na kutafiti uhusiano kutokana na mitazamo
ya watu.
Kwa upana zaidi ni kwamba elimu
inayotokana na michezo ya kuigiza shuleni inawapa wanafunzi fursa
za kuendeleza uelewa wao kwa kutafiti mwenendo, thamani na tabia, kujenga
uhusiano, ushirikiano kwenye kundi, kutafsiri na kuchambua, kuwasiliana na
kuwasilisha.
Kwa upande mwingine sanaa hii ya
kujieleza inamtaka mwanafunzi kujenga uelewa wao wenyewe na wengine
kupitia kuigiza, kujijengea ubunifu, kujenga mawazo ya kuwasiliana na
kushawishika kutumia lugha, kujieleza na mwenendo wa mazingira halisi na
ya ubunifu.
Aidha inalenga kwenye kujenga kujiamini
kwenye uhusiano wao na wengine na ungamuzi kwa wengine na kujenga stadi
na mbinu mbalimbali kupitia uigizaji.
Kama inakuwepo kozi hali ambayo inawahusu
zaidi wanachuo kutokana na mitaala ya shule za msingi na sekondari hapa
nchini kutokuwa na somo hilo kwenye mitaala yake huwezesha
mwanachuo kuyafikia malengo yake mahsusi.
Miongoni mwa malengo hayo ni pamoja kwa kutumia
zana, mbinu, stadi na vyombo vya habari na humtaka
mwanafunzi kuchunguza na kufanya majaribio kwenye uhusiano, mwendendo wa
kuajiri, kucheza, lugha, matumizi ya zana za kujifunza, sauti na mwanga.
Katika kuelezea hisia, mawazo, fikra na
suluhisho huwapa wanafunzi fursa ya kutoa michango na uhusiano
katika kutafiti tabia za binadamu kwenye mipangilio mbalimbali. Katika
mazingira ya ushirikiano ni lazima watashirikiana miongoni mwao wenyewe katika
kukubaliana na tafsiri na kuwasiliana na kuwasilisha.
Lengo jingine ni kutathmini na kutambua vema
ambako kunawapa wanafunzi fursa za kuangalia, kusikiliza na kutafakari.
Hali hiyo inawajenga kutambua mchango wao wenyewe na mchango wa wengine.
Hali hiyo pia inajenga kutambua ufanisi wa
kitaaluma na ridhaa na mchango wa vyombo vya habari. Wanafunzi huwa na msukumo
wa kutumia kile ambacho wameshajifunza wakati wanapokabiliana na masuala
mengine yanayotokana na uzoefu.
Katika hatua nyingine inaweza kuelezwa kuwa
tamthilia zinapoigizwa hutoa mchango maalumu na muhimu kwa mtu binafsi, kukua
kwa jamii pamoja na ukomavu wake.
Katika mazingira hayo ni kwamba tamthilia
hujenga uelewa wa mtu binafsi na wengine kupitia ugunduzi wa
uhusiano, kutumia lugha, mikakati na mbinu katika maonesho, ugunduzi wa hali na
thamani, uzoefu wa ubunifu, kufanya kazi pamoja na wengine, kujenga
uelewa wa msingi na kutoa msukumo wa kupenda na kufurahia tamthilia.
Kimsingi kwenye ubunifu ushiriki wa wanafunzi
huwezesha kuwa na mwitiko unaochochea uelewa na kutumia lugha sahihi na
mwenendo mzima wa tamthilia na kwa kufanya hivyo wanakuwa wamegundua uhusiano
uliopo katika mazingira wanayoishi.
Katika kuwasilisha wanafunzi hujikuta
wakishirikiana pamoja mazao ya kazi yao ya ubunifu pamoja na watazamaji
ambao wanakuwa wameingizwa kwenye shughuli za maonesho. Uwasilishaji ni kazi ya
kikundi lakini mchango wa mwanafunzi mmoja mmoja unaweza
kutambuliwa.
Kwa upande wa suala la maarifa na kuelewa
wanafunzi huweza kupata habari, uzoefu na kuzitambua stadi
zinazotolewa kupitia tamthilia.
Mifano ya tamthilia ambazo zimewahi kutumiwa
kwenye fasihi kwenye mihtasari ya masomo ya lugha kwa shule za sekondari
ni pamoja na Ngoswe; Penzi Kitovu cha Uzembe Kazini, iliyoandikwa na Eddi
Ganzel na Mashetani iliyoandikwa na Ibrahim Hussein.
Mfano katika tamthilia ya Mashetani kwa mtazamo
wa juu juu fikra inaweza kuwa ni kusoma mambo ya mashetani lakini undani wake
unaonesha jinsi mfumo wa kinyonyaji unavyokandamizi jamii wakati wengine
wakitumbua raha kutokana kwa kuzifaidi mali au rasilimali zinazostahili kuwa ni
za wote.
Fasihi andishi mara nyingi huwa na na mafumbo
ambayo yanahitaji upeo mpana wa kuelewa na hata hivyo inapoingizwa katika
maigizo katika tamthiliya huwezesha ujumbe unaowakilishwa kufika kwa urahisi.
Hapo ndipo mtazamaji au aliyewahi
kuisoma na kubakia akiwa na mawazo yanayoelewa hufumbuliwa upande
mwingine wa fikra na kuiona taswira iliyo sahihi kuwa ujumbe wake ulikuwa
unamaanisha au unalenga jambo fulani.
Kwa kusoma tu tamthiliya hizo inachukua muda
kupata ujumbe unaowasilishwa lakini kwenye maigizo inakuwa ni rahisi
zaidi kupata ujumbe huo na taswira inayowasilishwa na mwandishi kwa
jamii inaonekana wazi badala ya kuitafuta picha hiyo kwa kusoma tu.
Inaweza kuelezwa kwa lugha rahisi kuwa kuigiza
tatmthilia ni kusoma kwa vitendo kama inayokuwa kwenye masomo ya sayansi
ambako hufanyika majaribio baada ya kupata uelewa kwa njia ya
nadharia za somo husika.
Comments
Post a Comment