Featured Post

JENERALI DAVIS MWAMUNYANGE ATEULIWA KWENYE TUME YA KUCHUNGUZA GHASIA ZA BAADA YA UCHAGUZI ZIMBABWE



HARARE, ZIMBABWE
MKUU wa Majeshi mstaafu wa Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, ameteuliwa na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, kuwa mjumbe wa tume ya watu saba itakayochunguza vurugu za baada ya uchaguzi nchini humo.
Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Kgalema Motlanthe, ataongoza tume hiyo inayotarajiwa kumaliza kazi yake ndani ya miezi mitatu.
Tume hiyo inatarajiwa kuchunguza kiini cha vurugu hizo ambazo zilipelekea vifo vya watu sita baada ya wanajeshi kuzima maandammano ya wapinzani siku mbili baada ya uchaguzi wa Julai 30.
Uchaguzi huo ambao umehalalisha urais wa Mngangagwa ulitazamiwa kuwa ni mwanzo mpya wa siasa za kidemokrasia tangu kung'olewa madarakani kwa Robert Mugabe Novemba 2017. Hatahivyo, kuingia kwa jeshi mtaani na kuwafyatulia risasi waandamanani kumezua mashaka juu ya mustakabali wa Zimbabwe.
Swali kuu zaidi ni kuwa wengi wametaka kujua nani hasa aliwaamuru wanajeshi kuzuia maandamano.
Jenerali Mwamunyange ambaye alikuwa Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 10 toka 2007 mpaka alipostaafu 2017 ndio mtu pekee katika tume hiyo mwenye usuli wa mambo ya kijeshi.
Mwanasheria kutoka Uingereza Rodney Dixon ambaye aliiwakilisha serikali ya Kenya katika kesi ya vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007 katika mahakama ya ICC, The Heague ni moja ya wajumbe wa tume hiyo.
Mjumbe mwengine kutoka nje ya Zimbabwe ni katibu mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Madola Chifu Emeka Anyaoku kutoka Nigeria.
Kutoka ndani ya Zimbabwe wajumbe ni Profesa Charity Manyeruke na Profesa Lovemore Madhuku kutoka Chuo Kikuu cha Zimbabwe pamoja na Vimbai Nyemba ambaye ni rais wa zamani wa chama cha wanasheria wa Zimbabwe.

Comments