Featured Post

KASI YA UJENZI WA JENGO LA TRA PWANI HAIRIDHISHI -RC NDIKILO


Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo alipotembelea jengo la idara ya uhamiaji mkoani Pwani ambalo limekamilika kwa gharama ya bilioni 1.6(picha na Mwamvua Mwinyi).

Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo(kulia) alipotembelea ujenzi wa jengo la CRDB mkoani Pwani ambalo limekamilika kwa gharama ya milioni 900 , mbele kulia meneja CRDB Pwani Rosemary Nchimbi. (picha na Mwamvua Mwinyi
Jengo la mamlaka ya mapato mkoani Pwani ambalo linasuasua katika ujenzi wake ambao ulitakiwa kukamilika tangu june 2016 .(picha na Mwamvua Mwinyi)

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo la mamlaka ya mapato Tanzania, (TRA) mkoani humo, ujenzi ambao unasuasua kwa miaka miwili sasa na kubaki gofu.
Aidha amesema jengo hilo hadi lilipofikia halilingani na thamani ya sh.  1,653,267,510 ambayo ni awamu ya kwanza iliyofikia asilimia 61 hadi sasa.
Kufuatia hali hiyo, Ndikilo amemuelekeza meneja wa mamlaka hiyo mkoa, kumfikishia salamu kamishna wa mamlaka ya mapato makao makuu kufuatilia mradi wa ujenzi huo.
Mkuu huyo wa mkoa alieleza masikitiko hayo, wakati alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea maeneo ya ujenzi wa viwanja ya taasisi binafsi na serikali katika halmashauri ya Mji wa Kibaha, ikiwemo Uhamiaji, TRA na CRDB.
Alisema, lengo la kupewa viwanja hivyo ni kujenga maeneo hayo na sio kukumbatia viwanja bila sababu za msingi.
“Serikali ya mkoa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ilishatoa agizo tangu mwaka juzi kuwa maeneo hayo yote yahakikishwe yanajengwa na kama haiwezekani wanyanganywe wahusika na kupewa wengine wenye uwezo,” alisisitiza Ndikilo.
Ndikilo alishangazwa na kupewa taarifa pia kuwa ujenzi huo bado unahitaji zaidi ya milioni 200 wakati hatua ya kwanza haiendani na maelekezo ya serikali na mkoa.
“Gharama imesemwa itakuwa shilingi 2,693,402,120, ambapo mkandarasi Humphrey Construction Ltd, bado anahitaji fedha zaidi ambayo itafikia bilioni 2.8 jambo ambalo haliniingii akilini.”
“Kwanza mmeshaezeka mabati Leo hii mnaniambia mtaendelea na hatua nyingine ya ujenzi kwa ghorofa tatu ambapo mtaondoa mabati ambayo yameshagharamiwa halafu muongeze majengo tena, haiwezekani nitaagiza vyombo vyangu vya ulinzi na usalama vichunguze zaidi,” alifafanua Ndikilo.
Awali meneja wa TRA Pwani, Euvensia Lwiwa alisema jengo hilo lilitakiwa likamilike Juni 23, 2016, na ilipofika 2017 mkandarasi aliongezewa muda hadi Juni 2017.
Alisema, walisimamisha kazi ili kutafuta fedha za kuendeleza mradi kwa kipindi cha miezi mitatu Julai - Septemba 2017 suala ambalo limekwama kutokana na kukosa fedha.
Euvensia alielezea kuwa, kumekuwepo na mazungumzo kati ya mkandarasi, mshauri wa mradi na TRA kuhusu maelewano ya gharama za kumaliza mradi ambao bado upo chini ya mkandarasi.
Nae mshauri elekezi kutoka Alpha Architects Ltd ambaye pia ni meneja mradi, Fulgence Kibiki alisema, wamekwama kutokana na TRA kukosa fedha kwa wakati hali inayosababisha jengo kukosa ubora.
Akiwa kwenye ziara hiyo kwenye jengo la CRDB, meneja wa taasisi hiyo ya kifedha Rosemary Nchimbi alisema, jengo hilo ni la ghorofa moja na ujenzi unatarajiwa kugharimu sh. milioni 900.
Kwa upande wake, naibu kamishna wa uhamiaji ambae pia ni Ofisa wa idara ya uhamiaji Mkoani Pwani, Plasid Mazengo alisema jengo la uhamiaji limegharimu bilioni 1.6 na limeshaanza kutumika.

Comments