Featured Post

KING MAJUTO AFARIKI DUNIA


 
Rais Dkt. John Magufuli na mkewe Mama Janet walipomtembelea King Majuto wakati akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Muhimbili kabla ya kusafirishwa kupelekwa India kwa gharama za Serikali.


MSANII mkongwe wa vichekesho Amri Athuman 'King Majuto’ amefariki dunia jana usiku baada ya kulazwa siku chache zilizopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Taarifa za kifo chake zilianza kuenea baada ya mchekeshaji Lucas Lazaro Mhuvile, maarufu Joti, kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.
“R.I.P @Kingmajuto Umetuachia Maumivu Makubwa sana ktk Tasnia ya Comedy Tanzania Sisi wanao,Tutakukumbuka kwa kazi zako,Upendo wako,Tabasamu lako Daima milele,Tulikupenda sana ila Mungu amekupenda zaidi,Pumzika kwa Amani Mzee wetu,” aliandika Joti.
Muigizaji huyo alizaliwa mwaka 1948 jijini Tanga na kusoma shule ya Msambweni, Tanga, alianza kuigiza 1958 akiwa na umri wa miaka 9.
King Majuto alirejea nchini hivi karibuni akitokea India alikokuwa amekwenda kwa ajili ya matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa tezi dume katika Hospitali ya Apollo.
Mara aliporejea alipelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uangalizi
Kabla ya kupelekwa nchini India Mei 4, mwaka huu, King Majuto ambaye pia alikuwa akisumbuliwa na tatizo la nyonga, alilazwa katika Hospitali ya Tumaini jijini Dar, kisha akahamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Matibabu ya mzee huyo kwa kipindi cha takriban miezi miwili, yaligharamiwa na serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.





Comments