- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mkurugenzi wa Biashara wa kampuni ya
sukari ya Kilombero Sugar, Fimbo Butallah akizungumza na wananchi wa Mbagala
siku ya uzinduzi wa paketi ndogo za sukari ya ‘Bwana Sukari’ inayozalishwa na
kiwanda hicho. Paketi hizo zitauzwa kwa shillingi 500/- na shillingi 1000/-.
Mkurugenzi wa Biashara wa kampuni ya
Sukari ya Kilombero Sugar, Fimbo Butallah akizungumza na waandishi wa habari
siku ya uzinduzi wa paketi ndogo za sukari ya Bwana Sukari itakayouzwa kwa
shillings 500/- and shillingi 1000/-.
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Sukari ya Kilombero (KSC) imezindua paketi ndogo
za sukari yake ijulikanayo kama ‘Bwana Sukari’, ikiwa ni jitihada za
kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanamudu kununua sukari hiyo kutokana na
unafuu wake wa bei.
Paketi mpya za sukari chapa ya ‘Bwana Sukari’ zinapatikana
kwa ujazo wa gramu 350 maarufu kama ‘Robo Plus’ na paketi za gramu 160 maarufu
kama ‘Booster’.
Paketi za ‘Robo Plus’ zitauzwa shilingi 1,000/ kwa kila
paketi, na paketi za ‘Booster’ zitauzwa kwa shilingi 500/-kwa kila paketi.
Uzinduzi wa paketi mpya za ‘Bwana Sukari’ uliofanyika maeneo
ya Mbagala jijini Dar es Salaam ni sehemu ya mkakati wa kampuni ya KSC
kuhakikisha sukari yake inawafikia watanzania wa hali mbalimbali za kiuchumi.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka Bodi ya Sukari Tanzania (SBT),
Chama cha Wazalishaji wa Sukari Tanzania (TSPA), viongozi na wafanyakazi wa
KSC.
Akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi wa Biashara
wa KSC, Fimbo Butallah alisema kampuni ya sukari ya Kilombero imekua ikipanga
mikakati ya kuhakikisha bidhaa ya ‘Bwana Sukari’ inawafikia watanzania wengi
zaidi hapa nchini.
“Sukari ni moja ya bidhaa muhimu kwa matumizi ya kila siku
ya nyumbani na sukari ya Bwana Sukari ni moja ya sukari inayopendwa zaidi na
watumiaji wengi, tunawashukuru wateja wetu kwa kuikubali bidhaa yetu na
kuifanya ifanye vizuri sokoni, kuonyesha shukrani zetu tumeamua kuwaletea
paketi hizi ndogo ili wateja wetu wawe na uhuru wa kuchagua ujazo upi utawafaa
kwa matumizi yao,” alisema Fimbo.
Akiongeza kuwa, paketi mpya za ‘Bwana Sukari’ zitakidhi
mahitaji ya watumiaji wengi zaidi, “kwa mfano paketi za ‘Booster’ ambazo
zitauzwa kwa shilingi 500/-zitawafaa zaidi wale wanaohitaji sukari lakini kwa
wakati huo hawana uwezo wa kumudu kununua paketi kubwa au kwa wale wenye
familia ndogo.”
“Kwa ufupi, kupitia paketi hizi ndogo za Bwana Sukari
tunawapa wateja wetu uhuru wa kununua sukari ya ujazo mdogo lakini iliyofungwa
kwa hali ya usafi na usalama kabisa na kwa bei nafuu.”
Kwa kuanzia, paketi mpya za ‘Bwana Sukari ’zitapatikana
katika maduka yote ya rejareja mkoani Dar es Salaam na wilayani Kilombero
mkoani Morogoro wakati KSC inaendelea kufanya mikakati kuhakikisha bidhaa hii
inasambaa nchini kote siku za usoni.
Comments
Post a Comment