Featured Post

JOKATE MWEGELO: HUWEZI KUNISHUSHA CHINI KIRAHISI



NA MWANDISHI WA BBC
UNAPOSIKIA jina la Jokate Urban Mwegelo, akilini vinakuja vitu tofauti tofauti kwa kila anayemfahamu.
Yupo anayemfahamu kama mrembo aliyeshika nafasi ya pili katika mashindano ya urembo ya Miss Tanzania mwaka 2006 na kutwaa taji la Redds Miss Tanzania 2006.

Lakini mwingine atasema ni yule dada niliyemuona kwenye filamu za Kiswahili kutoka Tanzania, bado yupo atakayesema yule mwenye kampuni ya Kidoti, au aliyekuwa na uhusiano na Ali Kiba.
Mwingine naye atasema ni yule aliyekuwa anatangaza kwenye vipindi vya televisheni kama vile The One Show ya TV1 na Top Ten Most ya Chanel O.
Ni kweli Jokate ni mkuu wa wilaya pekee mwenye majina ama vyeo mbali mbali nchini Tanzania.
Kwa ufupi tu ni Mkurugenzi wa kampuni ya Kidoti, Mwanamitindo, mfanyabiashara, mshereheshaji, mwigizaji, mwimbaji, mtangazaji wa televisheni na kadhalika.
Baadhi wamekuwa wakitilia shaka uwezo wake wa kuhudumu katika wadhifa huo lakini mwenyewe anasema hilo halimnyimi usingizi.
"Huwezi kunishusha chini kirahisi, najiamini sana na kile Mungu amenipa, nafanyia kazi vipaji vyangu na nafanyia kazi taaluma yangu kwa nguvu zote na nina imani thabiti juu ya kile ninachokifanya kwa jamii yangu," Jokate anaiambia BBC.
Jokate aliteuliwa majuzi na Rais Dkt. John Magufuli kuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe iliyopo katika Mkoa wa Pwani, Tanzania.
Ni Mtanzania mwenye umri wa miaka 31. Alizaliwa Marekani mahali ambapo wazazi wake walikuwa wanafanya kazi. Lakini amesoma elimu ya msingi, sekondari na chuo kikuu Tanzania.
Waswahili husema, nyota njema huonekana asubuhi, alikuwa kiongozi tangu sekondari.
Akiwa katika shule ya Loyola Dar es Salaam, Jokate alipata nafasi ya uongozi na kuwa Dada Mkuu wa shule. Alipotoka shule akajiingiza katika masuala ya urembo.
Safari yake ya urembo ndiyo iliyozaa fursa mbali mbali katika uigizaji na kupelekea kupata Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike kupitia filamu ya 'Chumo' kwenye Zanzibar International Film Festival mwaka 2011, ambapo katika mashindano hayo hayo mwaka 2014, alipata Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike katika filamu za Kiswahili kupitia filamu ya 'Mikono Salama'.
Mbali na uigizaji, mwaka 2012 Jokate alifungua kampuni yake ya Kidoti Loving ambayo inajihusisha na bidhaa mbali mbali za urembo na hasa nywele.
Kampuni yake ilifanya vizuri sana na kuanza kuzalisha bidhaa zingine kama mabegi ya shule na ndala.
Mafanikio hayo yalipelekea mwaka 2017 Jokate kupata Tuzo ya Malkia wa Nguvu katika kipengele cha Ubunifu wa Biashara. Na mwaka huo huo alitajwa kuwania Tuzo ya Mjasiriamali wa Mwaka katika Tuzo za Africa Youth Awards.

Baadhi wanajiuliza anaweza kuongoza?
Jokate ana Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa na Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na ameingia katika siasa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa mmoja wa vijana wa UVCCM.
Baadaye alipata fursa ya kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM.
Jokate pia alikuwa miongozi mwa wanachama 450 wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA). Pamoja na kuchukua fomu hakufanikiwa kupata fursa hiyo.
Mwaka 2018 haukuanza vizuri sana katika shughuli zake za kisiasa kwani aliondolewa katika wadhfa wa kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM.
Na hii ni baada ya kuwapo kwa mzozo juu ya wadhifa huo tangu alipopata fursa hiyo.
Kupingwa kwake katika harakati za kisiasa si jambo geni, hasa baada Watanzania kuwa na maoni tofauti baada ya Jokate kutangazwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.
Wapo waliompongeza na walioona huwa hakustahili.
BBC imefanya mazungumzo na mkuu huyo mpya wa wilaya ya Kisarawe, ambaye anasema hasumbuliwi na wanaompinga.
"Binadamu tunatofautiana sio? Wapo ambao watafikiria A na wengine watafikiria B. Hatuwezi wote tukafikiria sawa sawa, ni maoni yao nayaheshimu lakini mimi najua Jokate Mwegelo ana talanta zipi, ana vipaji vipi na ana rekodi gani. Nadhani with time na wao watakuja kuelewa zaidi na watabadilisha maoni yao," anasema Jokate.
Hata hivyo, anaongeza kuwa ni Mungu tu ndiye anayemsaidia kumpitisha katika mapito mbali mbali ambayo ameyapitia na kumpa nguvu ya kuweza kupigana kila siku kwani akiona vijana wenzie wanavyo hangaika hujifunza na kutambua kuwa ni sehemu ya maisha.
"Maisha si lelemama, maisha si kwamba kila siku itakuwa ni chokoleti na pipi, kuna siku zingine itakuwa tafrani, lakini ndiyo sehemu ya maisha. Wanasema hakuna mafanikio bila changamoto," anaiambia BBC.
Je, unadhani ni wewe pekee huamini kama Jokate ameteuliwa na Rais kuwa mkuu wa wilaya? Si wewe tu, kwani hata Jokate hakuwahi kufikiria kama anaweza kuteuliwa na Rais.
Yeye alikuwa akiwaza nafasi zingine kama kuwa mwakilishi wa wananchi katika Bunge lakini si nafasi hiyo ya kuteuliwa ndani ya serikali.
Ataendeleza kazi yake ya uanamitindo na uigizaji? Jokate amezungumzia hatma ya harakati zake za uanamitindo, uigizaji na muziki.
"Dhamana niliyopewa ni kubwa na imani niliyoonyeshwa ni kubwa pia, na deni ambalo inabidi nililipe ni kubwa pia. Kwa hiyo niseme tu kwamba sasa hivi kipaumbele changu ni kutumikia wananchi wa Kisarawe, mengine yote yatafuata," ameiambia BBC.
Kama binti aliyekutana na vikwazo mbali mbali ikiwemo kukataliwa katika harakati za kisiasa anasema watoto wa kike wasikubali kuyumba, wajue kuna changamoto nyingi hasa ukiwa mtoto wa kike.
"Wengine hawataangalia vigezo ambavyo vinakufanya uwe kiongozi, wataangalia labda urembo wako, wataangalia au unavaa mavazi ya hivi, wataangalia historia yako. Wataangalia vitu ambavyo havina maana. Wataacha kuangalia vyeti vyako vya kimasomo, hivyo mabinti wawe thabiti," Jokate anasisitiza.
Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu walikuwa wakisambaza picha zake na video zake za zamani, hali iliyosababisha baadhi ya watu maarufu na hasa wanawake kupitia mitandao yao ya kijamii kukemea kitendo hicho.
Siku chache zilizopita Jokate alifuta picha zake zote katika mtandao wake wa Instagram.
"Ni mwanzo mpya na utawala mpya, ni mimi mwenye maamuzi, kuna vitu lazima uviheshimu ili uweze kufungua ukurasa mpya," Jokate ameiambia BBC.

Kuwatetea wanawake
Jokate ameonekana kujikita sana na masuala ya kuwatetea na kuwahamasisha wanawake.
Kipindi hiki ambacho ulimwengu unaadhimisha Wiki ya Kunyonyesha Watoto, ameandika ujumbe wa kuwahamasisha wanawake kuhakikisha wanawanyonyesha watoto wao.
"Muda na njia sahihi ya kunyonyesha mtoto maziwa ya mama, humpa afya, humfanya akue vizuri. Mama anayenyonyesha ale vyakula bora, kwa afya bora ya mtoto," ameandika kwenye Twitter.
"Nimewapongeza wamama wa @KisaraweMpya na wote Duniani kwa kujali afya za watoto. Karibuni Kisarawe."
Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu aliandika: "Siku ya wanawake duniani haipaswi kuishia kuwa ya matamasha au kuandika matamanio yetu ya namna mambo yanavyopaswa kuwa pekee. Tufanye kidogo tulichojaaliwa na kubadilisha maisha ya mmoja-mmoja."

Comments