- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MOSES NG’WAT, KATAVI
HALI si shwari katika
Kijiji cha Kamalampaka, wilayani Mlele baada ya kaya zaidi ya 50 kukosa makazi,
kufuatia nyumba zao kuchomwa moto kwa
kile kilichoelezwa kuwa walivamia hifadhi ya msitu wa serikali.
Gazeti hili lilishuhudia wakazi hao waliokuwa wakiishi
katika kitongoji cha Katobagula kijijini hapo, wakiendelea na maisha chini ya
miti, huku watoto wakishindwa kuendelea na masomo yao.
Wakizungumza kwa masikitiko, wananchi hao walisema zoezi
hilo lililoanza Agosti 15, 2018 liliongozwa
na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) pamoja na watu wanaodhaniwa kuwa ni
askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Walisema mbali na nyumba zao kuchomwa moto na nyingine
kubomolewa, katika oparesheni hiyo baadhi yao wamepoteza idadi kubwa ya mifugo
kama ng’ombe na mbuzi, ikiwemo kuporwa chakula walichozalisha.
Mmoja wa waathirika wa oparesheni hiyo, Lushu Lutunga (64),
alisema ameshangazwa na hatua hiyo ya kuchomewa moto nyumba zake sita kwa madai
zilijengwa ndani ya hifadhi wakati ukweli ni kwamba yeye yuko nje ya alama za
mpaka.
“Nimelipa jumla ya shilingi milioni 12 baada ya kukamata ng’ombe
zangu 128, na sasa mimi na familia yangu tunaishi chini ya mti hapa kijijini na
hatujui hatima yetu,” alilalamika Lutunga.
Aliongeza kuwa, hadi sasa hajui hatima ya chakula
walichobeba jumla ya magunia 128 ya mpunga, pamoja na mahindi zaidi ya magunia
40 walichokuwa wamezalisha kwa ajili ya chakula na biashara.
Naye Malapala Matoboki, alieleza kuwa, jumla ya nyumba zake
kumi zilichomwa moto huku yeye akikamatwa na kuwekwa ndani kwa siku mbili kabla
ya kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa mawili ya kuvamia misitu na
kukata miti ambapo alitozwa faini ya shilingi 150,000.
“Kabla ya kuzingira nyumba yangu na kunikamata, niliuliza
kwanini viongozi wa kijiji huja kuomba michango ya maendeleo ilhali wanajua
naishi isivyo halali, nikatoa risiti ikiwemo niliyochangia mbio za mwenge mwaka
huu kwa kutoa ng’ombe mzima, lakini hawakunielewa,” alibainisha Matoboki.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Anthony Maganga,
alithibitisha kufanyika kwa oparesheni hiyo na kwamba jumla ya watu 500
wamefurushwa ndani ya eneo hilo.
“Ni kweli tumekuwa tukiomba michango ya maendeleo kutoka kwa
wakazi hao, lakini haimaanishi kuwa wakitupatia michango ndio wanahalalisha
uvunjaji wa sheria,” alisema.
Kuhusu baadhi ya wananchi kupoteza mali zao ikiwemo vyakula
vyao kuporwa, Mtendaji huyo wa kijiji alisema, hadi sasa hakuna mwananchi
aliyetoa taarifa katika uongozi wa kijiji.
Diwani wa Kata ya Inyonga kilipo kijiji hicho cha
Kamalampaka, Sudi Mlolwa, alisema baadhi ya wananchi wamefikisha malalamiko yao
na kwamba aliwaelekeza kuyapeleka kwa Mkuu wa Wilaya ili kutafutiwa ufumbuzi.
Aliongeza kuwa, tatizo la mipaka katika kijiji hicho ni
kubwa na tayari kupitia vikao mbalimbali wamewasilisha maombi ya kuongezewa
eneo kutokana na ongezeko la watu kijijini hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, alipoulizwa
juu ya tukio hilo alisema ndio anapokea taarifa hizo kwa mara ya kwanza na
kushauri suala hilo lizungumziwe na Mkuu wa Wilaya kwa kuwa ndiye Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Recho Kasanda, alipotafutwa hata wa
njia ya simu hakupatikana na taarifa kutoka ofisi yake zilieleza kuwa alikuwa
nje ya ofisi kikazi katika Halmashauri nyingine ya Mpimbwe.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Mlele anaongoza halmashauri mbili za
Mpimbwe na Mlele.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Ofisi ya Wakala wa Huduma
za Misitu nchini (TFS) Wilaya hiyo ya Mlele haikuwa tayari kuzungumzia suala
hilo licha ya mwandishi wetu kufika ofisini hapo.
Comments
Post a Comment